Na MWANDISHI WETU
KUFUATIA kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Mbunge wa Jimbo la Isimani, William Lukuvi baadhi wasanii wamesema taifa limepoteza kiongozi muhimu na mchango wake hautoweza kusahaulika.
Lukuvi alifariki dunia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu.
Wakizungumza kupitia mtandao wa instagram, Mwenyekiti wa Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere aliandika kuwa Lukuvi alikuwa kiongozi bora na imara daima atakumbukwa na wengi.
“Mchango wako ni mkubwa kwa taifa utabaki kama kumbukumbu katika taifa letu na kizazi kijacho kitasoma historia yako, umekuwa kaka katika kila kona kwa vijana na watu wazima.
“Hatuwezi kuamini lakini kwa mapenzi ya Mungu tunapaswa kumshukuru kwa kila jambo, pumzika mwamba lala salama mwendo umeumaliza nasi tutakukumbuka daima Wiliam,” alisema.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa Watanzania na wana Iringa daima wataendelea kumbuka kutokana na mambo mazuri aliyoyafanya ndani ya taifa hili.
Nyota wa filamu za bongo, Wema Sepetu aliandika kuwa moyo wake umeumia sana baada ya kupokea taarifa ya kifo cha Lukuvi.
“Moyo wangu umeumia sana ulikuwa zaidi ya baba, pumzika kwa amani baba Lukuvi daah,” alieleza kupitia mtandao Wema Sepetu.




