Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini leo Julai 31, 2026 kwenda Angola kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, João Manuel Gonçalves Lourenço.
Akiwa nchini Angola, Rais Dk. Samia atashiriki uzinduzi wa Hospitali ya Rufaa iliyopewa jina la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Luanda.
Hafla hiyo pia itahudhuriwa na familia ya Mwalimu Nyerere ikiongozwa na mama Maria Nyerere.
Mbali na hilo, Rais Dk. Samia atafanya mazungumzo na Rais Lourenço pamoja na kushiriki hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na wenza wa Marais wa Afrika.
Ziara hiyo inalenga kuendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria na wa kindugu kati ya Tanzania na Angola, uliojengwa tangu enzi za harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.





