Na MWANDISHI WETU
MAKAMU wa Rais Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema Mashujaa wa Vita ya Majimaji wanapaswa kuenziwa kwa kuimarisha nidhamu katika utendaji kazi, kupinga ukabila na kutambua wajibu wa kila Mtanzania katika kulitetea na kulijenga Taifa.
Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa kilele cha Tamasha la 17 la Kumbukizi ya Miaka 120 ya Mashujaa wa Vita ya Majimaji, lililofanyika katika Viwanja vya Makumbusho ya Vita ya Majimaji, Songea, mkoani Ruvuma.
Amesema ni muhimu kuenzi mchango wa mashujaa hao kwa kuendelea kusimamia umoja wa kitaifa, kuhakikisha makabila yote yanaishi kama Taifa moja, kufanya kazi kwa bidii katika kuijenga nchi, pamoja na kupinga vitendo vya rushwa na kusimamia haki.
Ameongeza kuwa mashujaa wa Vita ya Majimaji waliweka pembeni ubinafsi kwa kuunganisha zaidi ya makabila 30 kupambana na wakoloni, jambo lililoweka msingi wa mustakabali bora wa Taifa la leo.
Makamu wa Rais amesema kumbukizi za Vita ya Majimaji ni nyenzo muhimu kwa kizazi cha sasa na kijacho kujifunza uzalendo, ujasiri na kujitolea, kwani mashujaa hao walitoa maisha yao kulinda heshima, utu na rasilimali za Taifa.
Aidha, ametoa wito kwa jamii kushirikiana na Shirika la Makumbusho ya Taifa kuanzisha makumbusho katika maeneo yao kwa lengo la kuhifadhi historia ya Taifa na kutumia fursa zilizopo katika malikale kukuza uchumi kupitia utalii wa utamaduni.
Amesema maboresho yaliyofanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii katika Sheria ya Malikale, Sura ya 333 na Sheria ya Makumbusho ya Taifa, Sura ya 281, yamefungua fursa kwa jamii na taasisi binafsi kuanzisha makumbusho.
Vilevile, Makamu wa Rais amezihimiza taasisi binafsi na jamii kwa ujumla kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwekeza katika kumbukumbu na malikale zilizopo nchini, kama chanzo cha ajira, pamoja na majukwaa ya kutangaza bidhaa, vivutio vya uwekezaji na utalii.




