Na MICHAEL KATONA, Iringa
SERIKALI imetumia sh. bilioni 64 kuboresha miundombinu ya Uwanja wa Ndege wa Iringa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza utalii na kuimarisha uchumi wa mkoa huo.
Akizungumza katika kongamano la wadau wa habari Kusini mwa Tanzania (MISA TAN SUMMIT), Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James alisema serikali inalenga kuboresha huduma za usafiri wa anga ili kurahisisha upatikanaji wa safari kwa watalii, wasafiri wa ndani na nje ya nchi.
Alisema sehemu ya fedha hizo imetumika kujenga jengo jipya la abiria na eneo la maegesho ya magari kwa gharama ya takribani sh. bilioni 41.06, ambapo jengo hilo linatarajiwa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja.
“Serikali inaendelea kuhakikisha miundombinu ya uwanja wa ndege inaboreshwa ili kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii katika Nyanda za Juu Kusini,” alisema James.
Aidha, James, alisema kufanyika kongamano mkoani humo, kutasaidia kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu shughuli za maendeleo na kutangaza fursa zilizopo Iringa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, aliomba serikali ya mkoa kutenga eneo kwa ujenzi wa kituo cha mawasiliano kitakachosaidia kuboresha upatikanaji wa taarifa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, aliwataka wanahabari kutumia majukwaa yao kuelimisha vijana kuhusu matumizi sahihi ya fursa za kiuchumi ili kupunguza umaskini.




