Na NASRA KITANA
WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba amesema serikali inaendelea vizuri na maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 huku ikiendelea kukarabati na kujenga viwanja ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Arusha na Dodoma.
Pia imekamilisha ujenzi na ukarabati wa uwanja wa Meja Isamuhyo na Shule ya Sheria ya Tanzania kwa ajili ya mazoezi.
Dk. Mwigulu aliyasema hayo Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2026/27.
“Tanzania inaendelea vyema na maandalizi ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027, maandalizi hayo yanausisha ukarabati na ujenzi wa viwanja pamoja na miundombinu wezeshi ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Arusha na Dodoma.
“Uwanja wa Arusha umefikia asilimia 75, ukarabati wa uwanja wa Benjamini Mkapa umefikia asilimia 95 na ujenzi wa Uwanja wa Dodoma umefikia asilimia nne, vilevile serikali imekalisha ujenzi na ukarabati wa uwanja wa Meja Isamuhyo na Shule ya Sheria ya Tanzania kwa ajili ya mazoezi,” alisema Dk. Mwigulu.
Aidha Waziri Mkuu alisema kuwa serikali itaendelea na ujenzi wa viwanja vya Leaders, Farasi, Gymkhana na Anex.
Hata hivyo, Dk. Mwigulu alisema serikali itaendelea kusimamia na kuratibu ushiriki wa Tanzania katika michezo ya kimataifa na mandalizi ya AFCON 2027ili kuacha urithi endelevu wa michezo, ajira, utalii na heshima kwa taifa.
Pia, alisema serikali itaendelea kusimamia ushiriki wa wanafunzi katika michezo ili kuibua vipaji vyao.
Wakati huo huo, Waziri Dk. Mwigulu alizipongeza timu za Simba, Yanga kwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku Singida Black Stars na Azam FC kwa kufikia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Waziri Mkuu aliipongeza timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwa kufanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya AFCON 2025.
“Ni dhairi kuwa mafanikio katika michezo ya mpira wa miguu ni chachu ya kuchochea hamasa katika nyanja za michezo hapa nchini na Afrika, nawapongeza Simba na Yanga kwa mafanikio makubwa waliyofikia kuchora ramani ya mpira hapa nchini.
“Katika mwaka 2026/27 ni dhairi mafanikio katika michezo ya mpira wa miguu na michezo mingine ni matokeo ya uwekezaji na hamasa iliyokuwa ikitolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassani, siyo tu kuleta burudani kwa mashabiki bali kuongeza ajira na uwekezaji kwa vijana,” alisema Mwigulu.
Alifafanua kuwa Rais Dk. Samia alipoweka ‘goli la mama’ alichochea ushindani na hamasa kwa klabu za hapa nchini kupambana na kukuza soka la hapa nchini.
“Niwapongeze wawekezaji walioweza kufanya uwekezaji mkubwa katika michezo, kwani wamekuwa chachu ya maendeleo ya soka letu.
“Nalipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) na uongozi wake chini ya Rais Wallace Karia kwa uratibu mzuri wa mashindano mbalimbali hapa nchini lakini naipongeza Wizara ya Michezo chini ya Waziri wake Paul Makonda kwani kupitia wizara hiyo kwa mara ya kwanza Tanzania imefanikiwa kuingiza klabu nne katika hatua ya makundi ya mashindano ya kimataifa na timu ya taifa kucheza hatua ya 16 bora katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.




