Na EMMANUEL MOHAMED
WADAU wa masuala ya saikolojia na haki za binadamu wametaja sababu zinazochangia matukio ya ukatilii nchini, ikiwemo afya ya akili na usaliti katika uhusiano.
Sababu zingine ambazo zinachangia matukio hayo ya kikatili ni msongo wa mawazo na historia za familia.
Akizungumza na UHURU, Mwenyekiti wa Kamati Endelevu ya Taaluma kutoka Chama Cha Wanasaikolojia Tanzania (TAPA), Jesusa Malewo, alisema ukatili kwa lugha nyepesi ni mtu kuelezea maumivu kwa njia isiyofaa.
“Maumivu hayo yanatokana na hali mbalimbali za kimaisha, kwa mfano, historia ya familia inaweza kumsababishia mtu kuwa mkatili. Mtu amekuwa akiona wazazi wake wakipigana, ni rahisi kufanya ukatili kwa mtu mwingine kutokana na kuwa amekuwa kwa kuviona vitendo vya kikatili,
“Kwa hiyo hali hii imekaa katika akili yake, hivyo ni rahisi kumfanyia mtu mwingine ukatili, kikubwa ni yale maumivu ambayo anayapitia wakati huo,”amesema.
Malewo alitaja sababu nyingine ni changamoto za kimaisha, ambazo hufanya baadhi ya watu kuwa na msongo wa mawazo.
“Kwa hiyo, kuwa na msongo wa mawazo inaweza kuwa ni kisababishi cha mtu kufanya ukatilii kutokana na kuwa kuna mambo mengi yanamsonga, kuna mambo yanampa wasiwasi, kuna mambo mengi hayajakaa vizuri kwenye maisha yake, kwa hiyo hata namna ya kuyatatua bado hajui atumie stadi zipi,”amesema.
Alisema kwa upande mwingine, sababu nyingine ya kuongezeka kwa matukio hayo ni usaliti katika uhusiano ambao wahusika wanashindwa kuelezeana ukweli wa mambo ambayo hayajitoshelezi katika uhusiano wao.
“Kwa mfano, kwa hawa waliopo katika uhusiano unakuta mtu alitendwa, yale maumivu ya hisia anahama nayo kwenda kwa mtu mwingine ambaye hana hatia,”amesema Malewo.
NINI KIFANYIKE
Mbali na hilo, alitaja jambo la kwanza ambalo linapaswa kufanywa kukabiliana na tatizo hilo; ni watu kuyatambua maumivu yao ya kisaikolojia.
“Siku ya mwisho watu waelewe na waone kawaida kutokuwa sawa lakini pia, watafute msaada wakati wanapojiona hawawezi kusimama, kwa hiyo wanahitaji msaada kutoka nje,”alisema.
Alisema ufumbuzi mwingine ni kujifunza stadi mbalimbali za maisha, ukiwemo ujuzi wa kutatua matatizo mbalimbali.
“Hatua ya kwanza kabisa ni kutambua tatizo, kwa hiyo kuna stadi mbalimbali ambazo mtu anaweza kujifunza kutokana na nini anachokihitaji,”alisema.
Alisema jambo lingine ni mtu kujijenga katika ukomavu wa kihisia ambao utamsaidia kutambua hisia zake, za mtu mwingine na pia kuzimudu.
DK. HENGA
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, alisema miongoni mwa mambo ambayo yanachangia ni kuwepo mfumo wa maisha ambao unawachanganya watu wengi.
Mkurugenzi huyo alisema, sababu nyingine ni watu kutofahamu haki za wengine kutokana na kuhisi wanawamiliki wenzao.
“Unakuta mwanaume anahisi huyu mke wangu ninammiliki, kama ni mtoto wangu ninammiliki, kwa hiyo anahisi anaweza kumfanyia chochote kwa sababu yeye hafahamu kuwa kila mtu ana haki yake,”alisema Henga.
Dk. Henga alisema kuna haja ya kuwaelimisha watu masuala ya haki za binadamu, kwani yatawasaidia kuheshimu haki zao bila kuvunja za wengine.
“Ninachoona ni kuwa watu pia wasikubali haki zao kuvunjwa, ukiona watu wanaonewa watu wakaripoti katika kituo cha polisi, itasaidia kupunguza matukio hayo,”alisema.
TAKWIMU ZA NBS
Kwa mujibu wa Ripoti ya Takwimu za Unyanyasaji na Ukatili wa Kijinsia nchini Tanzania, ya Mwaka 2024 kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ukatili umeongezeka katika jamii huku Mkoa wa Dar es Saalam ukiongoza.
Ripoti hiyo inaonyesha idadi kubwa ya waathirika waliripotiwa katika Mkoa wa Dar es Saalam, ambao katika mwaka 2023 walikuwa 10,391 sawa na asilimia 27.7 ya waathirika wote, ukifuatiwa na Arusha wenye waathirika 4, 565 sawa na asilimia 12.2.




