Na AMINA KASHEBA
KETE muhimu iliyobeba matumaini makubwa kwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kupata ushindi wake wa kwanza katika historia ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), itasukumwa leo wakati miamba hiyo itakapochuana na Uganda ‘The Cranes’.
Mtanange huo wa dabi ya Afrika Mashariki utapigwa saa 2:30 usiku katika Uwanja wa Al Medina uliopo Rabat, Morocco.
Timu hizo kutoka ukanda wa CECAFA zitachuana katika mchezo wa kundi C wa AFCON 2025, baada ya awali kila moja kuanza kwa kichapo.
Katika michuano hiyo, Tanzania ilianza kwa kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Nigeria wakati Uganda ikipigwa mabao 3-1 dhidi ya Tunisia.
Ili kufufua matumaini yake ya kutinga mtoano na kuweka rekodi ya kupata ushindi wake wa kwanza, Stars inapaswa kuifunga Uganda leo.
Katika michuano hiyo ya nne kwa Tanzania kushiriki, miamba hiyo haijawahi kushinda hata mechi moja kati ya mechi 10 ilizocheza katika AFCON, ikitoka sare mara tatu na kufungwa mara saba.
Akizungumza maandalizi ya mchezo huo, Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Miguel Gamondi, alisema wachezaji wake wako tayari kupambana kupata ushindi katika mechi hiyo.
Alisema Uganda siyo timu kubwa huku Stars ikiwa na wachezaji mahiri wakiwemo Simon Msuva na Mbwana Samatta ambao wana uwezo wa kuipa ushindi timu hiyo.
“Uganda siyo timu kubwa, wao na sisi ni kama sawa tu, angalia hata utofauti wao uwiano wa wachezaji ndani na nje, kisha utaona ni dabi na itakuwa mechi ngumu, lakini ubora utendaji uwanjani utaamua mchezo.
“Kwa upande wetu tuna wachezaji wanaoweza kushinda huu mchezo tuna kina Msuva na Samatta na hilo ni jambo ambalo Watanzania wanapaswa kulifahamu, ” alisema Gamondi.
Kocha huyo alifafanua kuwa katika mechi ya leo mchezaji, Feisal Salumu atakuwepo katika timu baada ya kumaliza adhabu aliyokuwa akiitumikia, hivyo Watanzania wategemee mambo mazuri kutoka kwa Stars.
“Feisal Salumu ni mchezaji muhimu, alikuwa na adhabu anaitumikia ya mchezo mmoja hivi sasa tuko naye, kikubwa kwetu ni kuwa na maandalizi mazuri ambayo yatatupa matokeo mazuri,” alisema Gamondi.
Kocha huyo aliongeza kuwa watapambana kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo dhidi ya Uganda.
“Khalid Aucho ni mchezaji mzuri sana anafanya kazi nzuri mtu, humuoni akifunga lakini kwangu ni kiungo aliyekamilika mwenye ushawishi mkubwa, sijui historia ya Uganda nadhani ni moja kati ya wachezaji wakubwa waliowahi kutokea Uganda.
“Nimemfundisha akiwa na Yanga hivi sasa Singida Black Stars, mchezaji nzuri sana lakini wachezaji wangu wamejipanga kupata matokeo mazuri, japokuwa tunaelewa utakuwa mchezo wenye ushindani kubwa,” alisema.
Naye Simon Msuva alisema malengo yao ni kupata ushindi katika mchezo wa leo, hivyo watapambana kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya kupata ushindi katika mechi ya leo.
Katika michuano mingine na mechi za kuwania kufuzu AFCON, miamba hiyo miwili ya Afrika Mashariki imewahi kukutana mara 61.
Katika mchanganuo huo, Uganda ndiyo kinara wa ubabe ikishinda mechi 33, Tanzania mechi 12 na timu hizo zimetoka sare mara 16.
Hivi karibuni, miamba hiyo ilikutana katika mechi za kuwania kufuzu fainali za AFCON 2023, ambapo Tanzania ilishinda bao 1-0 ugenini na Uganda ilipata ushindi kama huo ugenini.
Katika kundi hilo, Tanzania ilimaliza nafasi ya pili juu ya Algeria na kufuzu fainali hizo zilizopigwa nchini Ivory Coast.




