Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametaja faida za Mpango wa Nishati wa Tanzania, akisema utaongeza upatikanaji wa nishati safi na kuimarisha mageuzi ya kiuchumi.
Aidha, amebainisha mpango wa taifa wa kuwekeza katika vyanzo vya nishati jadidifu, ikiwemo ya jua, upepo, jotoardhi, umeme wa maji endelevu na kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Rais Dk. Samia alieleza hayo, jijini Addis Ababa, Ethiopia, aliposhiriki Mkutano wa Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika wanaosimamia Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSCC), pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa Umoja wa Afrika.
MABADILIKO YA TABIANCHI
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Dk. Samia alieleza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta muhimu za uchumi na zinazozalisha ajira, ikiwemo ya kilimo, nishati, uvuvi, utalii na miundombinu.
Dk. Samia alisema hali ya hewa isiyotabirika inaendelea kudhoofisha mifumo ya maisha na uzalishaji barani Afrika.
Rais Samia alisema, ndiyo maana Tanzania inatekeleza mkakati huo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, unaolenga kupanua upatikanaji wa nishati safi na kuimarisha mageuzi ya kiuchumi.
Alibainisha mpango huo wa taifa wa kuwekeza katika vyanzo vya nishati jadidifu, ikiwemo jua, upepo, jotoardhi, umeme wa maji endelevu na kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia una tija kubwa katika kukabili mabadiliko hayo ya tabianchi.
Vilevile, Rais Dk. Samia alitaja ajenda ya nishati safi ya kupikia kuwa, kipaumbele cha taifa kinacholingana na mwelekeo wa Afrika katika mabadiliko ya sekta ya nishati.
USHIRIKIANO WA KIKANDA
Kwa mujibu wa Rais Samia, kupitia miundombinu ya pamoja ya kikanda, Tanzania inaendelea kuchangia usalama wa nishati na mshikamano wa kiuchumi barani Afrika, hatua inayoongeza uwezo wa nchi kukidhi mahitaji ya uzalishaji, huduma za kijamii na ukuaji wa viwanda.
Rais Dk. Samia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utabiri na usimamizi wa majanga kwa kushirikiana na taasisi za kikanda, kwa lengo la kuchukua tahadhari za mapema.
“Taarifa za hali ya hewa kwa wakati huokoa maisha na kupunguza gharama za kukabiliana na majanga,”alisema Rais.
CHANGAMOTO
Hata hivyo, alibainisha tatizo la mifumo hiyo kukabiliwa na changamoto za upungufu wa rasilimali, hivyo kuhitaji kupewa kipaumbele katika ushirikiano wa kimataifa.
Rais aliongeza kuwa, mfumo wa kimataifa wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unategemea utekelezaji wa ahadi za kifedha kwa wakati na kwa ufanisi.
Alitaja utaratibu mgumu, gharama kubwa za utekelezaji na utegemezi mkubwa wa mikopo ni kikwazo endelevu kwa nchi zenye uwezo mdogo wa kifedha, huku akisisitiza umuhimu wa ruzuku na masharti nafuu ya fedha katika kulinda mafanikio ya maendeleo.
“Kwa Tanzania na nchi nyingi za Afrika, ufadhili wa ruzuku kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na fedha za masharti nafuu ni muhimu katika kulinda mafanikio ya maendeleo, huku zikikabiliana na hatari za mabadiliko ya tabianchi,”alisisitiza.
MALENGO YA DUNIA
Halikadhalika, alisema Tanzania inaunga mkono Malengo ya Dunia ya Kuhimili Athari za Mabadiliko ya Tabianchi na inaendelea kushirikiana kwa karibu na Kituo cha Afrika cha Matumizi ya Takwimu na Taarifa za Hali ya Hewa kwa Maendeleo (ACMAD) na taasisi za kikanda, kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema.
Alitumia kikao hicho kusisitiza kuwa, mifumo hiyo inahitaji kuimarishwa zaidi kifedha na kutambuliwa kama rasilimali ya pamoja ya kimataifa.
Pia, Rais Dk. Samia aliunga mkono juhudi za kuanzisha viwango vya pamoja vya Afrika katika masoko ya kaboni, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu kuhakikisha biashara hiyo inaleta manufaa halisi kwa jamii, taifa na kulinda mazingira.
Rais Samia alibainisha hatua zinazochukuliwa na Tanzania kuongeza thamani ya rasilimali, madini ya kijani, utalii endelevu, na miundombinu inayostahimili mabadiliko ya tabianchi, kama sehemu ya kujenga uchumi jumuishi na unaozalisha ajira.
Dk. Samia alisema Tanzania ipo tayari kushirikiana kwa karibu na nchi nyingine za Afrika, katika maandalizi ya mikutano ijayo ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, kuhakikisha vipaumbele vya bara hilo vinapata msukumo wa kisera na kiutendaji.
Alisema kuwa mafanikio ya pamoja yatategemea uratibu madhubuti kati ya serikali, taasisi za kikanda na taasisi za bara.




