Na MWANDISHI MAALUMU, Doha, Qatar
WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema Tanzania imepata fursa nyingine za ajira zaidi ya 4,500 kwa Watanzania walio tayari kufanya kazi Qatar kwa kada mbalimbali.
Amesema, alipotoa ufafanuzi kuhusu ziara yake ya siku tatu nchini Qatar na manufaa ambayo Tanzania imepata.
Dk. Mwigulu alikuwa nchini Qatar kwa mwaliko wa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani.
“Tunatarajia kupata nafasi nyingine 4,500 kwa Watanzania ambazo ziko katika hatua za mwisho za kukamilisha utaratibu.
“Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, ndiyo inaratibu zoezi zima kwa kushirikiana na wizara za kisekta, ikiwemo ya Mambo ya Ndani pamoja ile ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,” alisema Dk. Mwigulu.
Tanzania imekuwa ikinufaika na fursa za ajira nchini Qatar, ambapo hadi hivi sasa, kuna Watanzania 720 walioajiriwa katika Kampuni ya Taifa ya Usafirishaji ya Qatar (MOWASALAT) ikiwa ni sehemu ya nafasi za ajira 2,000 zilizotolewa katika awamu ya kwanza.
Katika awamu ya pili, Kampuni ya Power Holding International, imetoa nafasi za ajira zaidi ya 4,000 kwa Watanzania wenye ujuzi mbalimbali.
Akielezea kuhusu mazungumzo yao, Dk. Mwigulu alisema walijadili kuhusu hati mbili za makubaliano ambazo zilitiwa saini juzi na waliafikiana kwamba, hati moja iliyobaki ya kuepusha ukwepaji kodi na utozaji wa kodi mara mbili, ikamilishwe itiwe saini mapema iwezekanavyo.
Hati zilizotiwa saini ni ya Makubaliano ya Ushirikiano katika maeneo ya Zimamoto, Uokoaji na Huduma za Dharura kati ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya Taifa la Qatar na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. ,
Nyingine ni Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano wa Kisiasa na Kidiplomasia baina ya Taifa la Qatar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ziara hii kimsingi ililenga kutilia mkazo maeneo yaliyokubaliwa na viongozi wetu wakuu wa nchi wakati walipokutana,” alisema.
Dk. Mwigulu, alitumia fursa hiyo kumwalika Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Al Thani, afanye ziara nchini Tanzania, kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kufuatilia utekelezaji wa mambo waliyokubaliana.
Alisema kuwa, katika ziara yake, alikutana na wajumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika mwaka 2022 nchini Qatar.
“Lengo lilikuwa ni kupata uzoefu wao katika kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa na yakafanikiwa kwa kiwango cha juu sana.
“Hii ni fursa kwetu kwa sababu Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoandaa michuano ya Kombe la Mataifa Huru ya Afrika hapo mwaka kesho,” alisema.
Katika ziara hiyo, Dk. Mwigulu alifuatana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ngwaru Maghembe, Katibu Wakuu (OR-Uwekezaji), wabunge na watendaji wengine wa serikali.




