Na NASRA KITANA
MAKOCHA Pedro Goncalves wa Yanga na Steve Barker wa Simba, wamejipanga kupindua meza katika mechi za marudiano za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Simba na Yanga zitacheza mechi za marudiano za Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) huku Azam FC na Singida Black Stars zikishiriki Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC).
Katika mechi walizocheza ugenini, Simba ilipoteza 1-0 mbele ya Esperance de Tunis ya Tunisia ambapo zitarudiana Jumapili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam huku Yanga ikifungwa 2-0 na Al Ahly ya Misri.
Yanga na Al Ahly, mchezo wa marudiano utafanyika Jumamosi katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Katika Kombe la CAFCC, Azam FC ikiwa ugenini ilipata ushindi wa mabao 2-1, zitarudiana Jumapili katika Uwanja Azam Complex, Chamazi, huku Singida Black Stars iliyoshinda bao 1-0 dhidi ya Otoho d’Oyo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) itacheza mchezo wake wa marudiano Jumapili ikiwa ugenini.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Kocha wa Simba, Steve Barker alisema kuwa wanajua wamepoteza mchezo wa ugenini lakini atahakikisha wanapambana kupata ushindi katika mechi ya nyumbani.
“Tumepambana katika mchezo wetu wa ugenini, bahati haikuwa yetu, ila nitahakikisha tunapiga hesabu vizuri kwa kujenga timu yetu kuwa bora na kupata matokeo katika mchezo huo muhimu,” alisema.
Barker alifafanua kuwa wanaendelea kufanya marekebisho ya makosa waliyoyafanya katika mechi ya ugenini kuhakikisha wachezaji wanakuwa bora na kupata matokeo chanya.
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, alisema hesabu zao ni kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano hayo, watapambana mwanzo hadi mwisho kupata ushindi na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele.
“Tumepoteza mbele ya wapinzani wetu, lakini hiyo haijatuvunja nguvu kwani tumeanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu wa marudiano, tumepata majibu ya hesabu wapi tulikosea, tutapambana kufanya marekebisho tupate matokeo mazuri katika mchezo ujao,” alisema.
Pedro alisema hana hofu na kikosi chake kwani kila mchezaji ana morari ya kuhakikisha wanapata ushindi.
Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge alisema kuwa walikuwa wanahitaji alama tatu jambo ambalo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, hivyo wanakwenda kumaliza walipoishia katika mchezo wao wa marudiano.
“Tulikuwa tunahitaji alama tatu katika mchezo wetu na imekuwa hivyo pongezi kwa wachezaji namna ambavyo walijituma bila kuchoka, hivyo tunahitaji kumalizia kazi katika mechi yetu ya marudiano,” alisema.
Ibenge alisema kuwa malengo yao ni kuhakikisha timu inapata ushindi katika mchezo huo na kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.
Kocha wa Singida BS, Othmen Najjar alisema kuwa ushindi walioupata katika mchezo dhidi ya Otoho d’Oyo umewaongezea morari ya kutosha kuelekea katika mchezo wao wa marudiano.
“Tunajua mchezo utakuwa mgumu na wenye changamoto, lakini tutahakikisha tunapambana mwanzo hadi mwisho tupate matokeo mazuri na kusonga mbele,” alisema Najjar.
WACHAMBUZI WANENA
Wachambuzi wa soka nchini wamesema kuwa timu hizo bado zina nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano hayo na kutimiza malengo waliojiwekea.
Akizungumza jijini hapa, mchambuzi wa masuala ya soka nchini, Kennedy Mwaisabula alisema kuwa kwa hivi sasa timu hizo zinatakiwa kufanya mashambulizi ya mapema na kujilinda.
“Kwanza niwapongeze Singida na Azam FC kwa kazi kubwa waliyoifanya na kufanikiwa kupata ushindi, hivyo nina imani watapambana kusonga hatua inayofuata, lakini Simba na Yanga wanatakiwa kuongeza juhudi zaidi,” alisema Mwaisabula.
Naye mchezaji wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema kuwa kwanza wanajivunia kuwa na timu nne kimataifa na ana imani zitapambana katika mechi zao za marudiano ili kuweza kufanya vizuri zaidi.
“Simba na Yanga wamepoteza katika mechi zao za ugenini lakini nina imani wakipambana mwanzo hadi mwisho watapata ushindi na kusonga mbele zaidi na kutinga robo fainali ya mashindano hayo, lakini pia Singida na Azam wanatakiwa kuongeza juhudi zaidi ili kuendeleza ushindi wao,” alisema Pawasa.
Katika Ligi ya CAFCL, Simba ipo kundi D na inaburuza mkia baada ya kupoteza mechi zote tatu huku Yanga ikiwa kundi B ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi nne baada ya kushuka dimbani mara tatu.
CAFCC Azam ipo kundi B ikiwa nafasi ya tatu na kujizolea pointi tatu huku Singinda Black Star ikishika nafasi ya tatu na kujizolea pointi nne baada ya kushuka dimbani mara tatu.




