Na MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imesema katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imepata mafanikio makubwa katika kusimamia huduma za usafiri kufuatia kutumia vyema falsafa yake ya 4R.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Dk. Habib Suluo, alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Amesema Rais Dk. Samia kupitia falsafa yake amekuwa kinara wa kukuza shughuli za kijamii na kiuchumi, ikiwemo kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa sekta ya uchukuzi.
Dk. Suluo amesema idadi ya leseni za usafirishaji zilizotolewa kwa vyombo vya usafiri wa abiria, mizigo na vyombo vya usafiri wa kukodi ziliongezeka kutoka 239,953 mwaka 2021/22 hadi leseni 590,468 mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la leseni 350,515.
Pia, kupitia huduma ya tiketi mtandao kwa mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani iliyoanza kutolewa mwaka 2022, imekuwa na tija kwa kuwezesha abiria kukata tiketi za mabasi na treni kupitia Safari Tiketi App.
Kwa mujibu wa Dk. Suluo, huduma hiyo hadi Juni, mwaka huu, ilikuwa na watoa huduma 14 ambao mifumo yao imeunganishwa na LATRA.
Hata hivyo, ametahadharisha mamlaka hiyo inawafuatilia watoa huduma hao kutokana na baadhi taarifa zao kutoka katika mfumo kuonesha zina shaka.
Mkurugenzi huyo amesema kwa ujumla, utekelezaji wa mfumo wa tiketi mtandao umeboresha huduma kwa abiria kukata tiketi popote walipo, kuchagua muda wa kusafiri kulingana na mabasi wanayotaka.
Amefafanua huduma za kusafiri usiku zimekuwa na tija kwa wasafiri kutokana na wengine kupunguza gharama za matumizi, ambapo wakifika mikoa husika hufungiwa mizigo na kurudi walikotoka wakiwa wamelala ndani ya mabasi.
“Faida nyingine mtu anachagua gari na daraja la basi analotaka, kisha hulipa nauli kwa njia ya mtandao au fedha taslimu anapokuwa kwenye ofisi za mawakala au kampuni husika,” alisema.
Idadi ya abiria na miamala iliyofanyika kwa kipindi cha utekelezaji wa mfumo huo imeongezeka kutoka abiria 7,112 na miamala ya sh. bilioni 226.29 mwaka 2022/23, hadi abiria 28,673 na miamala ya sh. bilioni 993.96 mwaka 2025/26.
Amesisitiza watoa huduma za usafiri vikiwemo vivuko, mabasi ya mwendokasi, usafiri mtandao na abiria kwa ujumla, kuzingatia malipo kwa njia ya elektroniki kama ilivyoamriwa na Wizara ya Fedha kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.
MADEREVA NA WAHUDUMU
Dk. Suluo amesema katika kusajili madereva kuendesha magari yanayotoa huduma za usafiri wa umma na mizigo kwa usalama na wahudumu kwa kipindi cha 2022/23-2025/26), madereva 15,547 walisajiliwa na kufanya mtihani wa kuthibitishwa na LATRA kupitia Mfumo wa Kutahini Madereva (DTS), ambapo kati ya hao 8,642 waliofaulu na kuthibitishwa ni sawa na wastani wa asilimia 56.
“LATRA imeweka utaratibu wa lazima kwa madereva wa safari za usiku kwa mabasi ya abiria na mabasi ya kukodishwa kuwa na kitufe cha utambuzi,” alisema.
Amesema katika mifumo ya TEHAMA ya VTS na i-buttons inayofuatilia mienendo ya madereva barabarani, mafanikio makubwa yamepatikana kwa kuleta usalama wa huduma na kuepusha ajali.
Hata hivyo, alisema changamoto kwa madereva wanaofanya mitihani hiyo ni matokeo yao ya ufaulu kuwa chini kwa asilimia 56, hali inayoashiria baadhi hawajiandai vyema, waoga kufanya mtihani kwa kompyuta au hawana utaratibu wa kujisomea.
Akielezea wahudumu wa magari, mkurugenzi huyo wa LATRA amesema waliandaa mtaala wa kozi fupi ya wiki moja kwa kushirikiana na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo cha Biashara (CBE), Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).
“Kwa mujibu wa sheria, kabla ya wahudumu kusajiliwa wanapaswa kupata mafunzo maalumu kuhusu kazi zao kwenye vyombo vya usafiri, ikiwa ni pamoja na kujua sheria, kanuni, na taratibu husika na utoaji huduma bora kwa abiria na wateja,” alisema.
Katika kufanikisha utekelezaji wa jukumu hilo lililoanza 2023/24, Dk. Suluo alisema wanafunzi 656 walipata mafunzo na kufaulu, idadi iliyoongezeka na kufikia 7,216 hadi Juni mwaka huu, wahudumu wanaofaulu mafunzo hayo huwasilisha maombi ya kusajiliwa LATRA katika mfumo wa RRIMS.
Kwa upande wa Mifumo ya Teksi Mtandao, mamlaka imesajili kampuni 22 ikiwemo kuwaunganisha wasafirishaji wenye magari 23,532 wenye leseni hai za kutoa huduma hiyo.
Ameongeza kuanzia mwaka 2023/24 hadi 2025/26, LATRA ilitoa vyeti kwa mawakala 100 ilijumuisha kampuni-69, vyama vya ushirika saba, Taasisi za Umma (LGAs na Shirika la Posta Tanzania)-23 na mtu binafsi mmoja.
Mawakala hao walitoa asilimia 70 ya leseni za pikipiki, kukusanya sh. bilioni 7.9 na kulipwa kamisheni bilioni mbili. Suluo.
KUHUSU WIKI YA USAFIRI, EL-NINO
Vilevile, Dk. Suluo ametangaza mamlaka hiyo kuanza maandalizi ya Maadhimisho ya Pili ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini, 2026.
Maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini, Kuharakisha Usafiri Endelevu: Usafiri Salama, Rafiki kwa Mazingira na Jumuishi, yatafanyika Mlimani City, Dar es Salaam kuanzia Novemba 24 hadi 26. Washiriki 2,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania wameomba kushiriki.
Pia, Dk. Suluo aliwataka wadau wa sekta ya usafiri ardhini, wakiwemo wamiliki wa vyombo vya moto kibiashara, madereva, abiria na watoa huduma za usafiri ardhini, kuchukua tahadhari kabla, wakati na baada ya safari katika kipindi cha mvua za El-Nino kwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuzingatia maelekezo ya mamlaka husika kuhusu hali ya barabara na usalama wa safari.




