Na VICTOR MKUMBO
MAGWIJI wa soka nchini, wameibuka na kutoa maoni yao baada ya Kocha wa Taifa Stars, Miguel Gamondi kutangaza wachezaji wa awali watakaochujwa kuunda kikosi kitakachoiwakilisha Tanzania katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025), zitakazoanza mwezi huu nchini Morocco.
Kocha Gamondi ametangaza kikosi cha awali chenye wachezaji 50 ambapo baadaye watafanyiwa mchujo kuunda timu hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao Mtemi Ramadhan, Charles Boniface Mkwasa na Ken Mwaisabula walisema kocha anatakiwa kuangalia wachezaji wa muhimu kuhakikisha wanampa matokeo chanya katika michuano hiyo.
Mtemi Ramadhan akizungumza kwa njia ya simu kutoka Jijini Dodoma alisema ana imani lengo la kocha huyo ni kusuka kikosi kazi.
“Nimesoma majina ya nyota walioitwa na kocha, wapo wachezaji wakongwe na wengine ni wachezaji wapya, nina imani hao watakuwa msaada mkubwa kwa timu yetu kufanya vizuri,” alisema Mtemi ambaye aliwahi kuichezea Simba kwa mafanikio makubwa.
Aliongeza kuwa kitendo cha kuchanganya damu mpya na wakongwe kitakuwa kizuri kwani wachezaji kama Mbwana Samatta na Simon Msuva wanaelekea kustaafu kucheza soka.
Mchezaji wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka, Kenny Mwaisabula alisema kuwa kocha ameteua wachezaji wengi kuhakikisha anafanya mchujo wa kupata kikosi imara.
“Nampongeza kocha kwa kuchagua wachezaji wengi kutoka katika kila timu na kuhakikisha anatengeneza kikosi chenye muunganiko mzuri.
“Wachezaji wote walioitwa katika kikosi cha awali wana kiwango kizuri, bado tuna muda wa kukiandaa na kuhakikisha tunafanya vyema katika fainali za AFCON msimu huu.
“Ninaamini kocha amefanya kuchagua wachezaji wenye kiwango, hivyo baada ya mchujo ninaamini kitakapatikana kikosi bora zaidi cha ushindi,” alisema.
Kocha na mchezaji wa zamani, Charles Mkwasa alisema kuwepo wachezaji wengi siyo kibali cha kwenda kufanya vizuri, ila kocha anatakiwa kuchagua wachezaji wenye kiwango bora cha kwenda kushindana.
Alifafanua kuwa kocha Gamondi anatakiwa kuangalia nafasi ambazo anazihitaji kwa ajili ya kuhakikisha kikosi kinakuwa bora.
Alisema timu pinzani zitakuja na wachezaji wenye kiwango bora zaidi, hivyo kocha anatakiwa kutengeneza kikosi cha aina yake na kuwachagua wachezaji ambao siyo waoga kupambana kusaka matokeo chanya.
“ Wenzetu kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), watakwenda na wachezaji wote wazuri wanaocheza nje ya nchi yao, kwani wamejipanga kwenda kushindana na siyo kushiriki, hivyo kocha ana kazi ya kuchagua wachezaji wenye kiwango bora kuhakikisha anafikia malengo aliyojiwekea,” alisema.
Kwa upande wake kocha na mchambuzi wa soka, Joseph Kanakamfumu alisema kocha hatakiwi kwenda mbali sana na kikosi cha mwisho kilichocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Kuwait.
Alisema wachezaji hao wanatakiwa kuongezewa nguvu kwani kuna umuhimu wa Mbwana Samatta na Simon Msuva kutokana na historia zao katika soka.
“Kocha anatakiwa kutokwenda mbali sana na kile kikosi cha awali ambacho kilicheza na Kuwait kwani walionyesha kiwango bora.
“Wachezaji wa kile kikosi cha awali wanatakiwa kuongezewa nguvu wakiwemo Samatta na Msuva kwani wana umuhimu mkubwa katika michuano ya AFCON msimu huu,” alisema.




