Na ATHNATH MKIRAMWENI, Urambo
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amesema serikali itaendelea kupeleka maendeleo kwa wananchi wote.
Kihongosi alitoa kauli hiyo alipozungumza na wananchi na wafanyabiashara wa Soko la Ndizi, walioeleza wasiwasi wao kuhusu uamuzi wa kuhamishwa katika eneo la biashara.
Kihongosi alisema mabadiliko ya maendeleo huambatana na faida na changamoto, lakini lengo kuu la serikali ni kustawisha maisha ya wananchi.
Alisema katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, zikiwemo barabara za lami na Reli ya Kisasa (SGR), wakati mwingine wananchi hulazimika kupisha miradi hiyo kwa manufaa ya taifa.
Kuhusu soko jingine kutozinduliwa na Mwenge wa Uhuru, Kihongosi alisema kitendo hicho hakiufanyi mradi kuwa batili, bali huashiria uwepo wa dosari zinazohitaji kurekebishwa.
Kihongosi alimwagiza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, kushirikiana na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Said Nkumba, kukutana na wafanyabiashara na viongozi wa wilaya kusikiliza hoja zao na kufikia mwafaka.
Alisema haitakuwa busara kutoa uamuzi wa upande mmoja bila mazungumzo ya kina, kwa kuwa utamaduni wa CCM ni kusikiliza wananchi na kushughulikia changamoto zao.
Vilevile, wafanyabiashara wa Soko la Ndizi walieleza wamepokea notisi ya kuhama ifikapo Machi 30, mwaka huu hatua iliyozua hofu ya kupoteza mitaji yao endapo eneo jipya halitakuwa na wateja wa kutosha.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuchagua viongozi wa kusimamia maslahi yao kwa mujibu wa sheria na taratibu.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Nkumba, aliwahakikishia wafanyabiashara na wananchi Chama na serikali vimejipanga kutekeleza maelekezo yaliyotolewa kulinda maslahi ya pande zote.
Kihongosi alisema CCM inaendelea kusimamia ustawi wa wananchi kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli zao katika mazingira ya amani na utulivu.




