NA HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
IKIWA leo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa Zanzibar kinazindua kampeni zake, Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama hicho Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza kuwa, CCM itafanya kampeni za kistaarabu, itahubiri amani, umoja, mshikamano na kuondoa ubaguzi katika jamii.
Amesema, kuna baadhi ya vyama ambavyo havina sera na badala yake, wapo kuhubiri chuki na mgawanyiko jambo, ambalo litasababisha kuivuruga amani iliyopo nchini.
Dk. Mwinyi, aliyasema hayo Mjini Unguja, alipokutana na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari.
“Binafsi mimi niliwahi kusikia watu wapo katika majukwaa, sijawasikia hata siku moja wakinadi sera zao, pengine, hawana kwa sababu serikali ya awamu ya nane, imefanya kila kitu, ndiyo maana wamebaki kuhubiri chuki,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Ukipanda katika jukwaa leo kuzungumzia elimu utasema nini? utaishinda vipi CCM katika elimu, badala yake utageuza maneno badala ya kuzungumza elimu, afya, maji na mengineyo utaanza kusema huyu kafanya hivi, sasa hapo unamsaidiaje mzanzibari katika hilo?,” alisema.
Alisema kuna kila dalili kwamba, miaka yote ya uchaguzi kipindi kama hiki kunakuwa na sintofahamu na sasa hivi kumetulia kabisa na kusisitiza kuendelea namna hivyo hadi zitakapomalizika kampeni.
“Kuanzia Kesho (leo) mtawasikia katika majukwaa, badala ya kusema mtafanya nini kuwafanyia wazanzibari basi wao watakuwa wanawasema watu, nyie sikilizeni achaneni nao, tunaomba wasihimize au wasihubiri mgawanyiko, mfarakano, chuki katika nchi,”alisema.
Alieleza kuwa, Wazanzibari wanataka kuendelea kubaki na amani iliyopo hivyo alivisistiza vyama vyengine kuhubiri amani na kuacha kufanya siasa za chuki.
Aidha, Dk. Mwinyi aliwaomba waandishi wa habari kuhubiri na kuandika amani na wale ambao wanahubiri chuki basi kuachana nao.
“Nyinyi waandishi wa habari mna nguvu kubwa sana hivyo nawaomba tuandike amani, wale ambao wanahubiri chuki basi tuachane nao, ukichukua wewe mwandishi ukaandika maneno ya chuki, basi kalamu yako ina nguvu sana,” alisema
Aliongeza kuwa: “Huu kwangu ni wito kwenu nikitambua umuhimu wa ninyi waandishi na vyombo vyenu katika maswala ya amani katika nchi,tujitahidi kuidumisha amani tuliyonayo ili tuweze kupata maendeleo zaidi,” alisistiza Dk. Mwinyi.




