Na MWANDISHI MAALUMU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan amesisitiza dhamira ya Tanzania ni kuendeleza uwekezaji wa kimkakati unaoendana na vipaumbele vya taifa.
Alisema hayo alipozungumza na Balozi wa Italia nchini, Giuseppe Sean Coppola, aliyemtembelea Ikulu, jijini Dar es Salaam, ambaye aliambatana na ujumbe kutoka Kampuni ya Danieli Group inayoongoza duniani katika teknolojia na uhandisi wa uzalishaji wa chuma.
Kampuni hiyo imeonesha nia ya kuchunguza uwezekano wa kuwekeza katika sekta ya chuma nchini kwa kujenga kiwanda cha kisasa na kikubwa cha chuma mkoani Mtwara, kwa kushirikiana na mwekezaji mzawa.
Ushirikiano huo unatokana na majadiliano ya awali yaliyofanyika wakati wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia, pamoja na mashauriano ya kitaalamu na taasisi za Tanzania, ikiwemo Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji Tanzania (TISEZA) na wizara husika.
Mradi unaopendekezwa, ambao bado uko katika hatua ya awali ya uchambuzi, unakadiriwa kugharimu takribani Euro bilioni 1.5 (sawa na sh. trilioni 4.2 za Kitanzania), unatarajiwa kutekelezwa kwa awamu kulingana na tathmini zaidi na taratibu za uwekezaji.
Rais Dk. Samia aliueleza ujumbe huo, Tanzania inaendelea kujijenga kama kituo shindani na cha kuaminika kwa uwekezaji, ikitegemea rasilimali zake asilia, nafasi yake ya kimkakati, pamoja na mageuzi yanayoendelea kuboresha mazingira ya biashara.
“Tunakaribisha ushirikiano unaoongeza thamani ya rasilimali zetu, unaozalisha ajira kwa wananchi wetu na kuchangia dira yetu ya muda mrefu ya kujenga uchumi wa viwanda,”alisema.
Rais Dk. Samia alimhakikishia Balozi Coppola na ujumbe wake, serikali itaendelea kuwa wazi kwa wawekezaji wenye sifa, wanaoleta siyo mtaji pekee, bali pia teknolojia, ujuzi na dhamira ya muda mrefu katika maendeleo ya Tanzania.
BALOZI COPPOLA
Kwa upande wake, Balozi wa Italia nchini, Coppola alisema ushirikiano huo unaakisi kuimarika uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Italia chini ya mifumo mipana ya ushirikiano wa maendeleo.
“Nia iliyooneshwa na Danieli Group ni sehemu ya juhudi pana za kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zetu mbili, ikiwemo kupitia Mpango wa Mattei kwa Afrika.
“Mpango huu unalenga kukuza uwekezaji endelevu na wenye manufaa kwa pande zote, Tanzania inaonekana mshirika muhimu katika muktadha huu.
“Kwa sasa, tupo katika hatua ya kuangalia uwezekano na tunatarajia kuendelea kushirikiana kwa karibu na serikali ya Tanzania kadri majadiliano yatakavyoendelea,” alisema.
DANIELI GROUP
Naye, Mtendaji Mkuu wa Danieli Group, Giacomo Danieli, alieleza sababu za kimkakati zilizoifanya kampuni hiyo kuvutiwa na Tanzania.
“Tunaona fursa kubwa nchini Tanzania, siyo tu kutokana na uwepo wa rasilimali kama gesi na madini ya chuma, bali pia kutokana na ukuaji wa soko na nafasi yake ya kimkakati katika ukanda huu.
“Mtazamo wetu unalenga ushirikiano wa muda mrefu kuleta teknolojia ya kisasa inayozingatia mazingira, huku tukishirikiana na wadau wa ndani kukuza ujuzi na kujenga uwezo endelevu wa viwanda.
“Hii ni hatua ya awali, tumejipanga kuendelea na majadiliano ya kitaalamu kutathmini uwezekano wa mradi huu,” alisema Danieli.
Iwapo utatekelezwa, uwekezaji huo utachangia kwa kiasi kikubwa katika ajenda ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda chini ya Dira ya Taifa ya 2050, kwa kuimarisha uzalishaji wa ndani wa chuma, kupunguza uagizaji kutoka nje, kuongeza thamani ya rasilimali za ndani na kutengeneza ajira kwa vijana.
Aidha, unaweza kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uzalishaji wa chuma katika ukanda huu, hususan kwa nchi jirani zisizo na bandari, pamoja na kusaidia maendeleo ya miundombinu na usafirishaji katika ukanda wa Mtwara.
Kikao hicho kilionesha kuendelea kuimarika mvuto wa Tanzania kama kituo cha uwekezaji na dhamira ya pamoja ya pande zote mbili kuendelea kuchunguza fursa zitakazozalisha thamani endelevu ya kiuchumi na ukuaji shirikishi.






