Na MWANDISHI MAALUMU
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, amesema Tanzania imekuwa ni rejea muhimu ya amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani kote.
Guterres alisema hayo, alipotuma ujumbe kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Kombo na wenzake kutoka Tanzania.
Taarifa iliyotolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikino wa Afrika Mashariki, ilisema taswira ya Tanzania kama kielelezo cha amani, ilijaribiwa katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, mwaka huu ikiwa ni mara ya kwanza kukabiliwa na changamoto hiyo.
“Umoja wa Mataifa ungependa kuona Tanzania inaendelea kubaki katika umoja wake na kuwa mfano bora kwa mataifa mengine,” alisema Guterres alipokuwa akipokea ujumbe maalumu uliobeba salamu na ujumbe kutoka kwa Rais Dk. Samia.
Katibu Mkuu huyo alisisitiza umuhimu wa kuwepo mazungumzo ya kitaifa yenye maana, jumuishi na shirikishi kushughulikia chanzo cha matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29 na kutafuta njia za kudumu za kuzuia yasijirudie.
Aidha, aliahidi msaada kamili wa Umoja wa Mataifa wakati wote na hata baada ya Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa nchini Tanzania kukamilisha majukumu yake.




