Na SUPERIUS ERNEST
LEO ni siku ya kwanza ya Mwaka Mpya wa 2026, ambao watu wote duniani wanasherehekea sikukuu hii kubwa ya kimataifa.
Ni baada ya safari ndefu ya siku 365 za mwaka 2025, ambazo zilikuwa na muktadha tofauti kwa kila mmoja.
Wapo waliomaliza mwaka kwa furaha na wengine kwa huzuni, hata hivyo wote wanaanza mwaka mwingine mpya wa 2026 kadri walivyopata kibali cha Mungu.
Pongezi kwa wote kufanikisha kuvuka mwaka na kupata fursa nyingine ya kuanza mwaka mpya, hakika siyo kwa nguvu binafsi ni kibali cha Mwenyezi Mungu.
Watalaamu na wasomi wa duniani, husema mafanikio ya jambo hutambulika kwa mwanzo wake na mwisho wake.
USHAURI WA KITAALAMU
Safari hii ya mwanzo wa mwaka 2026, imewaibua wadau mbalimbali wakiwemo wa saikolojia, afya na viongozi wa dini wakishauri, namna njema ya kuukabili Mwaka Mpya wa 2026.
Kwa upande wake, Rais wa Chama Cha Wasaikolojia Tanzania, (TAPA), Magolanga Shegembe, ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, alisema ni vyema watu wanapoanza mwaka wakajipanga vizuri kisaikolojia kukabiliana na mazingira mbalimbali mema kwa mabaya yanayoweza kujitokeza.
Alieleza, japo watu wengi hawana utamaduni wa kujiandaa kisaikolojia katika kukutana na mazingira magumu lakini, ni muhimu wafanye hivyo wakikutana nayo wasiumie zaidi kisaikolojia na kiafya.
Sheghembi alisema kuamua mwaka unaazaje, inategemea na ulivyo umaliza mwaka ulioisha, kwani kama uliisha kwa changamoto hata kuanza kwake inaweza kuwa ngumu, kikubwa ni watu wajipange.
“Wapo waliopitia magumu na changamoto kubwa kinyume na matumai ni yao, hivyo wanaweza kuwa na maumivu makubwa.
“Wengine wanaweza kuchukulia kama sehemu ya kujifunza na wengine wakiona kama wamepoteza la msingi ni kuyatazama yale uliyopitia kama sehemu ya kujifunza na sio sehemu ya kukuumiza,”alisema.
Magelanga alisisitiza, kukubaliana na hali ya kile mtu alichopitia kuruhusu kuanza mwaka kwa akili mpya na mipango mipya.
“Watu watambue kuwa kuvuka mwaka ni fursa mpya ya mwaka huo, kupata na nafasi ya mpya ya kipekee aliyokupa Mwenyezi Mungu, kufanya kazi na kujijenga upya katika mipango yako,”alisema.
Alieleza kuwa, mtu anayekuwa na wakati mzuri ni yule anayezitazama changamoto kama fursa sio kama mateso au shida.
Magelanga alieleza kuwa, nafasi ya kuingia mwaka mpya ni kuanza mipango mipya majukumu mapya, kuongeza wigo zaidi ya vile ulivyofanya mwaka uliopita.
Alisisitiza, kuzitazama na kuzigeuza changamoto kuwa fursa ni njia njema na uwezo wa kuiandaa saikolojia yake na afya ya akili.
Kwa mujibu wa Magelanga, ni muhimu watu kutengeneza malengo, kuangalia uwezo wao, kuweka malengo yanayotekelezeka na kupimika yenye muda maalumu.
“Mfano, mtu anayeweka malengo ya kujenga nyumba walau msingi kwa mwaka ni tofauti na yule aliyeweka lengo la kutekeleza hicho kwa muda husika kama baada ya miezi minne, mitano au sita. Hivyo watu wanapoweka malengo ni vyema kuangalia muda maalumu,”alisema.
Alisema ukiwa na malengo bila kuweka muda ni ngumu kuyatimiza lakini, ukiwa na muda unaweza kujipima na kutekelezeka.
Magelanga alifafanua, kuweka malengo makubwa yasiyopimika na ambayo mtu hana uwezo nayo inaweza kusababisha sonona.
Alifafanua kuwa, safari ya kumaliza na kuanza mwaka ni binafsi, kila mtu na malengo yake na anatakiwa kuyatimiza.
Magelanga alihimiza kuwa, hata kama mtu alikumbana na magumu, changamoto nyingi ni vyema kushukuru kwa kuishi mwaka mzima hali hiyo inaweza kumpa mtu nguvu kisaikolojia na kuona anaweza zaidi.
“Ni vyema kila mtu ajitahidi kuwa na jambo la kushukuru na kujipongeza kwa yale aliyoyafanya kuliko kujilaumu, kwa kila jambo hali hiyo inashusha kujiamini na kuona kuwa hawezi kwa mengine.
“Pia, mwananchi jitahidi kuwa jambo ambalo linakupa faida na tija kuliko kujilaumu na kujuta wakati wote,”alisema.
Msaikolojia huyo, alisisitiza kutenga muda na kujitathimini hatua mtu aliyofikia na anayotaka kuyafanya.
Alisisitiza, watu kuweka malengo ya kufanya vizuri zaidi katika majukumu ya kila siku kifamilia na kijamii, kuliko vile alivyofanya kwa mwaka uliopita.
Alisisitiza watu kusamehe waliowakosea, kujisamehe wenyewe pale walipokea kwani hiyo inamfanya mtu kuwa mwepesi zaidi na kuondoa mizigo na uzito moyoni wa kufanya uamuzi.
“Kujitahidi kuwa safi na mwepesi katika mawazo, fikra na uhusiano, hivyo kuwa na nguvu ya kusonga mbele zaidi kuliko kurundika mawazo mengi na fikra hali inayosababisha tatizo la afya ya akili,”alionya.
Vilevile alihimiza kutunza uhusiano na watu wengine, kuanzia familia ambao ni utajiri wa watu kwani ni chanzo cha maendeleo na mafanikio zaidi.
“Hata kama umepitia magumu, changamoto, kubwa umekata tamaa, umepoteza wapendwa wako, fahamu kuwa huwezi kuwarudisha, jambo la msingi ni kukubaliana na hali kujipa faraja na kuona fursa ya kuanza mwaka.
“Pia, tuangalie ndugu walioumizwa, tuwatie moyo siyo kuwavunja moyo, itawasaidia kuwa nguvu na faraja ya kuendelea mbele,”alisema.
Pia, alisisitiza jamii kuwatafuta wataalamu wa saikolojia, wanaoweza kuwasaidia na kuwatoa katika changamoto za saikolojia.
Magelanga alieleza kuwa, kama mtu alivyo kuwa na daktari wake, anavyopeleka gari gereji, pia, wazoee kuwa na wataalamu wa saikolojia.
Alisisitiza, jamii kukaa kama familia, kutathmini pamoja na kuweka mipango, kuona namna ya kuendelea na kuepuka.
AFYA
Katika hatua nyingine, Daktari Bingwa wa magonjwa ya Moyo, Tulizo Sanga, ambaye ni Mkurugenzi wa Hospitali ya JKCI Dar Group, aliwapongeza wananchi kwa kumaliza mwaka mpya, ambao umekuwa na mafanikio makubwa.
Sanga alisema katika mwaka ulioisha wamekuwa na mafanikio makubwa, watu wengi walijitokeza kwa wingi kupata huduma za matibabu.
Alisema hivi sasa kuna maendeleo makubwa ya wananchi kujali afya zao na kuelimika, kwani wapo wanaokwenda kupima afya zao hata kama hawajawa katika hali hatarishi.
Kwa mujibu Sanga, jamii ijenga utamaduni huo na kuuendeleza kwani kama wanavyopeleka magari gereji vivyo hivyo, waweke muda maalumu wa kuwa wanafika hospitalini.
Dk. Sanga alisisitiza wananchi kuzingatia kanuni za afya, kufika hospitalini mara kwa mara na siyo tu pale wanapoumwa au kujisikia vibaya.
Alihimiza wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kuwapeleka watoto wao hospitali kuangalia afya zao mapema.
Dk. Sanga alisema, ni vyema kuchunguza wananchi wawe na afya bora ya moyo, kwani ndiyo injini ya mwili.
“Tunapoelekea mwaka mpya, kwa neema ya Mungu tuendelee kuitafuta afya yetu, iwe imara wakati wote, kutekeleza majukumu yetu.
“Sisi tumejipanga vyema kuwahudumia wananchi wakiwa na afya njema na kulijenga taifa, kwani taifa imara ni lile linalojengwa na wananchi wenye afya bora,”alisisitiza.
DK.KISENGE
Katika hatua nyingie, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya JKCI, Dk. Peter Kisenge, aliwasisitiza wananchi kujenga utamaduni wakupima afya ya moyo kupitia matawi yao mbalimbali yaliyopo nchini.
Dk.Kisenge alisema katika mwaka 2025, walifanya kazi kubwa ya kuwafikia wanachi kupitia huduma ya Rais Dk. Samia Tiba Mkoba, yenye lengo ya kufikishia wananchi huduma karibu.
“Hatutaki wananchi wapate shida, waingie gharama za kufuata huduma mbali, ndiyo maana tumetekeleza kwa kasi huduma ya matibabu ya moyo hata mwaka huu tutafanya hivyo zaidi,”alisema.
Alisema katika mwaka 2025, wamefanikiwa kufungua matawi mbalimbali ya JKCI likiwemo la Kawe, Oysterbay, Dar Group, Arusha na Chato, katika mwaka huu wataendelea kusogeza huduma karibu na wananchi.
Kisenge alisema katika mwaka huu wamejipanga vyema kuwafikia wananchi wengi zaidi, kuwapatia vipimo vya moyo na matibabu.
Alieleza kuwa, kampeni yao ni kuhakikisha hakuna mwananchi anayefariki dunia kwa kwa kukosa gharama za matibabu, ndiyo maana wanafanya jitihada za kuwafikishia huduma karibu.
“Kwa mwaka uliopita tulifka katika mikoa 16 na kuwahudumia wananchi wengi, kwa mwaka huu tumejipanga vizuri tunategemea kuwafikia wananchi wengi zaidi ya vile tulivyofanya mwaka jana,”alisema.
Alisema wanatoa vipimo bure vya moyo na magonjwa yasiyoambukiza kwa wananchi, kwa lengo la kulinda afya zao mapema kabla ya kuwa sugu na kutumia kuhitaji gharama kubwa kutibu.
Dk. Kisenge alisisitiza wananchi kujitokeza kupima afya zao, kujenga utamaduni huo kabla hawajawa katika hatari, kwani hatua hiyo itawawezesha kupata matibabu mapema na kuendelea na shughuli zao.
SHEIKH ALHAD
Vilevile, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano Tanzania, Sheik Alhad Musa Salim, alisema ni kuvuka mwaka ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kibali alichokitoa.
Alisema katika kipindi hiki, ni cha kujitathmini kila mmoja kwa mazingira yake kuanzia umri na maendeleo.
Sheik Alhad Alieleza, kila mmoja aone kuwa ana nafasi ya kujenga nchi, kudumisha amani ya taifa na kuwepo maendeleo.
“Katika mengi tuliyoyapitia tujifunze, kujitathimini na kujipanga upya, kutimiliza maisha na maendeleo,”alisema.
Alisisitiza wanandoa kujipanga upya kuepuka migogoro, kusameheana kwani migogo haijengi hivyo, yawepo maridhiano ya pamoja katika kujenga suluhu.
Sheik Alhad alisema msamaha ni sehemu ya tiba ya moyo, hivyo wananchi wasameheane na kusonga mbele zaidi kwa mafanikio.




