Na WAANDISHI WETU
MVUA inayoendelea kunyesha katika mikoa mbalimbali nchini, imeleta madhara, ambapo baadhi ya nyumba zimeezuliwa na kuta kuporomoka.
Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa Nchini (TMA), imewataka wananchi kuchukua tahadhari, hasa katika mikoa 20 inayotarajiwa kukumbwa na mafuriko kufuatia mvua hizo.
Mkoani Morogoro mvua kubwa imenyesha na hadi sasa nyumba zaidi ya 120 wilayani Kilosa zimeezuliwa paa, kuta kuporomoka na zingine zikiharibika.
DC SHAKA
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, alisema mvua hiyo, iliathiri maeneo ya Tarafa ya Magole Kata za Dumila na Mgaole.
Shaka, alisema tathmini ya awali ilibaini zaidi ya nyumba 120 zimepata madhara mbalimbali.
Alisema kamati ya maafa inaendelea kufanya tathmini ya kina kupata idadi sahihi ya nyumba, wananchi walioathirika na kiwango halisi cha uharibifu.
Tukio lingine lililotokea usiku wa kuamkia jana mkoani Tabora, watu wanne akiwemo mjamzito walisombwa na maji wakiwa ndani ya bajaji.
Tukio hilo lilitokea Malolo, Manispaa ya Tabora ikiwa ni matokeo ya mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kumkia jana.
Dereva wa bajaji hiyo, Abdulrahman Amiri, alisema tukio hilo, lilitokea saa tano usiku, baada ya kuzingirwa maji mengi barabarani.
“Tulijaribu kubadilisha njia, lakini tulipokaribia eneo la barabara ya lami, tulikumbana tena na maji yaliyokuja kwa kasi na kusababisha bajaji kusombwa na kuingia mtaroni,” alieleza.
KAMANDA ZIMAMOTO TABORA
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Loshipay Laizer, alisema waliwaokoa watu hao ambao walipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tabora, Kitete.
Katika Kata ya Isevya mkoani Tabora, nyumba ya mkazi wa kata hiyo, iliangukiwa na nguzo ya umeme.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Azimio, Kata ya Isevya, Rahimu Kakuti, alisema nguzo ilianguka kabla ya kuchukua tahadhari kwa kuzima umeme.
DC SONGEA
Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, Ruvuma, Wilman Ndile, aliwatembelea wakazi wa Mtaa wa Mitendewawa kufuatia maafa ya kuanguka nyumba tisa kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali.
Akizungumza na wananchi wa mtaa huo, Ndile, aliwataka kuchukua tahadhari hususan katika ujenzi wa makazi yao.
Alisisitiza umuhimu wa kujenga nyumba imara kwa kuzingatia viwango na utaratibu wa ujenzi ili kupunguza athari za majanga yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
RC TANGA
Mkoani Tanga, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Burian, alisema hakuna madhara yaliyoripotiwa kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha mkoani humo.
Hata hivyo, alitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari haraka ili kulinda maisha na mali zao.
Batilda aliyasema hayo kufuatia mvua iliyoanza kunyesha usiku wa kuamkia jana na kuendelea kutwa nzima.
Akizungumzia hali ya usalama, alisema ofisi yake imekuwa ikiwasiliana kwa karibu na wakuu wa wilaya zote nane za mkoa huo Kilindi, Handeni, Korogwe, Lushoto, Pangani, Muheza, Mkinga na Tanga kukusanya taarifa za kina.
“Hadi mchana wa leo (jana), hakuna taarifa za maafa, majeruhi wala uharibifu mkubwa wa miundombinu zilizorekodiwa katika wilaya zetu zote nane.
“Mkoa wetu ni miongoni mwa mikoa iliyotajwa kuwa na mvua nyingi, hivyo ni lazima tuendelee kuwa macho,” alisema Balozi Batilda.
Alitoa agizo kwa wananchi wanaoishi maeneo hatarishi hasa mabondeni na nyumba ambazo zinaweza kuleta madhara kuhama mara moja.
“Nawaomba wananchi mnaokaa mabondeni au kwenye nyumba ambazo zinaweza kuezuliwa na upepo, hameni sasa.
“Lengo ni kujilinda na adha zinazoweza kusababishwa na mafuriko au nyumba kuporomoka,” alisisitiza.
Aidha, Batilda aliwataka madereva wa vyombo vya moto kuchukua tahadhari barabarani kutokana na utelezi unaosababishwa na mvua.
“Madereva mnatakiwa kuwa waangalifu zaidi kipindi hiki, mvua hupunguza uwezo wa kuona mbali na kufanya barabara kuwa na utelezi. Epukeni mwendokasi kujikinga na ajali ambazo mara nyingi hutokea kipindi cha sikukuu,” alisema Dk. Batilda.
DC KINONDONI
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, alisema wamejipanga vyema kuhakikisha mvua inazoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo, Dar es Salaam haileti madhara.
“Tumejipanga vyema na tutahakikisha Kinondoni haitapata uharibifu wa mafuriko kuelekea mvua iliyotangazwa na TMA,”alisema.
Mtambule alisema wanaendelea kutoa elimu ya utunzaji mazingira kwa wananchi kuhakikisha wanasafisha mitaro, mito na kutoziba njia za maji.
“Leo hii (jana) tutakuwa na kikao na baadhi ya viongozi kujadili mvua hii itakayonyesha, lakini lengo letu kuu litakuwa ni kuielimisha jamii kuhusiana na utunzaji mazingira hasa kipindi hiki cha mvua inayotarajiwa kuanza kwa wingi,” alisema.
Hata hivyo, aliwataka walioziba vichochoro kwa sababu moja au nyingine, kufungua maji yapite katika njia zake.
“Kuna sababu nyingi zinazofanya kuwepo mafuriko ikiwemo mitaro kujaa uchafu, kuziba njia za maji na kutosafisha mito vitu hivi mara nyingi vinasababisha athari za mafuriko,”alisema.
Vilevile, alisema katika wilaya yake, kuna baadhi ya shule zinakumbwa na mafuriko kwa sababu ya miundombinu yake, lakini hadi sasa, wamerekebisha kwa kuweka kifusi na kuhakikisha maji hayatuami katika maeneo korofi.
DC TEMEKE
Mkuu wa Wilaya ya Temeke , Sixtus Mapunda, aliwataka watu wanaoishi mabondeni, wachukue tahadhari au kuhama maeneo hatarishi.
Alitoa tahadhari kwa wanywaji pombe kipindi cha usiku, wasijaribu kupima maji kwa kutumia mguu.
Aidha, aliwataka wananchi hao, waimarishe majengo yao kwa lengo la kujiepusha na athari zinazoweza kujitokeza kipindi cha mvua.
“Sisi viongozi wa Wilaya ya Temeke, tumejiandaa kukabiliana na mvua inayoendelea kunyesha kwa baadhi ya mikoa, tutahakikisha Temeke yetu inakuwa imara siku zote.
DAS UBUNGO
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ubungo, Hassan Mkwawa, aliwataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa mto Gide na Kibwegele, kutunza mazingira ya mito huo.
“Hivi sasa tunashikiriana na maofisa wa bonde kusafisha mito na maji ya mvua yaweze kupita vizuri kuelekea baharini na kwa hali hiyo, wilaya yetu haitakuwa na mafuriko.
Pia, Mkwawa alisema wameanzisha mfumo wa kusafisha mitaro kuondoa taka zote.
Alisema wananchi walishashuhudia nyumba zikidondoka zilizokuwa pembezoni mwa Mto Gide, hivyo hali hiyo hawataki ijirudie.
“Hatutaki tena nyumba zidondoke na ndiyo maana, tumeanza mapema kusafisha mito na mitaro na wale wote nyumba zao zipo kandokando ya mto, wanatakiwa kuhama,” alisema.
DC ILALA
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliwataka wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na TMA, huku akionya vikali watu wenye tabia ya kutupa taka katika mitaro na kutiririsha maji machafu.
“Nawataka wananchi wa Wilaya ya Ilala wachukue tahadhari dhidi ya mvua hiyo. Pia, waepuke kutupa taka katika mito na mitaro kuepuka kuziba njia za maji na kusababisha athari ya mafuriko,” alisema Mpogolo.
Aidha, mkuu huyo wa wilaya, aliwatumia salamu za kheri ya mwaka mpya wananchi wake na kueleza mvua itakayonyesha iwe yenye kuleta heri, isiwe ya maafa ili wananchi waende kufanya shughuli zao za kiuchumi.




