Na ATHNATH MKIRAMWENI
SERIKALI imewahakikishia Watanzania upatikanaji wa dawa za ARV, haujatetereka nchini.
Pia, Serikali imewekeza sh. bilioni 189 kutoka vyanzo vya ndani kupata ARV, vifaa vya maabara na usafirishaji wa sampuli, hatua ambayo imewezesha upatikanaji wa dawa kuwa wa uhakika asilimia 100 kutokana na akiba iliyopo hadi Oktoba, mwakani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Ulemavu), William Lukuvi alisema upatikanaji wa dawa za ARV, hautetereki na huduma zote zinazohusiana na VVU na Ukimwi, zinaendelea kutolewa bure na serikali.
Lukuvi alisema serikali inaendelea kuhakikisha kuwa dawa za ARV, zinapatikana kwa urahisi katika vituo vyote vya afya nchini na huduma za matibabu na matunzo, zinatolewa bure kwa wote wanaohitaji.
Alieleza mbali na changamoto za kimataifa za upungufu wa rasilimali, Tanzania haijakutana na upungufu wa dawa za ARV.
Alisema serikali imewekeza rasilimali za ndani, ikiwemo kuimarisha Mfuko wa Ukimwi kwa lengo la kuhakikisha huduma za matibabu zinaendelea kutolewa bila usumbufu.
Pia, alisema Serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za maabara na ongezeko la mashine za kupima kiwango cha vvu mwilini.
Lukuvi aliwasisitiza wadau wote kuunga mkono juhudi za kitaifa za kumaliza ukimwi kama tishio la afya ya umma ifikapo mwaka 2030 likiwa ni lengo linaloendana na ahadi za kimataifa.
Aidha, alisema asilimia ya watu wanaojua hali zao za vvu iliongezeka kutoka asilimia 91 hadi 92, kiwango cha matumizi ya matibabu asilimia 98 hadi 98.5 na kiwango cha kukandamiza virusi asilimia 97 hadi 98.1.
Idadi ya vituo vya matibabu na huduma kutoka 7,805 hadi 8,203, uwezo wa uchunguzi wa virusi umeimarika kwa kuongezwa kwa mashine za uchunguzi nchi nzima.
Hata hivyo, Lukuvi alieleza wasiwasi kuendelea kwa maambukizi mapya ya vvu miongoni mwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, ambao wanachangia asilimia 33 ya maambukizi mapya.
Alisema wanawake vijana wanachangia asilimia 80 ya maambukizi, lakini Serikali inaendelea kutoa elimu shuleni na jamii.
Pia, alisema Serikali inakagua upya Sera ya Kitaifa ya VVU na Ukimwi iendane na mwelekeo wa kimataifa na kuimarisha majibu ya kitaifa.
Naibu Waziri wa Afya, Dk. Florence Samizi, alisema serikali imewekeza sh. bilioni 189 kutoka vyanzo vya ndani kupata ARV, vifaa vya maabara na usafirishaji sampuli.
Akizungumza kwa niaba ya watu wanaoishi na vvu, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na VVU, Leticia Kapela alisema ARV zinatolewa bure, zinapatikana na zina ubora.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, Dk. Samwel Sumba, alisema zaidi ya Watanzania milioni 1.5 wanaoishi na VVU, wanapata matibabu.




