Na NASRA KITANA
TIMU za Simba na Yanga zimetoa msimamo kwamba zipo tayari muda wowote kuendelea na mechi zao tano za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ligi Kuu Tanzania ilisimama kwa muda kupisha mechi za Kimataifa za kirafiki ambazo zilitakiwa kucheza Juni 5 na Juni 9, mwaka huu nchini Morocco ambazo kwa sasa zimefutwa
Awali Taifa Stars ilipangwa kuchezaJuni 5, mwaka huu na Uganda kabla ya kuibakibili Rwanda, Juni 9, mwaka huu mechi zote zilipangwa kuchezwa jijini Marrakech nchini Morocco na kurejea tena Juni 12, mwaka huu.
Baada ya kuondolewa kwa mechi hizo, Kaimu Ofisa Habari wa TPLB, Yahya Abushehe alisema baada ya mechi hizo kufutwa Bodi itatangaza tena ratiba mpya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema wamejipanga muda wowote kurejea uwanjani kwa ajili ya ligi hiyo yenye ushindani mkubwa.
Alisema timu yao tayari ilikuwa katika mandalizi ya mechi zinazofuata.
“Tunajua zile mechi za timu ya Taifa hazichezwi tena na wachezaji watarajea, hivyo sisi kama klabu tupo tayari kwa mapambano muda wowote,” alisema Ahmed.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema hawana wasiwasi na wanapenda michuano hiyo iendelee kuchezwa.
“Timu yetu ipo tayari muda wowote ule kwa ajili ya kupambana na kupata matokeo mazuri, sisi hatuna hofu yeyote tunasubiri kama kutakuwa na mabadiliko yeyote ya ratiba basi tupo tayari kwa ajili ya mapambano,” alisema.
Kamwe alisema kila mchezaji anapenda kuitumikia timu kuhakikisha ushindi unapatikana.
Naye Mkuu wa idara ya Habari na Mawasiliano, Azam FC, Zacharia Thabit ‘Zaka’, alisema timu yao inaendelea na mazoezi na wamejipanga muda wowote kushuka dimbani.
“Sisi tumejipanga muda wowote kushuka dimbani kwa ajili ya kupambana na mechi zetu tano zilizobakia hivyo kila mchezaji anajua nini anatakiwa kufanya na tupo tayari kurejea uwanjani,” alisema Zaka.
Hadi sasa Yanga ikibaki na mchezo dhidi ya Mashujaa FC, Fountain Gate FC, Azam FC, TRA United na JKT Tanzania.
Simba yenyewe imebaki na mechi dhidi ya Pamba Jiji, Mbeya City, Mtibwa Sugar, Singida Black Stars na KMC huku Azam wao wakibaki na mchezo dhidi ya Fountain Gate, Mashujaa, Yanga, Coastal Union na Dodoma Jiji.
Yanga inaongoza ligi hiyo, ikiwa na pointi 60 ikifuatiwa na Simba yenye alama 58 huku Azam ikishika nafasi ya tatu, ina pointi 52.




