Na NASRA KITANA
LICHA ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi ya Kenya katika Kombe la Kagame, Kocha wa Singida Black Stars, Miguel Gamondi, amesema bado kikosi chake hakina muunganiko mzuri.
Singida ilipata ushindi huo katika mchezo wake wa pili wa michuano hiyo uliopigwa katika Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam.
Awali, miamba hiyo ilitoka suluhu ilipovaana na Ethiopia Coffee ya nchini Ethiopia.
Gamondi alisema kutokana na muda mfupi aliokuwa nao tangu ajiunge na timu hiyo, wachezaji bado hawajafikia muunganiko anaoutaka.
Kocha huyo alikiri kwamba kuna wakati wanashindwa kudhibiti mchezo kutokana na wachezaji wake kutozoeana vya kutosha, jambo linalosababisha makosa ya mara kwa mara uwanjani.
“Tumepata ushindi lakini sijapata muunganiko ndani ya kikosi changu, nitaendelea kupambana kuijenga timu iweze kuwa vile ambavyo ninahitaji,” alisema.
Kocha huyo alisema kwamba kadri siku zinavyosonga na wachezaji wakipata mechi zaidi za ushindani, changamoto hizo zitapungua na timu itaonekana bora zaidi.
Wakati huo huo, Gamondi alisema katika mechi mbili zilizopita za mashindano ya Kagame, alikosa huduma za wachezaji wake muhimu akiwemo Khalid Aucho na Marouf Tchakei.
Wachezaji hao kwa mujibu wake wana mchango mkubwa katika kuongeza nguvu na ubora wa kikosi hicho na kurejea kwao kutakuwa na maana kubwa katika malengo ya timu.
Naye kocha wa Polisi Ettiene Ndayiragije alikiri kwamba kuna wakati wanashindwa kudhibiti mchezo kutokana na wachezaji wake kutozoeana vya kutosha, jambo linalosababisha makosa ya mara kwa mara uwanjani.
Alisema kadri siku zinavyosonga na wachezaji wakipata mechi zaidi za ushindani, changamoto hizo zitapungua na timu itaonekana bora zaidi.
“Kikosi changu kimeleta somo baada ya kupoteza mchezo huo hivyo tunakwenda kujipanga upya tupate ushindi katika mchezo unaofuata,” alisema.
Ndayiragije alisema wapinzani wao ni timu yenye uzoefu mkubwa na waliweza kudhibiti mchezo hata walipokuwa chini ya presha.