Na AMINA KASHEBA
BONDIA wa ngumi za kulipwa, Mtanzania Frank Shagembe, leo atapanda ulingoni kuzichapa na Mghana Haruna Osumanu katika pambano la mkanda wa WBO Afrika uzito wa juu mwepesi.
Pambano hilo la raundi 10 litafanyika katika viwanja vya Posta vilivyopo Kijitonyama, Dar es Salaam.
Kabla ya pambano hilo, mabondia mbalimbali Watanzania watapanda ulingoni kuzichapa na wanamasumbwi kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafia Boxing Promotions ambayo ndiyo mwandaaji wa mtanange huo, Ally Zayumba, alisema maandalizi yamekamilika na kila bondia amejipanga kuonyesha kiwango kikubwa.
“Kutakuwa na mapambano 14 ndani yake, kutakuwa na mikanda saba ambayo itapiganiwa na mabondia kutoka Tanzania na wapinzani wao kutoka nje ya nchi, nina imani kutakuwa na mambo mazuri.
“Pambano kuu atacheza Frank Shagembe dhidi ya Osumanu kutoka Ghana ambao watagombania mkanda wa WBO Afrika,” alisema.
Zayumba pia alisema Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), itatumia jukwaa hilo kutambulisha mikanda mipya ya ubingwa wa taifa katika masumbwi ya kulipwa.
Bondia Shagembe alisema amejiandaa vyema kuonyesha kiasi gani anahitaji kuweka historia katika masumbwi nchini licha ya mpinzani wake kuwa na rekodi nzuri.
“Ninapanda ulingoni kuzichapa na bondia mahiri mwenye rekodi kubwa, nitahakikisha mkanda wa ubingwa wa WBO Afrika unabaki nyumbani kwani nimejipanga kushinda,” alisema.




