Na AMINA KASHEBA
USAJILI mpya wa Yanga umeanza kulipa, fuatia jana timu hiyo kupata ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa ya Kigoma katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mtanange huo uliopigwa Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, Yanga ilitawala mechi hiyo huku nyota wake wapya Mohamed Damaro, Allan Okello na Laurindo Aurelio ‘Depu’ waliotua dirisha dogo, wakiwasha moto wa hali ya juu.
Katika mtanange huo, Depu alifunga bao moja na kutoa pasi moja ya bao, Damaro akipachika bao moja wakati Okello akitoa pasi moja ya bao.
Mabao mengine ya Yanga yalifungwa na Duke Abuya, Pacome Zouzoua, Prince Dube na Mudathir Yahya, kila mmoja akiweka kimiani bao moja.
Kutokana na ushindi huo, sasa Yanga ipo kileleni mwa msimamo wa ligi, ikiwa na alama 19 katika mechi saba.
Baada ya mtanange huo, sasa Yanga inajipanga kwa mechi mbili mfululizo za kundi B Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Yanga itachuana na Al Ahly mwishoni mwa wiki nchini Misri kabla ya kurudiana mwishoni mwa mwezi huu katika Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.
Yanga: Abuutwalib Mshery, Bakari Mwanyeto, Dickson Job, Maxi Nzengeli/Mudathir Yahya, Pacome Zouzou/Laurindo Dilson, Kibwana Shomary, Allan Okello, Chadrack Boka/ Balla Conte, Mohamed Damaro/ Mohamed Hussein, Prince Dube na Duke Abuya/Kouassi Yao.
Mashujaa: Erick Johola, Mpoki Mwakinyuke, Samwel Onditi, Abdulanasir Assa, Salum Kihimbwa, Hassan Ali, Mundhir Vuai, Jafari Kibaya, Yusuf Dunia, Mohamed Salum na Samson Madeleke.




