Na MWANDISHI WETU
WAKATI Simba imetangaza panga kwa wachezaji saba ikiwa ni sehemu ya kutaka kusuka kikosi chao kitakachoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara 2026/27, tamasha lao, limepangwa kufanyika Agosti 8, mwaka huu.
Kupitia ukurasa rasmi wa Instagram wa klabu hiyo, Simba ilichapisha ujumbe wenye neno ‘Asanteni’ ukiambatana na picha pamoja na majina ya wachezaji hao, baadhi yao wakiwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo msimu uliopita huku wengine wakicheza kwa mkopo katika klabu tofauti.
Wachezaji waliotangazwa kuondoka ni Chamou Karaboue, Naby Camara, Edwin Balua, Joshua Mutale, Awesu Awesu, Omari Omari na kipa Moussa Camara.
Hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya kikosi yanayofanywa na Simba kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano ya kimataifa.
Baadhi ya nyota hao walikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Simba katika msimu uliomalizika na walitoa mchango wao mkubwa katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Aidha, taarifa hiyo, imeeleza kwamba uongozi wa klabu hiyo, utaendelea kufanya mabadiliko zaidi ya kikosi chao, ili kuimarisha timu kwa ajili ya msimu ujao.
Wakati huo huo, baada ya vikao vya muda mrefu hatimaye viongozi wa Simba umepitisha Agosti 8, mwaka huu, kuwa ‘Simba Day’ itafanyika jijini Dar es Salaam huku uzinduzi ukifanyika Ngorongoro, Arusha, Julai 25, mwaka huu.
Taarifa za ndani ya klabu hiyo, zimeeleza kuwa hivi sasa uongozi huo upo katika utaratibu wa kufanya tathmini ya uwanja utakaofanyika tamasha hilo na ratiba kamili itatoka.
Tamasha hilo limekuwa likifanyika kila mwaka na hutumika kwa ajili ya kutambulisha kikosi kipya ambacho kitatumika katika msimu wa mashindano wa 2026/2027.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema tamasha hilo lipo na watatangaza lini litafanyika na uwanja gani baada ya uzinduzi utakaofanyika Ngorongoro.
“Msimu huu tutakuwa na tamasha bora tofauti na yale yaliopita, muda mfupi kuanzia leo tutatangaza lini tutafanya tamasha hilo muhimu kwetu na mahali ambapo litafanyia,” amesema Ahmed.
Ahmed alisema msimu huu tamasha hilo litakuwa na vitu vingi tofauti, ‘suprises’ za kutosha na wasanii wengi kwani wanahitaji kuwa na tamasha la tofauti na la kihistoria.
“Simba Day ya mwaka huu linafikisha miaka 17 tangu kuanzishwa kwake tangu mwaka 2009,”alisema kiongozi huyo.




