Na IRENE MWASOMOLA
TUME Huru ya Uchunguzi, kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya Uchaguzi wa Oktoba 29, mwaka huu, imeainisha mambo mbalimbali yatakayochunguzwa.
Pia, imeahidi itakuwa huru na baadhi ya ushahidi utakaochukuliwa kwa mashahidi, utaambatana na watakaohojiwa kula kiapo.
Miongoni mwa mambo yatakayochunguzwa na Tume hiyo ni chanzo halisi cha ghasia, madhara yaliyojitokeza vikiwemo vifo, watu kujeruhiwa na uharibifu wa mali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, alisema Tume hiyo, itafanya kazi kwa siku 90 kuanzia Novemba 20, mwaka huu, aliwataka wananchi na makundi mbalimbali kutoa ushirikiano.
“Tutachukua ushahidi utakaotumika siyo tuchukue ushahidi ambao hauwezi kutumika, ndiyo maana kwenye mambo mengine, itabidi tuchukue ushahidi chini ya kiapo,” alisema.
MAMBO YA KUCHUNGUZA
Pia, Jaji Chande alitaja jambo la nne litakalochunguzwa ni mazingira, hatua zilizochukuliwa kubaini na kukabiliana na ghasia zilizojitokeza.
Alisema jambo la tano ni kupendekeza maeneo yanayohitaji kuimarishwa zaidi ili kuongeza uwajibikaji wa viongozi na raia katika kulinda amani, utawala wa sheria, haki za binadamu na utawala bora.
Aidha, Tume hiyo, itachunguza jambo lolote ambalo itaona ni muhimu na linaendana na majukumu yake.
Mbali na mambo hayo sita, Jaji Chande, alisema baadhi ya ushahidi, utachukuliwa kwa faragha na mazingira maalumu, kuwaepusha watoa ushahidi kupata madhara iwapo watabainika wametoa ushirikiano kwa Tume.
“Uchambuzi wetu wa haraka, tumeangalia na kuona Watanzania wenzetu wanataka nini, wanataka uchunguzi kamilifu usifanyike nusu nusu, pili wanataka tuwe wa wazi kwenye kazi,”aliongeza.
MAKUNDI YA KUHOJIWA
Jaji Chande, alisema Tume itahoji wadau mbalimbali wakiwemo waathirika wa vurugu, watuhumiwa, vyama vya siasa, asasi za kiraia na vikundi vya waendesha pikipiki maarufu bodaboda.
Pia, aliwataja wengine ni vyombo vya ulinzi na usalama, waandishi wa habari, watafiti na wamachinga.
Jaji Chande, alisema watatumia mbinu mbalimbali za kuyafikia makundi hayo, wakiwemo vijana kwa kuwa, anaamini wana majibu mengi ya kile kilichotokea.
Pia, alisema Tume itatumia utaratibu kama wa Mahakama kwa kutoa wito kwa mtu kufika kuhojiwa.
Alisema watafanya kazi kwa weledi kwa kuwa, Tume hiyo itapimwa ndani na nje ya nchi, huku akiwataka Watanzania kuipa muda ifanye kazi yake kikamilifu.
“Msitupime kabla, lakini sisi tunaelewa tumejikita kwa Watanzania wanataka nini tuwape nini, kama njia moja ya kupona kilichotokea, wote tupo kwenye maumivu makubwa, lakini tuone tunajiponyesha vipi,”aliongeza.
Novemba 18, mwaka huu Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliunda Tume hiyo baada ya kutokea vurugu na uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29.
Hatua hiyo, ilikuwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyotoa akihutubia Bunge la 13 Jijini Dodoma, ambapo aliahidi kuunda Tume Huru ya Kuchunguza tukio hilo.
Mbali ya Mwenyekiti Jaji Mstaafu Chande, wajumbe wa Tume ni aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Balozi Dk. Stergomena Tax, Jaji Mkuu Mstaafu Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue.
Wengine ni Balozi Paul Meela, Balozi David Kapya, Mwanadiplomasia Balozi Radhia Msuya na Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu Said Mwema.




