Na ELIZABETH JOHN
JESHI la Polisi, limesema limebaini mbinu ovu 12 zilizopangwa na wanaokusudia kuandamana Desemba 09, mwaka huu, yakiwemo matumizi ya silaha za moto.
Aidha, limesema linachukua hatua madhubuti kukabiliana na wimbi la uhalifu wa kimtandao na mipango ya vurugu inayodaiwa kuhamasishwa kupitia mitandao ya kijamii.
Kauli ya Jeshi la Polisi, imekuja siku moja baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuwahakikishia Watanzania, kuwa serikali itaendelea kulinda nchi, mipaka, raia na mali zao wakati wote.
Rais Samia, alitoa kauli hiyo, alipowahutubia Watanzania kupitia mkutano wake na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, (JNICC).
Taarifa ya Polisi iliyotolewa na Msemaji wake, DCP David Misime, imesema Jeshi hilo, linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda maisha ya wananchi na mali zao, huku likihakikisha amani na utulivu, vinaendelea kuimarika nchini.
“Hicho wanachohamasisha na kukiita maandamano ya amani, mtu yeyote aliyewasikiliza na akaendelea kuwasikiliza, wanahamasishana na kuelekezana, ambaye hajui kutumia silaha na hajapitia mafunzo, siku hiyo asishike silaha, wawaachie waliopata mafunzo ya matumizi ya silaha. (Kwa maana rahisi, watu hawa wanazo silaha za kutimiza lengo ambalo wamekusudia).
“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, vimekuwa vikifuatilia kwa karibu sana yanayoendelea katika mitandao ya kijamii na katika makundi sogozi, wakihamasisha wanayoyaita maandamano ya amani yasiyo na kikomo Desemba 9, mwaka huu,” ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Misime, kupitia mitandao na klabu mbalimbali za mtandaoni, Polisi wamebaini kuwa waandamanaji wanahamasishana siku hiyo kusiwe na shughuli yoyote itakayoendelea na kuhakikisha wanaharibu na kuchoma moto minara ya mawasiliano.
Mengine yaliyobainika, wanahamasishana wahakikishe Bandari ya Dar es Salaam haifanyi kazi, wafunge barabara zote za kuingia na kutoka katika mipaka yote, vijana wakapore mali za watu kwa sababu wanacho kisingizio kwamba, njaa inawasukuma kufanya hivyo na kuzuia huduma zisitolewe hospitalini.
Pia, alisema wanahamasishana kuwafuata walipo watumishi wa serikali kuwadhuru.
“Wapo wengine wameapa na kutamka watakaoandamana wasifike katika mitaa yao, kwani watawashughulikia ipasavyo, wengine wanasema hawatokubali kupata hasara,” alisema.
“Huo ni uhalifu mkubwa unaoendelea kuhamasishwa, hali kama hiyo kwa nchi yoyote duniani, ni tishio kubwa la maisha ya watu, uchumi wa nchi na masuala yote ya kijamii,” alisema.
Hivyo, alisema Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kwa nafasi zao kuepuka wanayoyahamasisha, kwani yamelenga kuharibu taifa na kurudisha machungu na madhara yaliyotokea nyuma.
“Taifa letu linahitaji uponyaji kama jitihada za viongozi wetu wa kitaifa zinavyoendelea kufanyika hivi sasa na hatuhitaji tena vurugu,” alisema.
Kuhusu sherehe za mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka, Misime alisema Jeshi la Polisi, linawahimiza wananchi waendelee kuzingatia usalama wa maisha na mali zao.
Alisema watakaosafiri kwenda mikoa mbalimbali, wahakikishe wanaacha waangalizi au walinzi katika makazi yao.
Vile vile wazingatie sheria za usalama barabarani na kufuata ishara mbalimbali zilizopo barabarani kuepuka ajali.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi linawahakikishia wananchi wote wapenda amani, kwamba litaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kulinda maslahi ya taifa, maisha ya watu na mali zao.




