Na WAANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, kutokana na vifo vya watumishi wa afya saba waliofariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama Ziwa Tanganyika.
Vifo hivyo vilitokea Machi 14, 2026 asubuhi wakati watumishi hao wakienda kuhudumia wananchi wa Kata ya Kagunga Kijiji cha Kagunga.
Rais Dk. Samia alitoa salamu hizo jana kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X zamani Twitter.
“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya ndugu zetu saba, watumishi wa afya mkoani Kigoma, waliofariki baada ya boti yao kuzama katika Ziwa Tanganyika leo (jana) asubuhi wakati wakielekea kutimiza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi kwenye Kata ya Kagunga Kijiji cha Kagunga,” alieleza.
Aidha, Rais Dk. Samia aliwataka Watanzania kuungana kuwaombea kwa Mungu marehemu hao wapumzike kwa amani na awape uponyaji majeruhi wanaoendelea kupata matibabu.
“Ninatoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mheshimiwa Simon Sirro, familia za wafiwa, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu,” alisema.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa alisema amepokea kwa masikitiko taarifa za vifo vya watumishi hao, huku akitoa pole kwa watumishi wote wa afya nchini.
Alisema watumishi wa afya wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kujitolea katika kuokoa maisha ya wananchi, wakati mwingine wakifika katika maeneo yasiyofika kirahisi.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Sirro, alitoa pole kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Kigoma na familia za waliopatwa na tukio hilo na kueleza serikali ipo tayari kutoa msaada utakaohitajika.
KAMANDA ZIMAMOTO
Aidha, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa Kigoma, Michael Maganga alisema ajali hiyo ilitokea saa mbili asubuhi, jana katika Kijiji cha Kalalangabo, Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Alisema waliothibitika kupoteza maisha miili yao imepatikana, japokuwa wengine watatu waliokuwa katika boti hiyo hawakuwa wamepatikana.
“Watu wengine tisa waliokuwa kwenye boti hiyo waliokolewa na wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kigoma, Maweni, juhudi za kutafuta miili ya watu watatu zinaendelea,” alisema.
Kamanda huyo alisema upepo mkali ulioanza asubuhi na kusababisha mawimbi makubwa ndiyo chanzo cha ajali hiyo.
MVUA YAUA WATU TISA SINGIDA
Wakati huo huo, watu tisa wakiwemo watoto saba wamefariki dunia mkoani Singida kufuatia mvua inayoendelea kunyesha nchini.
Athari nyingine ambazo zimejitokeza mkoani humo ni kuharibika miundombinu ya barabara na kubomoka madaraja mawili.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa Singida, Halima Dendego alipozungumza na gazeti hili wakati akieleza hali ya mvua inayoendelea kunyesha mkoani humo.
“Tumepata vifo vya watoto saba na watu wazima wawili, tunamuomba Mungu awapumzishe watu wetu, tunaendelea kuchukua tahadhari kadri ya siku hadi siku.
“Athari nyingine tulizopata ni barabara nyingi zimeharibika na madaraja mawili yamepata hitilafu kubwa kwa ujumla na miundombinu imeharibika,” alisema.
Aidha, alisema serikali ya mkoa huo inaendelea kurabati miundombinu hiyo iliyoharibika kwa dharura na kuhakikisha inarudi katika hali yake ya awali.
Pia, alisema mkoa huo hupata mvua kuanzia Oktoba hadi Februari kila mwaka kwa wastani wa milimita 800, ambapo msimu huu mvua ilianza kunyesha Novemba mwishoni na kuendelea hadi Machi.
Akizungumzia hali ya mvua, Dendego alisema imepita kiwango kinachotarajiwa na kusababisha mafuriko katika baadhi ya maeneo.
Hivi karibuni Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), iliwataka wananchi kuchukua tahadhari kufuatia mvua inayoendelea kunyesha nchini kutokana kuunganika na mvua za masika na vuli.
IMEANDIKWA NA ZIANA BAKARI (DAR) NA FADHILI ABDALLAH (KIGOMA).




