Na CELINA MATHEW
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa juhudi zake za kufanikisha utekelezaji wa mradi wa soko la kisasa na stendi ya mabasi mkoani Bukoba, uliokuwa ukisubiriwa kwa zaidi ya miaka 10, lakini sasa unaendelea kutekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, alipofanya ukaguzi wa mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 18.9.
Amesema utekelezaji wa mradi huo unaonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kutimiza ahadi kwa wananchi, akibainisha kuwa fedha zinazotumika ni mkopo kutoka Benki ya Dunia na si msaada wa bure, jambo linalodhihirisha uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za maendeleo.
Aidha, Kihongosi amesema ameridhishwa na ubora wa ujenzi unaoendelea, huku akiwapongeza wahandisi, mkandarasi pamoja na vijana wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo.
Amesisitiza umuhimu wa kulipwa kwa stahiki za wafanyakazi kwa wakati na kuhimiza kuongeza kasi ya ujenzi licha ya changamoto za mvua.
Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi huo, Nixon Kissa, amesema utekelezaji umefikia asilimia 19.45 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2027.
Ameeleza kuwa mradi huo utakuwa na vizimba 1,848 pamoja na maduka 234, hatua itakayochochea ukuaji wa biashara katika mkoa wa Kagera hususan Bukoba.