Na Mwandishi Wetu
KUMEKUWA na matukio ya ukatilki dhidi ya watoto kwa kiwango cha mtu kujiuliza kulikoni!
Serikali imekuwa ikichukua hatua dhidi ya uhalifu huo na mahakama imetoa adhabu kwa watenda ukatili, lakini hali haijakoma.
Ukatili dhidi ya watoto ambao hawawezi kujitetea kwa hili ama lile, umeendelea kutendwa na watu ‘makatili’ kwa viwango vya kutisha.
Watoto hufanyiwa ukatili wa aina mbalimbali; wa kijinsia, kimwili, kihisia, kisaikolojia na ule wa kingono ukijumuisha ubakaji na ulawiti.
Mama anashikwa na hasira inayoitwa ‘hasira kali’, anachukua mfuko wa ‘rambo’ anaufunga katika mikono ya mtoto na kuutia motoni.
Mikono ya mtoto inaungua; akiulizwa kisa cha yote hayo anajibu kadokoa mboga ya kuliwa jioni; hivi ni mtu mzima gani ambaye katika maisha ya utotoni hakuwahi kudokoa mboga?
Kama kuna watu wazima ambao hawajapitia utundu huo, hawawezi kujaa kiganjani, ni wachache na si ajabu anayemuadhibu mtoto kwa kiwango cha kumsababishia ulemavu wa maisha, alikuwa ni mdokozi ‘nambari wani’, lakini mama yake hakumtia motoni.
Watoto nyumbani kudokoa kitoweo au vyakula vingine ni sehemu ya makuzi yao; kinachotakiwa ni mzazi au mlezi kumkanya kwa adhabu isiyo ya kikatili, lakini itakayompa fundisho kwamba kudokoa dokoa ni tabia mbaya.
Udokozi wa sukari na maziwa ya unga unapendwa na watoto, hata wazazi wakiwakamata na kuuliza nani kadokoa sukari au maziwa, hakuna anayesema.
Sukari na maziwa ya unga, huwaumbua watoto wengi kwa sababu ushahidi ubaki nje ya mdomo, chembechembe za sukari au maziwa mama anapoziona, huuliza kuona watoto ni wa kweli kiasi gani, lakini mdokozi atakataa kuwa mdokozi ni yeye.
Iwapo kila mzazi angechoma moto mikono ya watoto wadokozi wa kitoweo; hasa nyama; nchi hii ingekuwa na watu katika makovu wengi sana wakiwemo viongozi wanaoheshimika.
Utoto ni hatua ya makuzi ya aina yake, weka maziwa ‘freshi’ kwenye friji kama hutakuta yameongezwa maji, unadhani nini kimefanyika? Je, utamchoma mdomo au ulimi?
Weka kopo la maziwa ya ‘laktojeni’ kwa ajili ya mdogo wao anayenyonya, kama hutakuta yamepungua kwa kiwango cha kutisha.
Utawaita kuwauliza nani amebugia maziwa ya mtoto, jibu litakuwa “siyo mimi mama”, tosheka na jibu hilo, toa adhabu za ‘saizi’ yao tena kwa busara siyo kuchoma moto viungo vya watoto, majuto ni mjukuu.
Watoto wanakimbia nyumbani wanatupa nguo za shule na mikoba ya madaftari porini, hawataki kurudi nyumbani kutokana na ukatili wanaofanyiwa, wanaona heri kulala nje mitaani!
Mtoto amekosa kakosa kidogo tu, mama wa kambo anamchongea kwa baba ambaye akili zake nazo ‘zimetekwa’ kimapenzi, anamuadhibu kikatili mtoto wake kwa ajili ya ‘kumfurahisha mamsapu’.
Nini kinachotakiwa kufanyika ili kukabiliana na ukatili ambao unafanyika dhidi ya watoto kwa sababu mbalimbali na kwa viwango tofauti nyenye madhara anuai hadi wengine kusababishiwa vifo, vilema vya maisha na hata kupotelea mitaani?
Kunahitajika busara katika kuwaadhibu watoto na siyo hasira, hasa ikizingatiwa ukatili wa aina mbalimbali una madhara makubwa kwa watoto; kiakili, kisaikolojia, kinafsi na kimwili.
Matukio ya watoto kwenda kinyume na inavyotarajiwa, yanaweza kusababisha uchungu na hasira, lakini kunahitaji busara siyo hasira za kuumiza watoto.
Ukatili dhidi ya watoto ni changamoto inayohitaji kushughulikiwa kwa haraka na kwa umakini. Ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha haki na ustawi wa watoto unalindwa.
Ukatili kwa watoto husababisha athari kubwa na madhara ya muda mrefu. Watoto wanaokumbwa na ukatili wanaweza kupata sonona, wasiwasi, na msongo wa mawazo.
Kuwa na majeraha na magonjwa yasiyopona, ukuaji na ustawi wao kudorora. Watoto walio na wanaofanyiwa ukatili hukosa kujiamini na huona ni bora kujitenga na jamii.
Kumekua na matukio ya kusikitisha na kukasirisha ya vitendo vya kinyama na kikatili dhidi ya watoto kwa sababu ya watu wazima kushindwa kuzuia hasira zao.
Imani za kishirikina nazo zinachangia ukatili kwa watoto kwa sababu imefikia hatua baba anambaka mtoto wake kutimiza masharti ya mganga wa kinyeji kwamba akifanya ukatili huo atatajirika.
Mtu mzima badala ya kufanya kazi kwa bidii ili kupata utajiri, anatekeleza ushauri wa kijinga wa kumfanyia ukatili mtoto wake wa kumzaa bila aibu!
Katika matukio mengine baba wamezaa na mabinti zao; hii ni fedheha na ukatili mkubwa kwa sababu hata mtoto azaliwaye akikua na kujitambua, atajisikia vibaya na kupata athari za aina mbalimbali kwa sababu ya kitendo cha mtu mzima mmoja hovyo.
Katika matukio mengine katika jamii za kiafrika watoto wametolewa kafara au kufanyiwa vitendo vya kikatili kama sehemu ya matambiko ya kimila yanayodhaniwa kuleta utajiri au kuondoa mikosi.
Ni jukumu la kila mtu mzima kupinga ukatili vitendo vyote vya ukatili dhidi ya watoto. Kuna watu ambao wamekuwa ni mfano bora wa kuiga kwa kutoa taarifa na serikali kuingilia kati kunusuru watoto.
Adhabu kali zinapaswa kutolewa kwa wale wanaopatikana na hatia ya ukatili dhidi ya watoto. Ni muhimu kuwa na utekelezaji madhubuti wa sheria kuhakikisha wale wanawafanyia watoto ukatili wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
Vyombo vya habari rasmi na visivyo rasmi, vinapaswa ‘kupaza’ sauti pale waandishi wake wa habari wanapoona kuna mtoto au watoto wanapitia kwenye ukatili.
Ni muhimu kuimarisha huduma za ushauri nasaha na matibabu kwa watoto waliokumbwa na ukatili kuwasaidia kupona na kurudi katika hali zao za kawaida.
Ushirikiano kati ya serikali, jamii na wadau wengine wa masuala ya watoto, ni muhimu ukaimarishwa kwa kuwekeza rasilimali na utaalamu kupitia kampeni za kuondoa ukatili wa aina zote dhidi ya watoto.
Ni jukumu la wote kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama yanayowawezesha kustawi huku wakifurahia maisha ya kuwa watoto.




