Na AMINA KASHEBA
BONDIA wa ngumi za kulipwa, Mtanzania Frank Shagembe, ametamba kwamba hapa nchini bado hajaona bondia wa kupigana naye na kama kuna mzawa anaamini ana uwezo huo, anamkaribisha ulingoni.
Shagembe ambaye hivi sasa ni bingwa wa WBO Afrika anayecheza uzito wa juu (kilo 76), amesema mabondia wenye uzito wake nchini wamekuwa wakihofia kuchuana naye.
“Hivi sasa akili yangu ni kucheza na mabondia kutoka nje ya nchi maana hapa nyumbani wananikimbia sana kwa kuhofia nitawapiga, hivyo nimeongea na uongozi wangu wanitafutie mapambano nje ya nchi, “amesema.
Bondia huyo amesema mkanda wa WBO utakuwa chachu ya kuzidisha mazoezi kwa bidii kwa sababu anahitaji kushinda mikanda mikubwa mingine.
“Hivi sasa nimezidisha muda wa kufanya mazoezi kwa sababu nina kiu ya kushinda mikanda mikubwa na kutangazwa jina langu katika anga za kimataifa,” amesema.
Bondia huyo aliwashauri mashabiki na Watanzania wategemee mambo mazuri kutoka kwake kwani amejipanga kuonyesha kiwango bora pambano hadi pambano.




