Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema Tanzania itaendelea kuimarisha na kulinda ushirikiano wake na China, akieleza kuwa utamaduni umeendelea kuwa daraja muhimu la kuunganisha mataifa hayo mawili.
Makonda alisema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mazungumzo kati ya Tamaduni yaliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Alisema Tanzania na China zimeendelea kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo sanaa, utamaduni, elimu pamoja na diplomasia ya watu kwa watu.
“Utamaduni umeendelea kuwa kiungo muhimu cha urafiki na mshikamano wetu,” alisema Makonda.
Aidha, alisema mafanikio mengi yaliyofikiwa kupitia ushirikiano huo yanaonesha namna mahusiano ya kihistoria kati ya mataifa hayo yalivyoendelea kuimarika.
Makonda alitaja mradi wa TAZARA Railway Construction kuwa moja ya alama kubwa za ushirikiano huo pamoja na mchango wa China katika harakati za ukombozi wa Afrika.
“Miradi mikubwa kama Reli ya TAZARA ni ushahidi wa urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na China,” alisema.
Pia alisema Serikali imeanza ujenzi wa Kituo Kikuu cha Kisasa cha Uhifadhi wa Historia ya Ukombozi wa Afrika katika eneo la Kongwa mkoani Dodoma kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu muhimu za harakati za ukombozi wa bara hilo.
Maadhimisho hayo yaliambatana na maonesho ya sanaa na ngoma za asili kutoka Tanzania na China.
Kwa upande wake, Chen Mingjian alisema mwaka huu ni mwaka wa mabadilishano ya watu kwa watu kati ya China na Afrika pamoja na maadhimisho ya miaka 70 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Afrika.
Alisema urafiki wa Tanzania na China umejengwa tangu zamani kupitia mshikamano na ushirikiano wa maendeleo ikiwemo kipindi cha ujenzi wa Reli ya TAZARA.




