Na Mwandishi Maalumu, Ethiopia
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameshiriki katika mkutano wa ngazi ya juu na vyombo vya habari uliolenga kujadili ufadhili endelevu wa mapambano dhidi ya Malaria barani Afrika, akisema vita dhidi ya ugonjwa huo si suala la afya pekee, bali ni ajenda ya maendeleo, uchumi na ustawi wa rasilimali watu barani Afrika.
Pia, Rais ametumia jukwaa la mkutano huo wa pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU), unaofanyika katika Makao Makuu ya Umoja huo, jijini Addis Ababa, Ethiopia, kueleza namna Tanzania inavyopambana na Malaria.
Mkutano huo ulioandaliwa na Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Umoja wa Viongozi wa Afrika katika Mapambano dhidi ya Malaria (ALMA), ulilenga kujadili namna ya kuimarisha ufadhili wa ndani wa programu za Malaria, kupunguza utegemezi wa misaada ya nje na kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika.
UONGOZI THABITI
Akizungumza jana katika mkutano huo, Rais Dk. Samia alisema mapambano dhidi ya Malaria barani Afrika yanahitaji uongozi na usimamizi thabiti wa Waafrika wenyewe, umiliki wa kweli wa programu zake na dhamira ya kisiasa ya muda mrefu.
Rais Samia alieleza kuwa, vita dhidi ya Malaria si suala la afya pekee, bali ni ajenda ya maendeleo, uchumi na ustawi wa rasilimali watu barani Afrika.
UZOEFU WA TANZANIA
Akieleza uzoefu wa nchi katika mapambano dhidi ya Malaria, Rais Dk. Samia alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika ajenda ya kutokomeza ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na kuwa mwenyeji wa ALMA kama taasisi ya kuratibu mapambano hayo barani Afrika, iliyojengwa juu ya mifumo madhubuti ya uwajibikaji na uwezo wa utekelezaji unaolenga matokeo.
Rais Dk. Samia alisema Tanzania imewekeza kwa kiasi kikubwa katika utafiti wa kisayansi na ubunifu kupitia Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), ikiwemo utafiti wa teknolojia za kisasa za kudhibiti maambukizi ya Malaria.
Alibainisha jitihada za Tanzania za kuongeza matumizi ya vyandarua vya kujikinga dhidi ya mbu waenezao Malaria, chanjo, kuboresha mifumo ya matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa.
Kwa mujibu wa Rais, Serikali imeimarisha ushirikiano wa sekta mbalimbali kuhakikisha afua za Malaria zinaunganishwa kikamilifu katika mfumo wa huduma za afya ya msingi na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.
Katika kuimarisha ufadhili wa ndani, Rais Dk. Samia alisema kupitia Mabaraza ya Kutokomeza Malaria ya Tanzania Bara na Zanzibar, Serikali imeendelea kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za dini, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo katika uhamasishaji wa rasilimali za ndani kwa mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Pia, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa na kuwa, pamoja na jitihada za ndani, taasisi za kimataifa na washirika wa maendeleo wanapaswa kutekeleza ahadi zao kikamilifu na kwa wakati, hususan katika kuimarisha Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Malaria (The Global Fund) na matumizi ya rasilimali za Benki ya Dunia ya Programu za Malaria.
Alisema jitihada za kutokomeza Malaria zinahitaji mshikamano wa pamoja wa nchi wanachama, ufadhili endelevu na matumizi ya takwimu sahihi katika kufanya uamuzi na ubunifu unaozingatia mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.
RAIS BOKO
Rais wa Jamhuri ya Botswana na Mwenyekiti wa ALMA, Duma Boko, alidokeza kwa mujibu wa Ripoti ya Maendeleo ya Malaria Barani Afrika ya Mwaka 2025, bara hilo bado ipo mbali kufikia lengo la kutokomeza Malaria ifikapo mwaka 2030.
Rais Boko alihimiza nchi wanachama kutenga bajeti mahsusi ya mapambano dhidi ya Malaria, kuanzisha Mabaraza ya Kutokomeza Malaria na kutumia mifumo ya takwimu kuboresha utekelezaji.
Kamishna wa Afya, Masuala ya Binadamu na Maendeleo ya Jamii wa Umoja wa Afrika, Balozi Amma Twum-Amoah, alisema kupungua kwa ufadhili wa kimataifa katika miaka ya karibuni kumeathiri juhudi za nchi mbalimbali za kupambana na Malaria.
Alisisitiza umuhimu wa kuwa na mabadiliko ya mtazamo katika ufadhili, uhimilivu wa mifumo ya afya dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, ushiriki mkubwa wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika mapambano dhidi ya Malaria.
MKUTANO
African Leaders Malaria Alliance(ALMA) ni Muungano wa Wakuu wa Nchi wa Afrika, unaolenga kuharakisha kutokomeza Malaria na kuimarisha mifumo ya afya.
Mkutano huu wa ngazi ya juu ulifanyika pembezoni mwa shughuli za Umoja wa Afrika ukileta pamoja Wakuu wa Nchi, Mawaziri wa Afya nawadau wa maendeleo.
Mkutano ulijadili Ripoti ya Maendeleo ya Malaria Afrika 2025 inayoonyesha kuwa, Afrika bado inabeba zaidi ya asilimia 90 ya maambukizi na vifo vya malaria duniani huku kasi ya kutokomeza ikipungua.
Wito wa kuweka msukumo mkubwa wa kutokomeza Malaria unalenga kufikia lengo la 2030 kupitia umiliki wa nchi, uwajibikaji na uongozi wa pamoja.




