SYLVIA SEBASTIAN NA EMMANUEL MOHAMED
NI ripoti ya kuponya taifa na kuleta maridhiano, ndivyo inavyotarajiwa leo wakati Tume ya Kuchunguza matukio ya kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka jana, itakapokabidhi ripoti yake.
Tume hiyo itakabidhi ripoti yake kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, baada ya safari ya siku takribani 153 za kukusanya ushahidi wa kubaini chanzo cha matukio hayo, dhamira na athari zake kiuchumi na kijamii.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanazuoni na wanasiasa nchini, wameonyesha matarajio yao makubwa kuhusu ripoti ya tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Othman Chande.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na UHURU, wanazuoni na wanasiasa walisema ripoti hiyo italiponya taifa, kuleta maridhiano, suluhu na mwelekeo mpya wa taifa.
DK. TIMOTHY LYANGA
Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Timothy Lyanga, alisema matarajio ni kwamba ripoti hiyo itaipa nafasi serikali kutafakari yale ambayo tume hiyo imetoa mapendekezo ya kilichotokea.
Dk. Lyanga alisema Rais Dk. Samia aliona ni vyema kuunda timu ya wataalamu ya kubaini chanzo cha matukio hayo na kuitaka ilete mapendekezo yake baada ya kufanya uchunguzi.
“Tunachotarajia tume hiyo kutoa mapendekezo yake kutokana na kile ambacho imekipata, kutokana na wadau mbalimbali walivyoweza kukutana nao kuhusu tukio hilo,”alisema.
Alisema ripoti hiyo inatarajiwa kuwa ya uwazi kutokana na kiongozi wake, Jaji Mkuu mstaafu Chande, ambaye ni mwenye maadili, hekima na uadilifu, hivyo Watanzania wana matarajio kuwa, atawaletea kitu ambacho kitaleta suluhu kilichotokea.
“Pia, tume hiyo itatoa mapendekezo mbalimbali ya kushughulikia kilichojitokeza, hivyo hekima ya Rais Dk. Samia, ikaona ni vizuri ikawakutanisha wadau na siyo kuongea na kila mtu, tuna matarajio ripoti hii itaondoa zile hisia za kila mtu alizonazo,”alisema.
DK. IBRAHIM MWANGALABA
Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa Benki ya Maendeleo, Dk. Ibrahim Mwangalaba, alisema matarajio yake kwa ripoti hiyo ni kutibu kiu ya Watanzania.
“Rais Dk.Samia ameunda tume hiyo kufanya uchunguzi wa matukio hayo, hivyo ninaamini imekuwa huru kwa kiasi cha kuwaponya mioyo ya Watanzania na kubaki taifa moja litakalojenga imani na serikali,’’alisema.
JUMA ALI KHATIB
Mwenyekiti wa Chama Cha ADA TADEA, Juma Ali Khatib, alisema ana matumaini na tume ya Jaji Chande kutokana na uwezo wake.
“Inapotokea changamoto kama hiyo ni vizuri kuunda tume ya ndani ya nchi yako, ninawaomba wanasiasa wenzangu kuipokea ripoti hiyo kama itakavyokuja na tuweke uzalendo mbele,”alisema.
Alisema ripoti hiyo itawajenga Watanzania kuwa kitu kimoja kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi.
“Ripoti hii isitugawanye bali tuwaamini walioifanyia kazi na tuwape moyo tuendelee kushirikiana kwa namna moja ama nyingine,”alisema.
Pia, alisema ana imani na Tume ya Jaji Chande na kwamba, ripoti hiyo itakuwa na weledi mkubwa kwa kuponya majeraha ya Watanzania.
HASSAN DOYO
Aliyekuwa Mgombea wa Urais wa NLD, Hassan Doyo, alisema ripoti hiyo itatoa ufafanuzi wa kina kuhusu kilichotokea.
“Matarajio yangu kwa ripoti hii itasaidia kueleza kinaga ubaga kilichotokea kutokana na ushahidi walioupata,”alisema.
Doyo alisema matarajio ya ripoti ni kuona ukweli kilichotokea Oktoba 29, mwaka jana, kutokana na kuwa imani na tume hiyo ambayo italeta uponyaji wa majeraha hayo.
HADIDU ZA REJEA
Hadidu za rejea za tume ni kuchunguza na kubaini chanzo halisi cha yaliyotokea, malengo yaliyokusudiwa na waliopanga kutekeleza vitendo hivyo, madhara yaliyojitokeza ikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na hasara za kiuchumi zilizojitokeza.
Pia,tume iliangalia maeneo mazingira na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali na vyombo vyake katika kukabiliana na vurugu hizo.
Kupendekeza maeneo yanayohitajika kuimarishwa kwa kuongeza uwajibikaji wa viongozi na raia kwa minajili ya kulinda usalama na utawlaa bora, utawala sheria, haki za binadamu na mfumo madhubuti wa majadiliano ya kisiasa na kijamii hadi kufikia maridhiano na kuhakikisha vurugu hizo hazijirudii.
Rais Samia aliunda tume hiyo Novemba, mwaka jana, ambayo ilipaswa kuwasilisha ripoti yake Aprili 4, mwaka huu, hata hivyo, iliongezewa siku 21, kwa lengo la kupokea ushahidi zaidi, kupata uchambuzi wa kiyasansi ukiwemo wa picha na kuandaa kwa Lugha ya Kiswahili na Kingereza.




