Na MWANDISHI WETU
MAREKANI imeipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kwa hatua kubwa ya maendeleo, hususan katika ujenzi wa miundombinu.
Kauli hiyo ilitolewa na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Balozi Andrew Lentz, alipokutana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Ikulu Zanzibar.
Balozi Lentz alisema amefurahishwa na maendeleo ya Zanzibar hasa ujenzi wa miundombinu, akisema ni kipaumbele kwa nchi inayolenga kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi.
Pia, Balozi Lentz aliahidi kupanua ushirikiano na Zanzibar katika sekta za afya, mabadiliko ya tabianchi, biashara na uwekezaji.
RAIS DK. MWINYI
Kwa upande wake Rais Mwinyi, alisema Zanzibar ina mipango na mikakati madhubuti kuhakikisha inajitegemea na kujitosheleza katika nishati ya mafuta na umeme, kuwa kituo kikuu cha usafirishaji kupitia bandari kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Rais Dk. Mwinyi alisema ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani, unatarajiwa kumaliza changamoto zilizopo na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, ikiwemo mitambo ya megawati 200, matanki ya mafuta na bandari yenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa ambayo itaondoa msongamano wa Bandari ya Malindi.
Alisema ukuaji wa sekta ya uwekezaji nchini na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, umeifanya Zanzibar kutafuta njia mbadala za kujitegemea katika nishati ya umeme, mafuta, gesi na kuleta mageuzi katika ujenzi wa Bandari ya Mangapwani.
Pia, aliihakikishia Marekani kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali na kuishukuru kwa misaada yake kwa Tanzania, ikiwemo Zanzibar, akibainisha kuwa bado zipo fursa nyingi kwa kampuni na wawekezaji kutoka Marekani kuwekeza nchini.
BAADHI YA MIRADI
Katika kipindi cha Rais Mwinyi, barabara zimejengwa ikiwemo ujenzi wa flyover kutoka Mwanakwerekwe hadi Amani uliogharimu sh. bilioni 23.7 na Daraja la Uzi linalounganisha Unguja Ukuu na Kisiwa cha Uzi lenye urefu wa kilometa 2.2.
Pia, Rais Mwinyi amejenga miundombinu ya usafirishaji ya bahari, ukiwemo ujenzi wa Bandari ya Mangapwani, Bandari ya Fumba na Bandari ya Mpigaduli (Maruhubi).
Miradi mingine, Rais Mwinyi ametoa fedha za ujenzi wa shule mpya 60 zikiwemo 36 za ghorofa katika kila wilaya kwa lengo la kuondoa msongamano wa wanafunzi.
Pia, amejenga masoko makubwa kila wilaya yakiwemo Soko la Mwanakwerekwe, Jumbi, Mombasa na Chuini.
Katika hatua nyingine, Rais Mwinyi amelihakikishia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kuwa SMZ itaendelea kushirikiana na shirika hilo katika kuimarisha huduma za mawasiliano Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alisema hayo Ikulu, Zanzibar jana, alipokutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL, David Nchimbi, aliyekwenda kujitambulisha.
Rais Mwinyi alisema sekta ya mawasiliano ni muhimu katika kukuza uchumi wa kidijitali, kuimarisha huduma za kijamii zikiwemo za elimu, afya ya mtandao na kuchochea uwekezaji wa utalii Zanzibar.
“Tutahakikisha tunaimarisha huduma za mawasiliano kwa sababu zinaleta tija katika kukuza uchumi,”alisema Rais Mwinyi.
Rais Mwinyi alisema mawasiliano imara ni yenye uhakika na yatakayongeza ufanisi wa shughuli za Serikali, biashara na huduma kwa wananchi.
Naye Mwenyekiti wa bodi hiyo, alimshukuru Rais Mwinyi kwa ushirikiano mzuri unaoendelea kati ya shirika hilo na SMZ.
Nchimbi alisema TTCL itaendelea kutoa huduma bora na za kisasa kwa kukidhi mahitaji ya wananchi na kuchochea maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini.
Alimweleza Rais Mwinyi kuimarika mawasiliano Zanzibar, kutaleta manufaa makubwa kwa TTCL, yakiwemo kupanua wigo wa soko, kuongeza idadi ya wateja wa huduma za intaneti, mawasiliano ya simu na kukuza mapato ya shirika.




