Na Jacqueline Liana
LEO ni siku ya kwanza ya mwaka 2026 baada ya kuuagana na 2025. Kibwagizo cha moja ya nyimbo za Bendi ya Sikinde kinauliza nani kauona mwaka? Nani kamaliza mwaka? Katika kibwagizo hicho kinahitimishwa kwa kuimbwa kwamba ni majaliwa yake Mungu kuuona mwaka mpya.
Kwa nini wanamuziki hao waliimba hivyo, jibu ni kwamba kumaliza mwaka mmoja na kuingia mwaka mwingine, aisee, zinahitajika kudra za Muumba wa mbingu na dunia.
Pia, huonywa kwamba, asiwepo binadamu wa kujipiga kifua kwa tambo na kusema ameuona mwaka mpya kwa jitihada zake binafsi, kwa kuwa wapo ambao walijitahidi kufanya hili ama lile, kuweza kuuona 2026, lakini kama wasemavyo Waswahili, jitihada haishindi kudra au kudura.
Kipindi cha mwaka mmoja ni kirefu katika maisha ya binadamu; kila mwaka hutokea mambo ambayo baadhi huacha alama na kumbukumbu za kihistoria kwa mtu mmoja mmoja, familia, ukoo, taifa na kimataifa.
Ndivyo ilivyokuwa mwaka 2025 kwa Watanzania, kila mmoja ataukumbuka kwa matukio ya furaha na huzuni pia, maisha ndivyo yalivyo, ni kama barabara ndefu isiyokosa kona.
Kitaifa Watanzania wameumaliza 2025, wakiwa bado na bumbuwazi la vurugu za Oktoba 29, ambazo zilitia doa jeusi katika amani ya Tanzania, ambayo siyo tu inasifiwa na Watanzania wenyewe, bali hata wananchi wa mataifa mengine.
Kutokana na amani ya Tanzania, nchi nyingine zikivurugikiwa wananchi wake hukimbilia nchini kujihifadhi tangu enzi za uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere hadi miaka ya karibuni.
Katika hilo, wananchi wa Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambao ni majirani na Tanzania, ni mashahidi kwa kuwa baadhi yao kama siyo wanaendelea kuishi nchini kwa amani, basi waliwahi kuishi wakiwa wakimbizi na kwa sasa wamerejea kwao.
Licha ya vurugu hizo, ambazo tayari Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameunda tume ya kuchunguza chanzo chake, Watanzania wamevuka kipindi hicho kigumu wakiwa wamoja huku amani ya nchi ikiendelea kushamiri.
Siku za mwishoni mwa mwaka jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, alisema, Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano wa amani katika Bara la Afrika na duniani kwa jumla.
Kauli ya mtendaji huyo mkuu wa UN, ni ushahidi dhahiri wa utambulisho wa kihistoria wa Tanzania kimataifa, hivyo hapana budi hadhi hiyo kulindwa na kudumishwa ndani ya miezi yote 12 ya 2026 na miaka chungu tele ijayo.
Guterres alisema, Tanzania wakati wote imekuwa ni rejea muhimu ya amani na mshikamano wa kijamii katika Bara la Afrika na duniani. Umoja wa Mataifa umekuwa ukishughulikia kurejesha amani katika nchi ambazo zimepoteza tunu hiyo kutokana na sababu mbalimbali; zikiwemo za vurugu, migogoro na hata vita kamili.
Guterres anaposema Tanzania ni rejea ya amani duniani; anajua mchango wa Tanzania katika kuhahikisha dunia ni mahali salama kwa kila binadamu kuishi.
Kauli ya Guterres kuhusu amani ya Tanzania ni ujumbe mzito kwa Watanzania kwamba hawana budi kujivunia amani ya taifa lao.
Ni miaka 64 sasa, tangu Tanzania ilipopata Uhuru Desemba 9, 1964 na kujijengea sifa ya kipekee Afrika na duniani ya kuwa taifa lenye amani na umoja, likivuka mipaka ya udini, ukabila, rangi ya ngozi ya mtu na hata itikadi za kisiasa, kuendelea kuwa lenye amani na umoja.
Amani ya nchi ilijaribiwa na kutoa somo kwa Watanzania linalowataka kuzingatia busara iliyopo katika methali ya “usione vyaelea vimeundwa”, amani ya Tanzania imeundwa, wapo walioumiza vichwa kuhakikisha inakuwepo na kudumu.
Matamanio ya kila anayewatakia mema Watanzania, ni kuona Tanzania inaendelea kuwa kinara wa amani kwa bara la Afrika na duniani, kwa sababu inategemewa pia na wananchi wa mataifa mengine.
Guterres anaposema kwamba Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani na mshikamano wa kijamii Afrika na dunia kwa ujumla, ni ukweli ambao unathaminiwa na wapenda amani ndani ya nchi na nje ya mipaka ya Tanzania.
Hatua ya Watanzania kuushinda ‘mtihani’ huo wa Oktoba 29, wakiwa wameshikamana, ni ujumbe kwa wanaharakati waliochochea vurugu hizo kwamba Tanzania ni taifa imara lenye watu wanaojitambua.
Watanzania kwa mshikamano wameendelea kuchapakazi, wakitekeleza kaulimbiu aliyoasisi ‘Kazi na Utu Tunasonga Mbele’ huku wakiitazama kesho yao kwa matumaini.
Tangu kupatikana kwa uhuru mwaka 1961, taifa limekuwa likijivunia amani ya nchi na hata kuwa kimbilio la raia wa mataifa mengine, kutafuta kujihifadhi baada ya amani kuharibika makwao.
Ni Bahati mbaya kuna baadhi ya watu wanaposikia amani ikisisitizwa kulindwa na kutunzwa hutoa maneno ya kejeli kwamba, amani ya Tanzania inatokana na upole wa Watanzania.
Hawa ni wale wanaopinga uwepo wa amani nchini unatokana na kazi ambazo zilifanywa na waasisi wa taifa Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume, ambao walihakikisha Watanzania wanaishi katika misingi inayosababisha uwepo wa amani nchini.
Ni katika hali ya amani ndipo maisha ya raia mmoja mmoja na taifa kwa jumla yanaweza kustawi, katika vurugu hakuna maendeleo kama ambavyo ilishuhudiwa. Changamoto hutatuliwa vyema kukiwa na amani.
Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, umoja na mshikamano. Haipaswi kuruhusu amani kuvurugwa, ilindwe kwa gharama yoyote kwa sababu thamani yake haina mfano kwa maisha ya Watanzania. Heri ya Mwaka Mpya 2026, amani ndiyo mpango mzima.




