Na MUSSA YUSUPH,
Dodoma
UWEKEZAJI mkubwa uliofanyika chini ya uongozi mahiri wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, tangu alipoingia madarakani miaka mitano iliyopita, umeiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa machache Afrika yaliyopiga hatua kubwa katika sekta ya afya.
Miongoni mwa mafanikio yakupigiwa mfano ni ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya kutoka 10,153 mwaka 2021/2022 hadi kufikia vituo 13,683 Machi mwaka huu sawa na ongezeko la vituo 3,530 vilivyojengwa katika kipindi cha Awamu ya Sita.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Wizara ya Afya, ongezeko hilo, linahusisha zahanati 8,706 kutoka 7,189, vituo vya afya
1,359 kutoka 956, hospitali 475 kutoka 404 na vituo vinginevyo vya kutoka huduma za afya 3,143 kutoka 1,604.
Katika kipindi hicho, Serikali ya Rais Dk. Samia, imejenga majengo mapya ya kisasa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Hospitali ya Kanda Benjamin Mkapa, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Hospitali ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Kusini Mtwara na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato.
Akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 bungeni jijini hapa jana, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, alisema serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu, vifaatiba, dawa na wataalamu katika sekta hiyo muhimu.
UJENZI HOSPITALI ZA RUFAA
Waziri Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji (CCM), alisema kuwa, serikali imejenga hospitali kumi mpya za rufaa za mikoa ambapo hospitali tano za mikoa ya Katavi, Njombe, Geita, Simiyu na Songwe hazikuwa na hospitali hizo huku hospitali tano za mikoa ya Ruvuma, Shinyanga, Singida, Mara na Lindi zilihamishwa kutoka majengo ya zamani kwenda maeneo mapya.
Vilevile, alisema serikali imeongeza majengo katika hospitali za rufaa za mkoa za Ligula (Mtwara), Sekou Toure (Mwanza), Maweni (Kigoma), Sumbawanga (Rukwa) na Kitete (Tabora).
“Hivyo, kwa sasa mikoa yote nchini ina hospitali za rufaa za mikoa na wilaya zote zina hospitali katika ngazi ya halmashauri.
“Pia, serikali imefanya ukarabati wa majengo ya zamani katika hospitali kongwe 50 za halmashauri, ukamilishaji maboma ya zahanati 980, ujenzi wa vituo vya afya 390, ujenzi wa mitambo ya kuzalisha hewa tiba ya oksijeni kwa wagonjwa mahututi na wagonjwa wa dharura,” alibainisha.
HUDUMA ZA DHARURA
Katika utoaji huduma za dharura nchini, alisema idadi ya majengo maalumu ya kutolea huduma za dharura, imeongezeka kutoka saba yaliyokuwepo mwaka 2021/2022 katika ngazi ya rufaa pekee hadi kufikia 125 Machi mwaka huu, yakijumuisha ngazi ya rufaa na msingi, sawa na ongezeko la majengo 118.
Alieleza kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria kwani kwa mara ya kwanza huduma hizo zimefikishwa hadi ngazi ya afya ya msingi ambapo zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania hupata huduma.
“Uwekezaji huu umeimarisha upatikanaji huduma za dharura ndani ya muda muhimu wa saa moja ya kwanza ambao kitaalamu ni kipindi muhimu cha kuokoa maisha na kuzuia madhara makubwa kama ulemavu au kifo.
Alisisitiza: “Wizara inaendelea kusimamia ubora wa huduma hizi kwa kuwa ushahidi unaonesha huduma bora za dharura zinaweza kupunguza vifo kwa wastani wa asilimia 40, hivyo kuokoa maisha ya wagonjwa wa dharura, ajali na majanga.”
ONGEZEKO IDADI YA VITANDA
Kwa mujibu wa Mchengerwa, idadi ya vitanda vya wagonjwa imeongezeka kutoka 86,131 mwaka 2021/2022 hadi 156,932 Machi mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vitanda 70,801 sawa na asilimia 82.
Pia, alisema idadi ya vitanda katika vituo vya umma kwa wagonjwa mahututi (ICU) imeongezeka kutoka 258 mwaka 2021/2022 hadi 1,647 Machi mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vitanda 1,389.
“Ongezeko la vitanda hivyo limeboresha huduma kwa wagonjwa mahututi, wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum na wagonjwa wote wa kulazwa, kuwezesha kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika,” alisisitiza.
AFYA YA MAMA NA MTOTO
Waziri huyo alisema katika miaka mitano iliyopita, serikali imeimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto kupitia diplomasia ya afya, hivyo kuwezesha kutekeleza miradi mbalimbali iliyogharimu sh. trilioni 1.2 zilizowezesha kuongezeka wodi maalum za watoto wachanga kutoka 49 mwaka 2021/2022 hadi 438 Machi mwaka huu.
Kadhalika, alisema vituo vya uchunguzi awali wa saratani ya mlango wa kizazi katika ngazi ya msingi, vimeongezeka kutoka 732 mwaka 2021/2022 hadi 1,700 Machi mwaka huu.
“Katika kipindi hicho kupitia mpango wa madaktari wa Dk. Samia, mafunzo kazini kwa watumishi 29,129 yametolewa na jumla ya watu 286,381 wamehudumiwa. Vilevile, serikali imehakikisha upatikanaji dawa muhimu za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa asilimia 85,” alieleza.
VIFO VYA UZAZI VIMEPUNGUA
Katika hotuba yake, Mchengerwa alibainisha kuwa mafanikio katika sekta ya afya nchini yamechangia kupunguza vifo vya
uzazi kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi vifo 104 mwaka 2022.
Alisema kushuka kwa vifo hivyo kumesababisha Rais Dk. Samia kuchaguliwa kuwa kinara wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika bara la Afrika.
Kutokana heshima kubwa iliyopewa Tanzania, alisema serikali imedhamiria kuwekeza katika afua za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza kwa asilimia 50 ya vifo 104 kwa takwimu za sasa ifikapo 2030.
“Lengo ni kuvuka Malengo Endelevu ya Dunia ya vifo vitokanavyo na uzazi kufikia chini ya 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo 2030,” alifafanua.
VIFAA VYA UCHUNGUZI MAGONJWA
Katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa mionzi kwa wagonjwa, alisema serikali imenunua na kusimika vifaa tiba vya uchunguzi na matibabu ya wagonjwa vyenye thamani ya sh. bilioni 241.6 ambavyo vinapatikana kuanzia ngazi ya
hospitali ya taifa hadi ngazi ya afya ya msingi.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi Machi mwaka huu, MRI zimeongezeka kutoka saba hadi 13, CT Scan 12 hadi 45, Mini Angio Suite tano, kipimo cha uchunguzi na tiba ya magonjwa ya mfumo wa chakula na mfumo wa uzazi (Fluoroscopy) 14, Digital X-ray 147 hadi 559, Ultrasound 476 hadi 970, huduma ya kutibu matatizo ya moyo ya dharura (CathLab) moja hadi nne.
“Matibabu ya hali ya juu ya magonjwa ya saratani (PET CT SCAN) ambayo haikuwepo awali sasa ipo moja. Kuongezeka kwa vifaa na vifaa tiba vya uchunguzi kumepunguza rufaa za ndani na nje ya nchi, kumewezesha kusogeza huduma kwa wananchi kwa gharama nafuu, kusaidia kutoa matibabu sahihi zaidi na kupunguza muda wa kupata huduma.
“Tumeshuhudia siku za karibuni wananchi wengi wakijiuliza kwa nini magonjwa yameongezeka?, pamoja na sababu
nyingine za mtindo wa maisha na mabadiliko ya tabia nchi, uwezo wetu wa kugundua na kutambua magonjwa umeongezeka sana kufuatia uwekezaji huu mkubwa,” alisisitiza.
MATIBABU YA KIBINGWA
Mchengerwa alisema serikali imeendelea kuboresha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi katika ngazi ya rufaa ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana ndani ya nchi.
Alizitaja baadhi ya huduma za ubingwa bobezi zilizotolewa kwa wagonjwa kuanzia mwaka 2021/2022 hadi Machi mwaka huu ni upandikizaji figo kwa wagonjwa 170, upandikizaji uloto kwa wagonjwa 57, upandikizaji vifaa vya usikivu kwa
wagonjwa 102 na uwekaji puto tumboni kwa wagonjwa 200.
Huduma zingine ni kuondoa mawe kwenye mfumo wa mkojo kwa kutumia mawimbi, mshtuko kwa wagonjwa 510, upandikizaji nyonga na magoti kwa wagonjwa 1,791, upasuaji mgongo kwa wagonjwa 1,688, upasuaji kibiongo kwa wagonjwa 98, upasuaji na urekebishaji mifupa ya kiuno kwa wagonjwa 647.
Pia, huduma zingine za kibingwa zilizotolewa ni upasuaji vichwa vikubwa na mgongo wazi kwa wagonjwa 2,095, upasuaji magoti kwa njia ya matundu kwa wagonjwa 1,246, upasuaji ubongo kwa kufungua kichwa kwa wagonjwa 1,208, upasuaji ubongo na mishipa ya fahamu kwa wagonjwa 785.
“Uvunjaji mawe kwenye mfumo wa mkojo kwa wagonjwa 1,347, upasuaji moyo (kwa kufungua kifua) kwa wagonjwa 73, kuzibua mishipa ya moyo kwa wagonjwa 2,074, upandikizaji wa kurekebisha mapigo ya moyo kwa wagonjwa 34, upasuaji macho kwa kutumia matundu madogo kwa wagonjwa 1,078, upasuaji ubongo kwa kutumia teknolojia ya mawimbi kwa wagonjwa 13.
“Matibabu ya radiolojia kwa wagonjwa 1,680, matibabu ya mfumo wa chakula na ini kwa wagonjwa 9,666, tiba mionzi bobezi kwa wagonjwa 1,651, tiba ya mionzi ya ndani kwa wagonjwa 10,056, tiba ya ‘immunotherapy’ wagonjwa 4,024, huduma za upasuaji magonjwa ya saratani kwa wagonjwa 6,097 na wagonjwa 731 wa saratani walifanyiwa uchunguzi kwa kutumia PET-CT scan,”alisema.
WAGONJWA ZAIDI NJE YA NCHI WATIBIWA
Waziri huyo, alibainisha kuwa, uwekezaji umewezesha wagonjwa 26,770 kutoka nchi za Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zambia, Malawi, Msumbiji, Kenya, Burundi, Angola, Rwanda, Sudani ya Kusini, Somalia na Uganda.
Kadhalika, alisema mwaka 2021/2022 hadi Machi mwaka huu, sh. trilioni 1.4 zimetolewa kugharamia ununuzi bidhaa za afya kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
Alisema kati ya fedha hizo, sh. bilioni 150 zilitolewa kulipa madeni ya MSD huku sh. bilioni 141.9, zilitolewa kununua dawa za ukimwi, malaria, kifua kikuu na sh. trilioni 1.1 zilitumika kwa manunuzi ya bidhaa za afya kwa vituo vya kutolea huduma za afya.
UJENZI WA VIWANDA
Pia, alisema katika kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya dawa na bidhaa za afya nchini, wizara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imewezesha kuanzishwa viwanda vipya 11 vya dawa na vifaa tiba ambavyo ni viwanda viwili vya kuzalisha maji tiba na viwanda vitatu vya kuzalisha vitendanishi vya maabara.
Viwanda vingine ni vitatu vya kuzalisha dawa za vidonge na maji, viwanda vitatu vya kuzalisha vifaa tiba ambapo vitawezesha uwepo endelevu wa maji tiba, vitendanishi vya maabara, dawa za maji na vidonge.
ONGEZEKO LA WATUMISHI
Kwa upande wa rasilimali watu, alisema serikali imeendelea kuajiri wataalam katika sekta hiyo ambapo wataalamu 53,633 wa kada mbalimbali wameajiriwa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Machi mwaka huu.
Hivyo, alisema hatua hiyo imewezesha idadi ya watumishi katika sekta hiyo kufikia 182,430.
Pia, alisema watumishi 9,039 waliajiriwa kwa mikataba ya muda mfupi kwa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato vya vituo husika vya kutolea huduma.
“Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wataalam bingwa na bingwa bobezi kwa ajili ya utoaji huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kwa kuanzisha Programu ya Samia Health Super Specialization Scholarship ambapo katika kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi Machi 2026,” alisema.
Alibainisha kuwa jumla ya wataalam 2,982 wamepata mafunzo katika fani mbalimbali za ubingwa na ubingwa bobezi ikilinganishwa na wataalam 961 waliofadhiliwa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021 sawa na ongezeko la wataalam 2,021.
“Ifahamike kuwa, mafanikio haya ya Sekta ya Afya katika kipindi cha Awamu ya Sita siyo takwimu tu za majengo,
vitanda, vifaa na huduma zilizoongezeka, ni simulizi ya maisha yaliyookolewa, matumaini
yaliyorejeshwa na utu wa Mtanzania uliolindwa.
“Kama ambavyo Mwalimu Nyerere aliamini kuwa maendeleo ya kweli ni maendeleo ya watu, kama Nelson Mandela alivyotufundisha kuwa heshima ya binadamu ndiyo msingi wa taifa huru na kama Kwame Nkrumah alivyosisitiza kuwa uhuru lazima uambatane na uwezo wa kujijenga.
“Serikali imeonesha kwa vitendo kuwa afya bora ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli. Hivyo, kila zahanati iliyojengwa,
kila hospitali iliyoboreshwa, kila mama aliyepata huduma salama na kila maisha yaliyookolewa ni ushahidi kwamba Tanzania inaendelea kujenga taifa lenye afya, usawa, utu na matumaini kwa vizazi vya sasa na vijavyo,” alisisitiza.
Kuhusu maombi ya fedha, Mchengerwa alisema wizara yake inaliomba Bunge kuidhinisha sh. trilioni 1.8 ili kuweza
kutekeleza malengo na vipaumbele iliyojiwekea kwa mwaka wa fedha 2026/2027
MAONI YA KAMATI
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Zeyana Abdallah Hamid, alisema ni muhimu serikali ikaendelea kuipa kipaumbele MSD kwa kuipatia mtaji.
Alisema endapo kiasi kinachoombwa cha mtaji kitapatikana, kitaiwezesha MSD kununua mahitaji yote ya bidhaa za afya bila kusubiri fedha za vituo vya kutolea huduma za afya.
Pia, alisema madeni yote serikali inayodaiwa yatafutiwe ufumbuzi kunusuru ustahimlivu wa Bohari Kuu ya Dawa.




