Na ZIANA BAKARI
BAADHI ya wadau wakiwemo, wasomi, wachumi, wanasiasa wakongwe ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), viongozi wa dini, wafanyabiashara na vijana, wameipongeza serikali kuanza kutekeleza ahadi ya kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Ahadi hiyo ambayo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aliitoa Agosti 28, mwaka huu, alipozindua kampeni ya uchaguzi mkuu wa CCM, Kawe jijini Dar es Salaam.
Alisema ndani ya siku 100 za uongozi wake, ataboresha huduma za afya kwa kuajiri wahudumu wa afya 5,000, wakiwemo wauguzi na wakunga.
Pia, aliahidi kuajiri walimu 7,000 wa masomo ya hisabati na sayansi, ikiwa ni mkakati madubuti wa kisayanisi wa kuhakikisha kila mtoto wa darasa la tatu, anaweza kusoma, kuhesabu na kuandika bila shida.
Kutokana na ahadi hizo kuanza kutekelezwa ndani ya siku tajwa zilizotangazwa na Rais Dk. Samia, wadau mbalimbali, walishauri ajira zilizotolewa ni vyema zisitolewe kwa upendeleo, badala yake, zitolewe kwa kila mwenye sifa na fani zilizotangazwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, baadhi ya wadau hao, waliwasihi vijana kuchagamkia fursa hizo, ambazo zitakuwa chachu kwa wao kujikimu kimaisha.
DK. MAGUO
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk. Mohamed Maguo, alisema Rais Dk. Samia, ana kila sababu ya kupongezwa kwa kusimamia ahadi aliyoahidi ya kuhakikisha ndani ya siku 100, atatoa ajira zitakazosaidia kuondoa wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana.
“Tunaamini vijana wenye sifa, watapata nafasi hizo, tunaiomba serikali suala la kutoa ajira kwa vijana, liwe endelevu kwa kuwa, wahitaji wapo wengi, niwaombe viongozi kubuni miradi ambayo itasaidia kuwa chachu ya kutoa ajira kwa vijana,”alisema.
PROFESA WANGWE
Mtaalamu wa Uchumi, Profesa Samuel Wangwe, alisema serikali imeanza vizuri utekelezaji wake kwa kutoa fursa za ajira kwa vijana hivyo, aliwasihi wahusika kuchangamkia fursa hizo na kutokata tamaa wanapotafuta kazi.
“Tunafahamu wimbi kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana, serikali imeanza mwanzo mzuri wa kuwaangalia vijana, niwaombe vijana kupendelea kujiajiri wenyewe kupunguza suala la ukosefu wa ajira,”alisema.
WANASIASA WAKONGWE
Mwanasiasa mkongwe nchini, Anna Abdallah, alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kusimamia vyema ahadi alizoahidi za kutoa ajira kwa vijana.
Akizungumzia umuhimu wa ajira hizo, Anna alisema zitasaidia kuondoa wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana ambayo ni changamoto katika jamii.
Aliyewahi kuwa, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga, alisema serikali inapaswa kupongezwa kwa kutekeleza ahadi kwa wakati.
Kwa mujibu wa Kanali Lubinga, utekelezaji umetekelezwa ndani ya muda uliotakiwa, hivyo aliomba wizara husika, kusimamia vyema suala la ajira kwa vijana.
VIONGOZI WA DINI
Shekhe wa Wilaya ya Temeke, Zairay Hassan, aliwasihi vijana watakaopata nafasi katika ajira hizo, kuwa waadilifu na kuheshimu kila mtu.
Alisema wapo baadhi ya vijana hujisahau mara wanapopata ajira na kuanza kutoheshimu wakubwa wao, jambo ambalo siyo zuri na halipendezi katika jamii.
MCHUNGAJI MSTAAFU
Kwa upande wake, Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Tabora, Isaya Mugaragu, aliwasihi wazazi kuwafundisha vijana wao kuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu hususan wanapopata ajira.
“Naamini vijana wanapokuwa na hofu ya Mwenyezi Mungu, hawataweza kufanya vitu vibaya wanapokuwa katika ajira zao, badala yake, watazingatia utiifu na uaminifu kwa wafanyakazi wenzao,”alisisitiza.
WAFANYABIASHARA
Aidha, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Machinga Complex, Stephen Lusinde, alimshukuru Rais Dk. Samia kwa kushirikiana na viongozi kutekeleza ahadi ya ajira kwa vijana, huku akiwasihi kutokata tama, bali waendele kuchangamkia fursa za ajira zinapotangazwa.
“Niiombe sana serikali, ajira hizo wanazotoa basi zitolewe kwa Watanzania kwa ujumla wenye sifa na fani husika, siyo kwa upendeleo, tukifanya hivyo, hatutasaidia kuondoa wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana,”alisema.
KATIBU UWAWADA
Naye, Katibu Mkuu wa Umoja wa Wafanyabiashara Walemavu Mkoa wa Dar es Salaam (UWAWADA), Jerome Chitumbi, aliiomba serikali kuendelea kutoa kipaumbele kwa walemavu hususan wanapotangaza fursa hizo za ajira.
Pia, alisisitiza kuwa, ajira zinazotangazwa zizingatie kutolewa kwa wenye sifa na siyo kutolewa kwa kujuana.
MAONI YA VIJANA
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana, (UVCCM), Tawi la Nzasa, Kijitonyama, Elias Mashauri, aliishauri serikali kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja, kutoa fursa za ajira kada ya ualimu ambayo itasaidia sehemu kubwa kuondoa wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana.
Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa Tawi la Mzimuni, Kawe jijini Dar es Salaam, Mohamed Sihaba, aliwasihi vijana wenzake, kuchangamkia fursa hizo ambazo zitakuwa chachu kwa wao kufikia malengo yao.
Mkazi wa Magomeni, Mariamu Kashanga, aliipongeza serikali kwa hatua hiyo ya utekelezaji wa kuongeza fursa za ajira kwa vijana ambapo itawasaidia sehemu kubwa ya wao kujikimu kimaisha.
Desemba 12, mwaka huu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, alisema serikali imeanza kutekeleza ahadi za Rais Samia alizoahidi kuzitekeleza ndani ya siku 100.
“Katika kufanikisha maelekezo hayo, serikali kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026, imefanikiwa kutoa vibali vya kazi 41,500, zikiwemo nafasi 12,000 za ajira ambazo ni ahadi ya Rais Dk. Samia, nafasi 5,000 ni upande wa afya na 7,000 ni kada ya ualimu wa masomo ya sayansi na hisabati,”alisema.




