Na HANIFA RAMADHANI,
Zanzibar
MGOMBEA Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema serikali itaendelea kuwajengea uwezo vijana katika kuwapa ujuzi kuhakikisha wanaelimika.
Dk. Mwinyi, ameyasema hayo huko Tunguu Kusini Unguja, akizungumza na vijana wa vyuo vikuu na makundi mbalimbali ya vijana, ukiwa ni mwendelezo wa kampeni zake za Urais za kukutana makundi tofauti.
Amesema akipata ridhaa ya kuwaongoza tena Wazanzibari, atahakikisha kuwa, anafanya kila linalowezekana, kuendelea kuongeza bajeti ya elimu, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na wale wa ngazi ya Diploma.
“Ninyi vijana ndiyo viongozi, ni kundi muhimu sana ambapo zaidi ya asilimia 65 ya wapiga kura wote ni vijana, hivyo ni lazima mjengewe uwezo mpate elimu bora,” amesema
Amesema Serikali ya Awamu ya Nane ilipoingia madarakani, bajeti ya sekta ya elimu ilikuwa ni sh. bilioni 80, hadi sasa bajeti ya Wizara ya Elimu, imefikia sh. bilioni 864.
“Kwa hivyo, kipaumbele cha kwanza tulichotoa ni elimu kwa sababu, tunataka vijana wetu katika nchi hii, waelimike,” amesema.
Akizungumzia bajeti ya mikopo ya elimu ya juu, Dk. Mwinyi amesema ilikuwa ni sh. bilioni 13, hadi kufikia mwaka huu, bajeti hiyo imepanda kufikia sh. bilioni 37.
Hivyo, amesema ndiyo maana vijana wanaopata mikopo, wamefikia 20,000 kutoka 8,000 waliokuwa wakipata mikopo hiyo.
Aidha, amesema serikali ilifanya maamuzi ya makusudi ya kutoa mikopo kwa wanafunzi, kuanzia ngazi ya Diploma ambapo tayari vijana 3,500 wa ngazi hiyo, wamepata mikopo ya serikali.
“Yote haya yanaonesha kipaumbele tulichokiweka katika elimu, kwa kutambua kwamba, tunawajengea uwezo vijana tunapowapa elimu,” amesema.
Amesisitiza kuwa, serikali itaendelea kuwajengea uwezo katika elimu kuanzia ngazi zote na kuendelea kuvijenga vyuo vya mafunzo ya elimu ya amali, vijana wanaokosa kuendelea katika elimu ya juu, wajifunze ufundi.
Amesema kundi la vijana, lina umuhimu wa pekee katika kufanya maamuzi au hatma ya uongozi nchini, kwa sababu idadi kubwa ya wapiga kura visiwani Zanzibar ni vijana ambayo ni asilimia 65.
Amesema serikali ya Chama Cha Mapinduzi, inatoa upekee maalumu kwa masuala yote yanayohusu vijana na kwamba, wanachotaka ni kupata fursa ambazo zipo katika maeneo matatu ambayo ni elimu, ajira na uongozi.
Dk. Mwinyi, amewahakikishia vijana hao kuwa, katika awamu ya pili akipata ridhaa, serikali yake itavuka lengo la kuajiri, itatoa ajira zaidi ya 350,000.
Amesema anatambua changamoto hiyo, imekuwa kubwa kwao na kwamba, atahakikisha vijana wengi zaidi, wanapata ajira katika uongozi wake.
DK. DIMWA
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Mohammed Said Mohammed, aliwataka vijana kuhakikisha kuwa, wanawahamasisha wenzao, kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29, mwaka huu.
Alisema vijana wanatakiwa kuwa mstari wa mbele, kuhimizana kuhusu suala zima la amani, umoja na mshikamano kwa mustkabali mpana wa maisha yao ya sasa na baadae.




