Na MWANDISHI MAALUMU, Zimbabwe
TANZANIA imeendelea kung’ara katika ukanda wa Kusini mwa Afrika baada ya kutajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa mifumo madhubuti ya usimamizi wa maafa, hatua inayozifanya nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kujifunza kupitia uzoefu wake.
Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi wakati wa Mkutano wa Sita wa Kawaida wa Kamati ya Mawaziri Wanaohusika na Usimamizi wa Maafa kwa nchi wanachama wa SADC uliofanyika mjini Masvingo, Zimbabwe, juzi.
Amesema Tanzania imefanikiwa kuimarisha mifumo ya kuzuia, kupunguza madhara, kujiandaa na kurejesha hali baada ya maafa kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya uratibu wa maafa nchini.
Kwa mujibu wa Mmuya, moja ya mafanikio makubwa ni kuanzishwa Kituo cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema ambacho kinafanya kazi muda wote kufuatilia na kuchambua taarifa za majanga.
“Kwa kupitia kituo hiki, serikali imepata taarifa za mapema kuhusu majanga yanayoweza kutokea, kufanya uchambuzi wa madhara na kuweka mikakati ya haraka ya kukabiliana nayo,” alisema Mmuya.
Ameongeza matumizi ya teknolojia ya kisasa katika ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu za wakati halisi yamechangia kuongeza ufanisi na kurahisisha utoaji wa taarifa rasmi kwa wananchi kuhusu namna ya kujiandaa dhidi ya maafa.
“Tunatumia takwimu za sasa na za zamani kutabiri hatari zinazoweza kujitokeza, jambo ambalo linaisaidia serikali kupanga kwa usahihi hatua za kurejesha hali na kuendelea kulinda maisha ya wananchi,” alielez.
Aidha, amewaalika wajumbe kutoka nchi za SADC kutembelea Tanzania kujionea namna mifumo hiyo inavyofanya kazi pamoja na ubunifu unaotumika katika usimamizi wa maafa.
Mkutano huo wa siku nne umezikutanisha nchi 16 wanachama wa SADC pamoja na wataalamu wa kitaifa na mashirika ya kimataifa kujadili utekelezaji wa programu za kikanda za usimamizi wa maafa na namna ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa mawaziri na washirika wa maendeleo kujadili uwekezaji katika sekta ya usimamizi wa maafa kwa lengo la kujenga ustahimilivu wa kikanda dhidi ya majanga yanayoendelea kujitokeza duniani.




