Na NASRA KITANA
KATIKA kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), dhidi ya Stade Malien ya Mali, benchi la ufundi la timu ya Simba limeweka wazi kuwa pamoja na timu yao kushindwa kufanikiwa kutinga robo fainali ya mashindano hayo lakini watapambana kuweka heshima kwa kushinda mchezo huo.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani kesho katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Stade Malien, utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1:00 usiku.
Wekundu hao wa Msimbazi wataingia katika mchezo huo kusaka heshima ya baada ya kushindwa kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo msimu huu.
Akizungumza baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha wa Simba, Steve Barker alisema ameridhishwa na kikosi alichokuwa nacho.
“Hivi sasa ninachohitaji ni timu yangu kushinda mabao mengi hasa katika mchezo dhidi ya Stade Malien na kuweka heshima.
“Sitaki kuona timu inafunga mabao machache, nahitaji kuingia katika mchezo huo wa kimataifa kwa kuhakikisha tunashinda mabao mengi na kuweka heshima katika michuano ya CAFCL,”alisema.
Barker alisema kuwa anajua mchezo utakuwa mgumu lakini hana hofu kwani wanahitaji kupata ushindi ili kuweka heshima baada ya kushindwa kutinga robo fainali.
“Utakuwa mchezo mgumu na wenye ushindani mkubwa, lakini hatutakubali kupoteza tunachohitaji ni kupata ushindi, tuweke heshima,” alisema Steve.
Kocha huyo alisema kwamba hana hofu na timu yake kwani ana imani kubwa na wachezaji aliokuwa nao kuwa watajituma na kufanya vizuri.
Wakati huo huo, Ofisa Habari wa timu hiyo, Ahmed Ally alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo tayari yamekamilika.
Alisema baada ya mchezo wa dhidi ya KMC, kikosi kilirejea kambini kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuikabili Stade Malien.
“Mchezo dhidi ya Stade Malien pamoja na kwamba hakuna tunapokwenda lakini sisi tumeupa thamani, tunataka kila shabiki wa Simba aone ni mchezo mkubwa, kwetu ni mchezo muhimu kwelikweli, hata kama tumefanya vibaya hatua ya makundi lakini hatutaki kuona Simba yetu inafanya vibaya zaidi, tunataka kwenda kusimia heshima ya mnyama.
“Wachezaji wetu wanaendelea vizuri ukitoa Wilson Nangu ambaye taarifa ni kwamba mwishoni mwa wiki tutampeleka Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji, ameumia kifundo cha mguu, baada ya upasuaji tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kusema atakuwa nje kwa muda gani.
“Kwa upande wa Yakubu Suleiman maendeleo ni mazuri na muda wowote atarejea kikosini.” alisema Ahmed.
Alisema kuwa msimu huu hawajafanikiwa kupata ushindi wowote Uwanja wa Mkapa katika michuano ya CAFCL, hivyo imani imepotea kwa mashabiki lakini wamejipanga kuirejesha katika mechi hiyo.
“Simba hatupo tayari kupoteza mara mbili dhidi ya Stade Malien. Tumewahi kufungwa na wengine kama Al Ahly lakini walipokuja kwa Mkapa tuliwarudishia. Hii ndiyo falsafa ya Simba, kama ilivyokuwa kwa Petro ndiyo itakuwa kwa hawa wengine,” alisema.
Aliongeza kuwa jambo moja la msingi ni kwamba dunia nzima itakuwa inaangalia mechi hii, hivyo watajitahidi washinde.
Hii ni mara ya pili kwa Simba kuishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 2003.
Katika mismamo wa kundi D linaongozwa na Stade Malien yenye pointi nane ikifuatiwa na Esperance yenye pointi sita huku Petro Luanda ikiwa na pointi tano na Simba ina pointi moja.




