• ePaper
Friday, May 8, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

KIBANO WALIOHARIBU SARUJI MIFUKO 1,262

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
February 14, 2026
in Habari, Kitaifa
0
KIBANO WALIOHARIBU SARUJI MIFUKO 1,262
0
SHARES
14
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

ELIZABETH JOHN Na MASHAKA MHANDO, Handeni 

WAZIRI Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kuwachukulia hatua watumishi wa wizara hiyo, waliosimamia ujenzi wa Chuo cha VETA wilayani Handeni na kusababisha kuganda kwa mifuko ya saruji 1,262.

Pia, amemwagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, kufanya uchunguzi wa matumizi mabaya ya fedha katika jengo la Kituo cha Afya Sindeni, ambapo milango 34 imebainika kuwa chini ya kiwango.

Dk. Mwigulu, alitoa onyo hilo jana alipozungumza na wakazi wa Handeni, baada ya kukagua na kufungua jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Handeni, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga.

Alimwagiza Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Batilda Buriani, kufuatilia miradi hiyo kwa karibu, akisisitiza kuwa, Wilaya ya Handeni, miradi mingi imekuwa na kasoro. 

“Kamanda wa TAKUKURU, wote waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria, Mkuu wa Mkoa, Balozi Dk. Batilda Buriani, ufuatilie wahusika wote kama wameweka milango hiyo kusudi kuiba fedha za serikali, wachukuliwe hatua. Mradi ule ni wa zaidi ya milioni 300,” alisema.

Alisisitiza kuwa, watumishi waliosimamia ujenzi wa maabara ya Chuo cha VETA na kusababisha mifuko ya saruji kuganda, wanapaswa kurudisha fedha hizo na kama walifanya uzembe, wachukuliwe hatua.

“Waliotumwa kujenga VETA ili vijana wasome, wamekaa ofisini wakagandisha mifuko 1,262. Huu ni uzembe, hatuwezi kuvumilia. 

“Nimemwagiza katibu mkuu wa wizara ya elimu, awachukulie hatua na wakatwe fedha katika mishahara yao kurejesha ili jengo lijengwe,” alisema.

Pia, Waziri Mkuu Nchemba alitoa onyo kwa watumishi wa serikali akiwataka waache kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wazingatie uadilifu.

AONYA KUBAGUANA

Katika hatua nyingine, Dk. Nchemba, aliwataka Watanzania kutoruhusu ufa wa kubaguana kwa sababu ya kazi au shughuli wanazozifanya, akisisitiza kwamba, tabia kama hiyo inaweza kuhatarisha amani na maendeleo ya nchi.

“Tusiingize ufa wa kubaguana kwa kazi zetu, hiyo siyo nchi yetu tuliyoachiwa. Mkulima asimbague mfugaji wala mfugaji asimbague mkulima. Tusiruhusu ufa wa kubagua kufanya hivyo, kutaharibu nchi yetu,” alisema. 

Alisisitiza kuwa, ongezeko la idadi ya watu na mifugo, linahitaji kupanga matumizi bora ya ardhi. 

“Wakulima ni Watanzania, wafugaji ni Watanzania. Mtu anaruhusiwa kwenda kuishi popote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mradi havunji sheria. 

“Tunaruhusiwa kwenda kuishi popote, lakini tuepuke migogoro inayoweza kujitokeza,” alisema.

Dk. Nchemba, alikumbusha kuwa kosa la mtu mmoja halipaswi kuwakilisha kijiji au kikundi chote. 

“Tusinyooshe kidole kwa mfugaji au mkulima. Ni sehemu chache sana, unaweza kukuta kuna wakulima tu na wafugaji tu,” alieleza.

 Alisisitiza kuwa, tabia ya kiburi, kuingiza mifugo kwenye mashamba ya watu, wengine haiendani na asili ya Tanzania na serikali haitaivumilia.

UZINDUZI MRADI WA UMEME

Awali, Waziri Mkuu, alikagua ujenzi wa kituo cha kupoza umeme unaofanyika eneo la Mkata, wilayani Handeni na kuweka jiwe la msingi la kituo hicho na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Mkata kwenda Kilindi. 

Pia, alizindua ujenzi wa njia za kusambaza umeme wa msongo wa kilovoti 33 zenye urefu wa kilometa 45 kutoka kituo cha Mkata kwenda Kwamsisi.

Akiwa hapo, Waziri Mkuu, alimwagiza Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, kuhakikisha malipo ya wakandarasi wa mradi huo zaidi ya sh. bilioni moja, yanafuatiliwa mradi ukamilike kwa wakati.

Alisema serikali ipo kazini kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ahadi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa, maeneo yenye changamoto, yataamuliwa na hatua stahiki kuchukuliwa. 

Alisema serikali inaendesha mradi mkubwa wa zaidi ya sh. trilioni moja nchi nzima, kwa lengo la kuimarisha upatikanaji umeme wa uhakika kwa ajili ya viwanda vilivyopo na vipya vitakavyoanzishwa. 

Pia, Dk. Mwigulu alitoa onyo kwa wakandarasi wanaopeleka fedha za miradi katika matumizi mengine badala ya kutekeleza kazi husika, serikali haitavumilia hali hiyo na itahakikisha fedha zinazotolewa zinalingana na kazi iliyofanyika.

“Fedha ya mradi iende kwenye mradi. Hatuna mzaha kwenye hili, nina taarifa kamili ya miradi zaidi ya 100 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 13 mkoani Tanga,” alisema.

Alieleza kuwa, ndani ya siku 100, serikali imeanza kushughulikia upungufu wa watumishi katika sekta ya afya na elimu, walimu 7,000 na watumishi wa afya 5,000 waliajiriwa, wakiwemo waliopangiwa kufanya kazi mkoani humo.

Aidha, mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, umeanza kwa makundi maalumu, wakiwemo watoto, wajawazito na wazee wasiojiweza, huku utekelezaji wake ukiendelea hatua kwa hatua.

Alisisitiza umuhimu wa viongozi na wananchi, kuendeleza amani, akibainisha kuwa, mipango yote ya maendeleo, haiwezi kutekelezwa pasipo amani.

Pia, alizindua jengo la ICU katika Hospitali ya Hamashauri ya Handeni lililojengwa kwa gharama ya sh. milioni 426 na kusema litapunguza adha kwa wakazi wa wilaya hiyo waliokuwa wakisafiri kilometa 160 hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga kupata huduma.

MKURUGENZI WA TANESCO

Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Tanznaia (TANESCO), Lazaro Twange, alisema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya Gridi Imara, yenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Wilaya za Handeni na Kilindi na migodi ya graphite ya Kwamsisi. 

“Mradi huu uliogharimu sh. bilioni 44.14 na ujenzi wa njia ya kusambaza umeme ni sh. bilioni 5.75. Unahusisha ujenzi wa vituo viwili vya kusambaza umeme pamoja na ufungaji wa transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 60 kila moja, ambazo zitapooza umeme kutoka kilovolti 132 hadi kilovolti 33 kwa ajili ya matumizi ya wananchi,” alisema.

Alisema kukamilika kwa miradi hiyo kutaleta manufaa makubwa ikiwemo kuondoa kabisa changamoto ya umeme katika maeneo husika, kuongeza mapato ya TANESCO na halmashauri kupitia tozo na kodi za huduma, pamoja na kutoa ajira kwa wananchi.

WAZIRI WA NISHATI

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alisema kabla ya mradi huo, umeme unaopatikana wilayani Handeni na Kilindi unatokea Tanga mjini, lakini mradi huo utakapokamilika Novemba mwaka huu, umeme utatokea Chalinze, utaenda kupoozwa Mkata, na hatimaye kuwafikia wananchi wa Handeni na Kilindi kwa uhakika zaidi.

Alisema kupitia miundombinu hiyo mipya, umeme utasafirishwa kutoka Mkata kwenda Msisi kwa umbali wa zaidi ya kilomita 45, hatua itakayoongeza uwezo wa usambazaji na kuimarisha huduma katika maeneo hayo.

Ndejembi alisema uwepo wa kituo hicho utaboreshesha hali ya upatikanaji umeme na kurahisisha shughuli mbalimbali wilayani humo ukiwemo uchimbaji wa madini, viwanda, kilimo na biashara, jambo litakalochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wa Handeni na Kilindi.

Alisema tayari ameielekeza TANESCO kuanza mara moja kubadilisha nguzo za miti na kuweka za zege katika njia ya umeme kutoka Tanga kuelekea Msisi kama hatua ya mpito. 

Aidha, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, alisema serikali ya Awamu ya Sita imetoa sh. bilioni 171 za ujenzi wa mradi mkubwa wa maji, huku mradi mbadala wa HTM ukiwa umemefikia asilimia 70 na mradi mwingine wa Segera hadi Kabuku umefikia asilimia 60 kwa gharama ya sh. bilioni 25.

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alieleza kuwa, serikali imetoa sh. bilioni 2.5 kujenga kituo cha uchakataji mkonge kilichopo Handeni, kitakachoongeza tija katika zao la mkonge.

Previous Post

SIKU 100 ZA KAZI NA UTU, ZAIKOSHA CCM

Next Post

WENYE UMRI HUU HATARINI KUPATA PRESHA YA MACHO

Next Post
WENYE UMRI HUU HATARINI KUPATA PRESHA YA MACHO

WENYE UMRI HUU HATARINI KUPATA PRESHA YA MACHO

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

AZAM, YANGA MECHI YA KISASI, HESHIMA

AZAM, YANGA MECHI YA KISASI, HESHIMA

2 months ago
SALOME AIBANA KAMPUNI YA DONGFANG KWA KASI ISIYORIDHISHA MRADI WA UMEME MALAGARASI

SALOME AIBANA KAMPUNI YA DONGFANG KWA KASI ISIYORIDHISHA MRADI WA UMEME MALAGARASI

2 months ago

Popular News

  • YANGA MBELE KWA MBELE

    YANGA MBELE KWA MBELE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • WATAALAMU WAFUNGUKA MITAZAMO YA MIKATABA 8

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. SAMIA AKEMEA VIONGOZI ‘KUVIMBA’

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DEMOKRASIA ISIZICHAFUE NCHI ZETU – RAIS DK. SAMIA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • ZIARA YA RAIS KAGAME, RUTO KUIMARISHA DIPLOMASIA KIUCHUMI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?