Na AMINA KASHEBA
ALIYEKUWA Kocha wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Hemed Suleiman Morocco, amesema mashindano ya Kombe la Mapinduzi ni chachu kubwa ya kuibua vipaji vya vijana kwa kupata fursa ya kuonekana na klabu mbalimbali.
Mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanatarajiwa kuanza kesho na kumalizika Januari 13, mwakani ambapo yatashirikisha timu 10 katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Katika mashindano hayo timu zinazoshiriki ni Yanga, Simba, Azam FC, Singida Black Stars, TRA United (Tanzania Bara), Mlandege, Muembe Makumbi, Fufuni, KVZ (Zanzibar) na URA ya Uganda.
Akizungumza na UHURU, Kocha Morocco, alisema mashindano hayo yamekuwa na historia kubwa visiwani hapo, pia hufanyika kwa ukubwa kutokana timu zinazoshiriki kuleta ushindani.
“Mashindano mazuri yanakuja kila mwaka, yanaibua vipaji kwa vijana tunawapa vipaumbile kutokana na ukubwa wake, hivyo kila mtu anakuwa akisubiri kwa shauku kubwa.
“Zanzibar huwa tunayapa vipaumbile kutokana na ukubwa wao, pia kunakuwa na wadau wengi ambao wanakuja kuangalia vipaji vya vijana na baada ya kumaliza kuna baadhi yao wanapata fursa ya kuchaguliwa na timu tofauti,” alisema.
Kocha huyo alitoa wito kwa wadau kujitokeza kwa wingi katika mashindano hayo kuona vipaji vya vijana na ushindani uliopo katika timu zinazoshiriki.
“Timu zote zinazoshiriki mashindano haya yako vizuri kwa sababu Zanzibar tuna timu nzuri na vijana wenye vipaji, tuna imani watafanya mambo makubwa, wadau wajitokeza kuja kuangalia kwani hata nchi za jirani huwa wanatamani kuja kushiriki,” alisema.




