• ePaper
Wednesday, April 22, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

SITAWAANGUSHA

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
April 22, 2026
in Habari, Kitaifa
0
SITAWAANGUSHA
0
SHARES
0
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na ATHNATH MKIRAMWENI

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema hatawaangusha mama na babalishe, kutokana na mchango wao mkubwa katika ukuaji uchumi wa nchi.

Amesema kundi hilo ni muhimu katika jamii, hivyo ataboresha kazi zao na kutatua changamoto zinazowakabili ili wafanye kazi kwa ufanisi na kujipatia kipato.

Rais Dk. Samia amesema hayo jijini Dar es Salaam jana baada ya kukagua mabanda ya mama na baba lishe walioshiriki Kongamano la Kitaifa la Baba na Mama Lishe lililobebwa na kaulimbiu ‘shiriki kulinda amani na  mshikamano wa taifa, amani ni hazina yetu mama na baba lishe’.

Amesema atashirikiana bega kwa bega na mama, baba lishe kuhakikisha wanafanya shughuli zao za kujipatia kipato katika mazingira bora na rafiki.

“Sitawaangusha, nitasikiliza changamoto zenu na kuzifanyia kazi,” alisema Rais Dk. Samia, alipozungumza na mama na baba lishe nje ya ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).

Akionekana mwenye furaha, Rais Dk. Samia amesema amekuwa karibu na mama na babalishe tangu wakati wa kampeni na baada ya kumalizika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, mwaka jana.

Rais Dk. Samia amewashukuru kumuunga mkono kwa kiwango kikubwa katika maeneo mbalimbali nchini wakati wa kampeni.

Amesema mchango wa kundi hilo ni muhimu na unastahili kuthaminiwa kwa sababu linalisha wananchi na kuwezesha shughuli nyingine za kiuchumi kufanyika kwa ufanisi.

MAAGIZO MATANO

Katika kuhakikisha kundi hilo linapata manufaa kiuchumi, Rais Dk. Samia, alitoa maagizo matano kwa wizara tano za kisekta akizitaka kuboresha mazingira ya utendaji wa mama na baba lishe nchini.

Rais Dk. Samia aliitaka Wizara ya TAMISEMI kutenga na kuendeleza maeneo rasmi ya kufanyia biashara kwa mama na baba lishe nchini ili wafanye kazi katika mazingira bora na heshima.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya maeneo hayo kwa kushirikiana na wawekezaji ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ufanisi zaidi.

Pia, aliagiza Wizara ya Nishati, kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza gharama za uendeshaji, kulinda mazingira na kuboresha afya za wahudumu.

Vilevile, aliitaka Wizara ya Afya kuimarisha utoaji wa elimu ya lishe na usalama wa chakula kwa mama na baba lishe, kulinda afya za walaji na kuboresha viwango vya huduma.

Jambo la nne, Rais Dk. Samia aliitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kushirikiana na taasisi zingine kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa mitaji kwa kundi hilo.

Pia, aliagiza Wizara ya Fedha kuweka mazingira rafiki ya kisera na kisheria kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kunufaika na huduma za kifedha.

AIDHINISHA JINA YA MAMA NA BABA LISHE

Katika hatua nyingine, Rais Dk. Samia alikubali pendekezo la kubadili jina kutoka “mama ntilie” na “baba ntilie” kwenda “mama lishe” na “baba lishe”  kuendana na hadhi ya kazi wanayofanya.

Rais Dk. Samia alisema serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria kuimarisha sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika uchumi.

KUHUSU DIRA YA MWAKA 2050

Rais Dk. Samia akizungumzia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050 alisema sekta binafsi itakuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa dira hiyo na kuitaka kushirikiana na serikali kuwawezesha mama lishe.

Alisema utekelezaji wa maendeleo ya taifa utafanyika kwa ushirikiano wa pande kuu tatu kuwa serikali itachukua sehemu ya utekelezaji kwa takribani asilimia 30, huku sekta binafsi ikipewa jukumu kubwa zaidi la asilimia 70.

Rais Dk. Samia aliongeza mashirika ya umma nayo yatakuwa sehemu ya mchakato kwa asilimia nane kwa  kushirikiana na serikali na sekta binafsi.

TUNZENI AMANI

Rais Dk. Samia  katika kongamano hilo, alisisitiza umuhimu wa amani kwa taifa na kusema amani ni hazina kubwa inayowezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku za kiuchumi na kijamii.

Alisema bila amani nchini, shughuli muhimu kama biashara, sherehe na huduma za kijamii hazitafanyika kwa utulivu.

Pia, aliwahimiza wananchi hususan mama na baba lishe, kuendelea kulinda na kudumisha mshikamano na utulivu wa nchi, kwa sababu mafanikio ya sekta zao yanategemea uwepo wa mazingira hayo.

“Kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki salama kuruhusu maendeleo endelevu kufikiwa,” alisema.

WAZIRI GWAJIMA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima alisisitiza umuhimu mkubwa wa kundi la mama na baba lishe katika uchumi wa taifa, kuwa wao ni mhimili muhimu wa sekta isiyo rasmi inayotoa ajira kwa maelfu ya Watanzania na huduma ya chakula kwa wananchi wa kada zote.

Alisema kuwa serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kupitia sera, mipango na programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha kiuchumi, ikiwemo urasimishaji wa biashara, upatikanaji wa mikopo nafuu, na uboreshaji wa miundombinu ya masoko.

Pia, kongamano hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha wadau, kubadilishana mawazo na kujadili changamoto na fursa zilizopo kwa mama na baba lishe nchini hivyo maoni na mapendekezo yaliyotolewa yataisaidia serikali kuboresha sera na mikakati ya maendeleo jumuishi.

UMALITA

Katibu wa Umoja wa Mama na Baba Lishe Tanzania (UMALITA), Julieth  Madata alisema Rais Dk. Samia ni kiongozi kipekee aliyeleta matumaini mapya kwa Watanzania.

Alisema uongozi wake umejengwa katika misingi ya hekima, uvumilivu na mshikamano wa kitaifa, hatua iliyochangia kuimarika uchumi, diplomasia na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Alisema Rais Dk. Samia ameonesha kwa vitendo mwanamke anaweza kuongoza kwa mafanikio makubwa na kuwa mfano wa kuigwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katika risala yao, mama na baba lishe waliomba msaada wa kitaalamu kutoka serikalini wa kuanzisha mfumo wa kidijitali utakaowaunganisha nchi nzima kupata masoko, mikopo na huduma za kifedha kwa urahisi.

Pia waliomba kuboreshwa masoko na vizimba vyao, likiwemo Soko la Kisutu jijini Dar es Salaam, eneo la Forodhani Zanzibar na kujengwa soko la kisasa Kigamboni litakalohudumia watalii na wananchi kwa ujumla.

Alisisitiza umuhimu wa kupunguziwa gharama za vizimba na kuwekwa mazingira rafiki kwa wafanyabiashara wote, wakiwemo watu wenye ulemavu, kupatiwa ofisi rasmi za umoja wao katika ngazi mbalimbali, kujengewa vituo vya kulelea watoto karibu na maeneo yao ya kazi na kukomesha vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na baadhi ya askari wa mgambo.

CHALAMILA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alimshukuru Rais Dk. Samia kuwainua mama na baba lishe kwamba  kundi hilo hivi sasa linatambuliwa na kuheshimiwa.

Akizungumzia mazingira na nishati safi, Chalamila alieleza serikali imepiga hatua kubwa kwa kuhamasisha matumizi ya gesi badala ya nishati chafu.

Alitaja mafanikio ya utekelezaji wa maagizo ya serikali ambapo zaidi ya shule 300 katika mkoa wa Dar es Salaam zimeanza kutumia nishati ya gesi badala ya kuni, zikijumuisha shule za msingi na sekondari. 

Chalamila alisisitiza hatua hiyo ni muhimu katika kulinda mazingira na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi hivyo aliahidi  kuwa Dar es Salaam itaendelea  kushirikiana na serikali kuu kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa kikamilifu.

Vilevile, aliikabidhi Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) zaidi ya sh. bilioni 94.1 kwa ajili ya mikopo ya wajasiriamali wadogo wakiwemo baba na mama lishe nchini.

Previous Post

YANGA YATIMUA VUMBI CAF, SIMBA MMH

Next Post

DK.NCHIMBI AMTAJA ASKOFU MFUMBUSA NGUZO YA UMOJA

Next Post
DK.NCHIMBI AMTAJA ASKOFU MFUMBUSA NGUZO YA UMOJA

DK.NCHIMBI AMTAJA ASKOFU MFUMBUSA NGUZO YA UMOJA

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

SERIKALI YATOA NENO SIMBASC

SERIKALI YATOA NENO SIMBASC

5 months ago
MAMBO YAZIDI KUNOGA AFCON 2027

MAMBO YAZIDI KUNOGA AFCON 2027

1 week ago

Popular News

  • DK.NCHIMBI AMTAJA ASKOFU MFUMBUSA NGUZO YA UMOJA

    DK.NCHIMBI AMTAJA ASKOFU MFUMBUSA NGUZO YA UMOJA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SITAWAANGUSHA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • YANGA YATIMUA VUMBI CAF, SIMBA MMH

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. SAMIA AMPA TANO SIMBU

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MAAJABU YA DP WORLD SIKU 730 BANDARINI DAR

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?