Na NASRA KITANA
LEO ni siku ambayo timu za Yanga na Simba zinatarajiwa kuonesha ubabe wao katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika(CAFCL) zitakazopigwa viwanja viwili tofauti.
Simba leo itakuwa ugenini katika mchezo wake wa kwanza wa hatua ya pili ya raundi ya awali ya CAFCL dhidi ya 15 Agosto ya Guinea ya Ikweta.
Pambano hilo, limepangwa kufanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuanzia saa 9:00 alasiri.
Huku watani wao wa jadi, Yanga watashuka dimbani kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya CFFA ya Madagascar ikisaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi utakaochezwa katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.
Huo ni mchezo muhimu kwa Yanga baada ya kufanikiwa kushinda mabao 4-0 ugenini katika uliofanyika huo huo Uwanja wa Azam Complex, ambapo CFFA iliiutumia kama uwanja wao wa nyumbani.
Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na mguu mmoja ndani ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupata ushindi mnono wa mchezo wa kwanza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi alisema timu yake imejipanga vizuri kuhakikisha inapata ushindi.
Mngqithi alisema katika mchezo wa kwanza walipata ushindi ambao hauwapi uhakika wa kusonga mbele zaidi ya kujipanga kushinda leo ili kutinga hatua inayofuata.
Manqoba alisema wachezaji wote wapo fiti kuhakikisha wanaenda kupambania timu yao kwa jasho na damu.
“Hata kama tuliweza kupata ushindi katika mchezo wetu wa kwanza, lakini hatutabweteka kwani tunahitaji kupata ushindi na kusonga mbele hatua inayofuata,” alisema Manqoba.
Kocha huyo alisema wamefanyia kazi kasoro zilizotokea katika mchezo wa kwanza na sasa kikosi chake kipo imara zaidi.
Manqoba aliwaomba mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi ili wakape sapoti wachezaji wake wafanye vizuri na kutinga hatua makundi.
Kwa upande wa kocha wa Simba, Steve Barker alisema kuwa timu yao imefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha inapata ushindi katika mchezo huo muhimu.
“Wapinzani wetu siyo timu ya kuibeza, kwani wapo vizuri hivyo tutahakikisha tunaenda kupambana nao mwanzo mwisho ili kupata ushindi.
Barker alisema watahakikisha wanapambana kwa jasho na damu ili kuweza kupata matokeo mazuri, kwani tunahitaji kupata ushindi ili kusonga mbele hatua inayofuata.
Kocha huyo alisema ana imani kubwa na kikosi chake kwani kila mchezaji ana morari ya kutosha kuhakikisha anaipambania timu kupata ushindi.
Barker alisema malengo yao makubwa ni kuona wanapata ushindi katika mchezo huo kabla ya kurejea katika mchezo wa marudiano ili kutinga hatua ya makundi.
15 DE AGOSTO YARUHUSU MASHABIKI UWANJA WA UHURU
Hatimaye timu za Simba na 15 de Agosto zimefikia makubaliano ya kuruhusu mashabiki kuingia uwanjani katika mchezo huo.
Awali, 15 de Agosto ambao ni wenyeji walitaka mchezo huo upigwe bila mashabiki.
Simba imethibitisha kufikia makubaliano hayo na 15 de Agosto kupitia taarifa rasmi iliyochapishwa katika kurasa za mitandao ya kijamii za klabu hiyo yenye maskani yake Msimbazi, jijini Dar es Salaam.




