• ePaper
Thursday, April 16, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

KWAHERI WILLIAM LUKUVI

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
March 26, 2026
in Habari, Kitaifa
0
KWAHERI WILLIAM LUKUVI
0
SHARES
7
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na WAANDISHI WETU

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametangaza kifo cha William Lukuvu, ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Ismani mkoani Iringa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Utaratibu).

Taarifa iliyotolewa jana kwa umma na kutiwa saini na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, ilisema Lukuvi alifariki dunia jana, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma, alikokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa mshtuko wa moyo.

“Mheshimiwa Rais anatoa pole kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, familia, wananchi wa Jimbo la Isimani, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huo,” ilisema taarifa hiyo.

DK. EMMANUEL NCHIMBI

Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema Lukuvi atakumbukwa daima, kwani alikuwa kiongozi mchapakazi na mzalendo, aliyetoa mchango mkubwa kwa taifa, jimbo lake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Vijana (UVCCM).

Alisema anaungana na Rais Dk. Samia kuomboleza kifo cha Lukuvi na anatoa salamu za pole kwa Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, wabunge, familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki, na wananchi wote wa Jimbo la Isimani.

DK. MWINYI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema atamkumbuka Lukuvi kwa mchango wake mkubwa, akibainisha kifo chake ni pigo kubwa kwa taifa.

Alisema wamempoteza kiongozi mzoefu, mzalendo na aliyejitolea kwa dhati kutumikia taifa kwa muda mrefu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na kutiwa saini na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu Zanzibar, Raqer Mohamed, ilisema Rais Dk. Mwinyi ametoa salamu za pole kwa Rais Dk. Samia, Spika wa Bunge, Azzan Zungu, familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki, wananchi wa Jimbo la Isimani na Watanzania kufuatia msiba huo.

Ilisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), ipo pamoja na familia ya marehemu na serikali kwa ujumla katika kipindi hiki kigumu cha kuomboleza kifo cha kiongozi huyo.

DK. MWIGULU NCHEMBA

Naye, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema amepokea kwa mshtuko taarifa ya kifo cha Lukuvi, ambapo juzi alizungumza naye.

Dk. Mwigulu alitoa salamu hizo za pole jijini Arusha, jana, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 110 wa Wadau wa Elimu kwa Umma (WASHITIRI).

“Tumepokea taarifa mbaya ya kifo cha mheshimiwa Lukuvi, amefariki leo (jana) asubuhi ghafla, jana (juzi) nimeongea naye, tulipanga tukutane katika mkutano wa wakuu wa mikoa leo na yeye ndiyo alikuwa waziri anayesimamia uratibu, asubuhi sana nimeambiwa anajisikia vibaya, lakini wamempeleka hospitali.

“Baada ya kufika hapa naambiwa hali ilibadilika zaidi na ameaga dunia, hili lipo nje ya uwezo wetu, limetokea niwaombe tusimame kimya dakika moja, tukimuombea ndugu yetu,” alisema Dk. Mwigulu.

Aidha, kupitia ukurasa wake wa instagram, Dk. Mwigulu alitoa pole kwa Rais Dk. Samia, Spika wa Bunge, familia, ndugu, jamaa, wafanyakazi na wananchi wa Ismani kufuatia msiba huo mzito.

“Taifa limepoteza kiongozi mahiri, mzalendo na mtumishi wa umma aliyejitolea kwa dhati katika kuwatumikia wananchi na kulijenga taifa,” aliandika Waziri Mkuu Dk. Mwigulu.

SPIKA WA BUNGE

Spika wa Bunge, Mussa Zungu, alitangaza kuahirisha vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge kutokana na kifo cha Lukuvi.

Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Umma, Ofisi ya Bunge, Dodoma, ilisema shughuli hizo za kamati ziliahirishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 176 ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Agosti, mwaka 2025.

MAWAZIRI WAZUNGUMZA

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, alisema, Lukuvi alikuwa kiongozi mchapakazi na mwenye maono ya kizalendo kwa taifa lake.

Alisema mara nyingi alikuwa anafanya kazi zake kwa kufuata uratibu uliopo ikiwemo sera.

“Tumempoteza kiongozi shujaa, mpenda watu, mzalendo, mtiifu na aliyekuwa anapenda maendeleo ya nchi yake,”alisema Kairuki.  

MOHAMED MCHENGERWA

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, alisema amejifunza mambo mengi kutoka kwa Lukuvi ikiwemo namna alivyoishi karibu na wananchi wake.

JUDITH KAPINGA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema taifa limepoteza kiongozi muhimu aliyependa kazi yake na alikuwa mzalendo katika kuwatumikia wananchi.

“Mezani kwa Lukuvi hakuna jambo lililokuwa linalala, ukimpelekea jambo lako alikuwa analichukua kama lake na kulisukuma hadi mwisho,” alisema Judith.

JUMAA AWESO

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema Lukuvi alikuwa mtu anayependa kujituma bila kushurutishwa ikiwemo kufuata sheria na kanuni katika uongozi wake.

Alisema alipenda kuona matokeo katika kazi anazofanya na kusimamia haki katika nyanja mbalimbali.

“Alipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alitatua kero nyingi za wananchi. Hata bungeni alikuwa akifanya kazi kwa uadilifu mkubwa, tumekuwa tukimwona kama mwalimu na mfano wa kuigwa,” alisema Aweso.

DAVID KIHENZILE

Naye, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa za msiba huo uliotokea ghafla.

Alisema Lukuvi alikuwa kiongozi aliyetoa mchango mkubwa nchini, mwadilifu, mchapakazi na mwalimu wa viongozi vijana wakati wote.

“Amekaa bungeni kwa muda wa miaka 30; hii inadhihirisha wananchi wake walimpenda na kumwamini. Kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa, kwani amehudumu serikalini muda mrefu na kwa weledi,”alisema.

Kihenzile alisema Iringa na taifa limepata pigo kutokana na kifo cha kiongozi huyo aliyekuwa na uzoefu wa miaka mingi serikalini.

WABUNGE WAELEZA

Baadhi ya wabunge kutoka mkoani Iringa, wamesema kifo cha Lukuvi ni pigo kubwa kwa mkoa huo kutokana na mchango wake mkubwa wa maendeleo.

RITTA KABATI

Mwenyekiti wa Wabunge Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati, alisema moja ya jambo kubwa analolikumbuka kutoka kwa Lukuvi ni namna alivyokuwa anapenda umoja na maendeleo kupitia ujenzi wa miradi ya maendeleo.

MZEE KIMITI

Mwanasiasa mkongwe, Paul Kimiti, alisema nchi imepoteza kiongozi imara aliyekuwa akijituma katika kazi za maendeleo ya nchi.

Alisema alimfahamu Lukuvi mwaka 1991 alipokuwa Naibu Waziri wa Kazi na Maendeleo ya Vijana.

Hata hivyo, Kimiti alieleza sababu ya Lukuvi kudumu katika uongozi ilitokana na ujasiri, mvumilivu na uchapa kazi hodari aliokuwa nao katika majukumu yake.

“Ndiyo maana wananchi wake wa Jimbo la Isimani kila uchaguzi walikuwa hawana wa kumchagua dhidi ya Lukuvi kwa sababu alikuwa ni kiongozi anayependa maendeleo,” alisema.

Kimiti alisema uchapakazi na uzalendo wake, vilimvutia Rais Dk. Samia kumchagua katika nafasi za uongozi.

“Rais Dk. Samia na viongozi wengine wa nchi hawakuwahi kumwacha Lukuvi katika nafasi za uongozi kwa sababu ya usikivu na uhodari katika kazi zake,”alisema Kimiti.

Alisema hawezi kumsahau Lukuvi kwa sababu alikua mikononi mwake ambapo wakati wote alionesha shauku ya kujifunza.

MARY CHATANDA

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda, alisema anamfahamu Lukuvi kwa muda mrefu tangu akiwa kiongozi wa UVCCM.

Mary alisema Lukuvi alikuwa ni mbunge mwenye msaada mkubwa kwa wananchi wa Jimbo la Isimani.

Alisema ndani ya bunge alikuwa mwalimu wa wabunge wapya kwa sababu alikuwa anapenda kuwaeleza mengi.

“Mara nyingi wabunge wadogo walikuwa wanapenda kumwita Lukuvi mwalimu au seneta, ameacha pengo katika sekta siasa,”alisema.

GEORGE MKUCHIKA

Mwanasiasa mkongwe nchini, George Mkuchika, aliwapa pole wananchi wa Isimani, wabunge na watanzania kwa kumpoteza mbunge huyo makini.

Mkuchika alimweleza Lukuvi ni mtu aliyejali wananchi wa jimbo hilo.

“Alikuwa anawajali watu wake, kipindi kile ilikuwa haiwezi kupita wiki moja bila ya kwenda jimboni kwake kutatua matatizo ya wananchi wake,” alisema.

CCM IRINGA

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin alisema Chama kimepoteza kiongozi mwadilifu, mzalendo, mchapakazi na mpenda maendeleo.

Alisema watamkumbuka kwa mchango wake mkubwa wa kutumikia taifa na wananchi wa Mkoa wa Iringa kupitia jimbo la Isimani.

“CCM inatambua kazi kubwa ambazo alizifanya kwa uzalendo na kujitolea. Tumepoteza kiongozi mwadilifu sana na mpenda maendeleo katika taifa,” aliongeza Yassin.

MWAKA ALIOZALIWA

Lukuvi alizaliwa Agosti 15, mwaka 1955, Kijiji cha Mapogoro, Wilaya ya Iringa Vijijini, Tanganyika, mkoani Iringa. 

Alisoma Shule ya Msingi Kitanewa kuanzia mwaka 1962 hadi mwaka 1970. Baadaye alipata mafunzo ya awali katika Chuo cha Ualimu Tabora (TTC) na baadaye kuhitimu shahada ya uzamili katika sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

SAFARI YA KISIASA

Lukuvi alianza safari ya kisiasa kwa kuchaguliwa Mbunge wa Jimbo la Isimani mwaka 1995 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), nafasi ambayo aliishika hadi kifo chake.

Aidha, alihudumu katika nafasi ya naibu waziri na waziri katika nyadhifa mbalimbali.

Januari 2015 hadi Januari 2022 alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Novemba 2010 hadi Januari 2015.

Pia, Juni mwaka 2023, Rais Dk. Samia alimteua kuwa Mshauri wa Rais katika Uhusiano wa Kisiasa na Kijamii, ambapo hadi kifo chake alikuwa Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge).

Vilevile, Lukuvi aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mjumbe wa Kamati ya Maadili ya Kamati Kuu CCM, mkuu wa wilaya na baadaye mkuu wa mikoa mbalimbali.

DONDOO ZAIDI

1975-1980 – Mwalimu

1980-1994- Uongozi Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)

1994-1995- Mkuu wa Wilaya Bukoba

1995- Bungeni

1995- 2000 – Naibu Waziri wa Vijana na Kazi

2000-2005 – Waziri wa Nchim Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu)

2006-2010 – Mkuu wa Mkoaw a Dodoma, Dar es Salaam

2010-2015- Waziri

2015-2022- Waziri wa Ardha, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

2023 – Mshauri wa Rais

2024-2026- Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Previous Post

STEVE NYERERE, WEMA SEPETU WAMLILIA LUKUVI

Next Post

DK. NCHIMBI ATOA KAULI UBORESHAJI WA MITAALA

Next Post
DK. NCHIMBI ATOA KAULI UBORESHAJI WA MITAALA

DK. NCHIMBI ATOA KAULI UBORESHAJI WA MITAALA

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

MUOSHA MAGARI AAMRIWA KUFANYA USAFI MAHAKAMANI

MUOSHA MAGARI AAMRIWA KUFANYA USAFI MAHAKAMANI

22 hours ago
TRILIONI 1.7/- ZANUFAISHA MIRADI MKOANI SINGIDA

TRILIONI 1.7/- ZANUFAISHA MIRADI MKOANI SINGIDA

7 months ago

Popular News

  • PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SERIKALI YAFUTA LESENI 40 ZA UTAFITI  WA MADINI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TIMU OFISI YA MAKAMU WA RAIS, WIZARA YA MAJI KUCHUANA MEI MOSI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SIMBA, FOUNTAIN GATE SIKU YA HESHIMA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. MWINYI AKAGUA MJI WA AFCON FUMBA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?