Na WAANDISHI WETU
IMETIMIA miaka 27, tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alipofariki dunia kwa maradhi, Oktoba 14, 1999.
Tangu mwanzo wa mwezi huu hadi leo, vyombo vya habari rasmi na visivyo rasmi, ikiwemo mitandao ya kijamii, vimekuwa vikitangaza na kuandika makala na taarifa kumkumbuka Mwalimu Nyerere.
Ni Rais wa Awamu ya Tatu ya Uongozi wa Nchi, Benjamin Mkapa aliyewatangazia Watanzania kifo cha Mwalimu Nyerere, kilichotokea katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, jijini London, Uingereza.
Watanzania walimpenda Mwalimu Nyerere, naye katika uongozi wake, aliwapenda na kuwatumikia kwa kiwango cha ‘kujikataa’ mwenyewe, ndiyo maana husemwa Nyerere alikufa masikini.
Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alikuwa ni kiongozi siyo tu uongozi wake ulijipambanua ndani ya nchi yake, bali Afrika na duniani kote, alikuwa kama msemo wa vijana ni ‘habari nyingine’ kitaifa na kimataifa.
Nyerere aliyezaliwa mwaka 1922, alizitendea haki siku ambazo alijaliwa kuishi duniani. Ameacha alama kitaifa na kimataifa, hakuja duniani kuzurura na kuondoka.
Wanapozungumzwa viongozi wa Afrika ambao wameleta mabadiliko ya maana katika mataifa yao, Mwalimu Nyerere ni mmoja wao, wala viongozi wa aina yake, hawajahi katika kiganja cha mkono, ni wachache mno.
Katika kitabu chake cha Uhuru na Umoja, Nyerere anaeleza namna alivyowawezesha Watanzania kuwa kitu kimoja licha ya kuwa, wanatokana na zaidi ya makabila 120.
Kama kuna nchi katika Afrika ambayo imefanikiwa kulijenga taifa lenye umoja na amani, ndani ya mipaka iliyowekwa na wakoloni, si lingine zaidi ya Tanzania chini ya uongozi thabiti wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
LUGHA YA KISWAHILI
Mwalimu Nyerere alitumia Kiswahili kuieneza na kuikuza ikiwa ni moja ya nyenzo ya kulijenga taifa imara la Tanzania, ambalo wananchi wake wanazungumza lugha moja.
Matumizi ya Kiswahili yameepusha taifa kuwa na misuguano ya ukabila na makundi na kulifanya taifa kuwa moja kinyume na hali ilivyo katika mataifa mengine.
JESHI LA KUJENGA TAIFA
Mwalimu Nyerere alitumia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kutoa mafunzo kwa vijana, kuwajengea uzalendo na kuwa tayari kulinda nchi yao dhidi ya maadui wa ndani na nje.
Ni katika jeshi hilo, vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini, walijiunga na kufundishwa kujitegemea, kujiamini, kuthubutu katika kubadili hali ya maisha yao na taifa lao.
Wakati wa uongozi wake, Mwalimu Nyerere alilijenga taifa katika misingi ya kiitikadi na kimaadili katika uongozi wenye lengo la kuimarisha uhuru wa Watanzania na kuwawezesha wananchi kujikomboa.
Misingi aliyoiweka na kuisimamia ni pamoja na uhuru, utu, usawa, haki, umoja, utaifa, uzalendo, uwajibikaji, uadilifu, kujitegemea, amani na maadili.
“Misingi hii ambayo wengine wanaita ni tunu, ndiyo mtima wa taifa letu, mtima ni zaidi ya moyo. Lakini, ndiyo fahari ya taifa letu inayojenga haki za msingi za binadamu, ndiyo kiini cha haki zote za binadamu,” aliwahi kusema Profesa Palamagamba Kabudi, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu.
Profesa Kabudi alisema, kwa Mwalimu Nyerere, amani na mshikamano ndiyo ilikuwa nguzo ya ustawi wa taifa na hata baada ya kifo chake, misingi hiyo inaendelea kuwa nguzo kwa taifa.
“Mwalimu Nyarere alisimamia maadili na miiko ya uongozi na watumishi wa umma, kwa nguvu zake zote akihimiza madaraka kiongozi wa umma ni dhamana.
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alijali ustawi wa kila mwananchi, ndiyo maana baada ya uhuru alitangaza vita dhidi ya maadui wakuu watatu; ujinga, maradhi na umasikini,” alisema Profesa Kabudi.
Mwanazuoni huyo, anasema kwamba, maisha ya uongozi ya Mwalimu Nyerere; kitaifa na kimataifa, yanamwingiza katika orodha ya mashujaa waliokataa kufa, wanaishi licha ya kufariki dunia.
Kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ni tukio lenye mguso wa kipekee kwa Watanzania waliomuona akiwa hai, na vijana ambao wamezaliwa baada ya kifo chake.
Ndiyo maana, hata baada ya kuondoka duniani, viongozi wa viwango vya Mwalimu Nyerere, siku zao za kuzaliwa na zile za vifo vyao, huendelea kuhesabiwa na kuadhimishwa kwa bashasha za aina yake, kama inavyofanyika leo ambayo ni siku Mwalimu Nyerere alifariki dunia.
Katika kumbukizi ya miaka 27 tangu kifo chake, baadhi ya wanasiasa, wanadiplomasia na wasomi nchini, walieleza namna ambavyo Baba wa Taifa anavyoendelea kukumbukwa.
STEPHEN WASIRA
Akizungumza na gazeti hili jana, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, alisema urithi mkubwa ulioachwa na hayati Nyerere ni umoja wa Watanzania, uzalendo na misingi ya uadilifu katika uongozi na matumizi ya rasilimali za taifa.
Wasira alisema Watanzania wanapaswa kuendelea kumuenzi hayati Nyerere kwa kulinda umoja wa kitaifa na kuepuka tofauti za kikabila na kidini, ambazo zimekuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili Afrika.
Alisema licha ya matatizo mbalimbali yanayolikabili taifa, umoja wa Watanzania umeendelea kuwa imara kutokana na misingi iliyojengwa na hayati Nyerere ya watu kuheshimiana na kuelewana.
Pia, alisema Nyerere atakumbukwa kwa kudai uhuru wa Tanganyika na baadaye kuunganisha Tanganyika na Zanzibar na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo alisisitiza umuhimu wa kuendeleza misingi ya uzalendo na uadilifu aliyoiacha Baba wa taifa, aliyeongoza nchi kwa miaka 23.
ANNA ABDALLAH
Mwanasiasa mkongwe, Anna Abdallah, alisema Nyerere atakumbukwa kwa kuwaunganisha Watanzania hali iliyosaidia hadi sasa kuwepo amani.
Alisema Nyerere ataendelea kukumbukwa kwa utayari wake, nguvu na utashi wake alioutoa kuhakikisha nchi za Afrika zinapata uhuru wake.
“Mwalimu Nyerere alijitoa kuhakikisha Tanzania inakuwa kituo cha ukombozi mwa nchi za Afrika na hata sisi tuliadhirika kwa sababu hiyo lakini yeye hakujali
Ann alisema mchango wa Nyerere hauishii katika upatikanaji uhuru, bali unahusisha uungaji mkono kwa wapigania uhuru wa mataifa mengine Afrika.
HAMAD RASHID
Mwanasiasa mkongwe, Hamad Rashid Mohamed, alisema Watanzania wanapaswa kuendeleza uhuru wa kiuchumi kwa kutumia rasilimali za nchi kujiletea maendeleo.
Alisema Nyerere alisisitiza umuhimu wa Tanzania kujitegemea kiuchumi, kuimarisha kilimo kwa lengo la wananchi kupata chakula cha kutosha na kujenga viwanda kupitia mashirika ya umma.
Alisema sera ya kutofungamana na upande wowote katika migogoro ya kimataifa ni miongoni mwa misingi muhimu aliyoiacha.
BALOZI AMINA SALUM ALI
Balozi Amina, alisema Nyerere atakumbukwa katika eneo la diplomasia kwa kuanzisha sera ya mambo ya nje ya nchi.
“Sera hii iliandaliwa na kusimamiwa na yeye mwenyewe kutokana na kuwa, alishiriki katika ukombozi wa uhuru aliona kuwa sera hii ndiyo itakayoongoza mahusiano ya nchi na nchi.
Alisema hayati Nyerere alichukizwa sana kuona nchi nyingi za Afrika bado zipo katika ukoloni wa kutawaliwa na ukoloni mamboleo.
“Mwalimu Nyerere aliamua Tanzania ijiunge na kundi la kutofungamana na upande wowote, mpaka leo bado tupo, hivyo mwalimu alisimamia haki na usawa,”alisema
BALOZI MNDOLWA
Balozi Francis Mndolwa alisema Nyerere alijitoa katika harakati za ukombozi mwa bara la Afrika kwa kuanzia nchi ambazo zipo karibu na Tanzania.
“Aliamini kuwa nchi hizo zikiwa na amani na sisi Tanzania tutakuwa na amani, ni mtu ambaye alipenda kushirikiana na viongozi wenzake,”alisema.
PROFESA ABEL KINYONDO
Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo, alisema Mwalimu Nyerere kipaumbele chake kikubwa kilikuwa ni masuala ya elimu.
Alisema kipindi cha uongozi wake alihakikisha elimu inatolewa bure huku, akitumia msemo wa elimu ni ufunguo wa maisha.
Dk. TIMOTHY LYANGA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Timothy Lyanga, alisema Mwalimu Nyerere ataendelea kukumbukwa kwa mchango wake katika sekta ya elimu.
Dk.Lyanga alitaja moja ya mchango mkubwa alioutoa Mwalimu Nyerere ni kuhakikisha Watanzania wanajua kusoma na kuandika kupitia uongozi wake.
Alisema Mwalimu Nyerere aliiona elimu kuwa ni nyenzo muhimu inayowajenga Watanzania kuungana.
Habari imeandaliwa na Emmanuel Mohamed, Athnath Mkiramweni, Rehema Maigala na Ziana Bakari




