Na NASRA KITANA
WAKATI kikosi cha Yanga kikitarajiwa kushuka dimbani leo kumenyana na Fountain Gate FC, mashabiki wanajiuliza Fountain Gate inaweza kuitibulia Yanga leo?
Yanga hadi leo hii, imefunga mabao manane katika michuano hiyo ikifuatiwa na Simba ambayo imepachika mabao saba huku zote zikiwa hazijapoteza mechi msimu huu.
Pia, Yanga imeruhusu nyavu yake kutikiswa mara moja, imeshinda mechi tatu na kutoka sare mchezo mmoja wa michuano ya ligi hiyo.
Katika msimamo wa ligi, Yanga ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 10 baada ya kushuka dimbani mara nne huku Fountain Gate FC ikiwa nafasi ya sita ikijizolea pointi 10 baada ya kushuka dimbani mara tisa.
Kutokana na hali hiyo, kivumbi kinatarajiwa kuwepo leo kama Fountain Gate FC itafanikiwa kuwazuia Yanga kupata bao lolote katika pambano hilo.
Timu hizo, zinatarajiwa kushuka dimbani katika mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, kuanzia saa 10:00 jioni.
Kuelekea pambano hilo, Kocha wa Yanga, Pedro Concalves alisema kuwa lengo lake ni kuhakikisha wanashinda katika mchezo huo muhimu.
Pedro alisema kuwa wanatarajiwa kuwa na mchezo mzuri kwani wapinzani wao wamekuwa na matokeo tofauti katika ligi.
Alisema kuwa baaada ya kurejea kutoka Algeria hawajapata muda mrefu wa kujiandaa, safari ilikuwa ndefu sana, hivyo watahakikisha hawatoki nje ya mstari na malengo waliyokuwa nao.
Pedro alisema sifa kubwa ya timu yao ni kuhakikisha wanashinda katika kila mchezo haijalishi mashindano gani.
“Tunafahamu kuwa wapinzani wetu wamejiandaa vizuri pia, tunaheshimu kila mpinzani anayekuja mbele yetu, tutacheza kama mchezo wa ligi ya Mabingwa Afrika, falsafa yetu haitabadilka kwani dhamira yetu ni ushindi tu,” alisema.
Pedro alisema kwamba wataendelea kufanyia kazi changamoto ndogo ndogo za majeraha kwa baadhi ya wachezaji ambazo zinawasumbua ili kuona utayari wao kimwili.
Naye nyota wa timu hiyo, Khomein Abubakar alisema kuwa wamemalizana na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL), kwa hivi sasa, akili zote na malengo yao ni mechi za ligi kuu.
“Kila mchezaji anajua nini cha kufanya, tuliwekeza nguvu kubwa sana katika ligi ya mabingwa, lakini bado tupo imara kimwili na kiakili na tupo tayari kupigania alama tatu muhimu kwa mchezo wa kesho (leo),” alisema Khomein.
Nyota huyo aliwaomba mashabiki na wapenzi wa timu yake kuhakikisha wanajaa kwa wingi uwanjani ili kuwapa sapoti ya kutosha.
Kocha wa Fountain Gate FC, Mohamed Laizer alisema anajua wanaenda kucheza na timu bora lakini wamejipanga kufanya vizuri.
“Tumekuja kupambana ili kupata ushindi, tunajua tunaenda kupambana na timu bora yenye wachezaji wenye viwango lakini tunajua udhaifu wao, hatutakubali kupoteza mchezo,” alisema Mohamed.
Naye mchezaji wa timu hiyo Derick Mukombozi alisema kuwa kama wachezaji wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata ushindi.




