Na MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, amelitaka Jeshi la Polisi nchini, kuchukua hatua kali dhidi ya watu wanaodai kupotelewa sehemu zao za siri kwani kila aliyedai hivyo alipochunguzwa alikutwa nazo.
Katambi alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam, akiwa katika ziara ya Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, alipokwenda kukagua ajali ya moto iliyoteketeza vibanda zaidi ya 500 katika Soko la Mawasiliano Simu 2000 iliyotokea Aprili 4, mwaka huu.
Alisema baada ya kuibuka taarifa hizo potofu katika mikoa ya Mbeya na Songwe, Jeshi la Polisi nchini lilichukua hatua haraka.
“Jambo hilo limefanyiwa uchunguzi wa kina kupitia Jeshi la Polisi mara moja na kubainika kila aliyeshutumu nyeti zake kupotea alifanyiwa uchunguzi na ukaguzi ulibaini nyeti hizo zipo. Ilibainika ni uzushi na uongo uliosababisha kupoteza maisha ya watu.
“Ni mila potofu na uzushi unaoleta madhara makubwa kwa Watanzania, wapo watu wenye ualbino walipoteza maisha kwa kuamini wakiwachanja viungo vyao au kuchukua uhai wao baadaye unaweza kupata nafasi za kibiashara, uongozi au kushinda katika uchaguzi
“Sisi wote tulioingia katika siasa hakuna aliyeshinda kwa viungo hivyo na kama ingekuwa hivyo wote tungekuwa wabunge ama kupata nafasi ya uongozi,” aliongeza.
Katambi alisema jambo hilo ni uzushi ambao unapaswa kukemewa kwa sura zote za kidini, kimila na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kusimamia sheria.
Waziri huyo pia alitoa onyo kwa wananchi wanaoeneza uzushi kama huo au kuchukua sheria mkononi, kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Pia, alilitaka Jeshi la Polisi nchini kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wanaotoa taarifa za uzushi kupitia mitandao ya kijamii zinazohatarisha amani ya nchi.
MATUKIO
Juzi, Jeshi la Polisi nchini, lilitoa onyo kali dhidi ya wanaoendekeza upotoshaji na uzushi wa nyeti za wanaume kutoweka na kuusambaza katika mitandao ya kijamii, hali iliyosababisha madhara makubwa kwa watu na familia zao.
Polisi walielekeza kwa yeyote anayejirekodi, anayetengeneza vichekesho kwa kutumia uzushi huo na wanaosambaza nao wasakwe, wakamatwe kwa hatua za kisheria.
Onyo hilo lilitolewa kupitia taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime.
Kwa mujibu wa Misime, imani hizo potofu za uzushi na za kusingizia watu wengine mpaka hivi sasa zimesababisha vifo vya watu saba ndani ya siku nne na wengine majeruhi wakiendelea na matibabu hospitalini.




