Na NASRA KITANA
KOCHA wa Yanga, Pedro Goncalves, amewapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha kiwango kikubwa katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Pamba Jiji ambao kikosi hicho kilishinda 3-0.
Yanga ilicheza mechi hiyo juzi katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambapo miamba hiyo ilipata mabao yake kupitia kwa Mudathir Yahya aliyepachika mawili na Maxi Nzengeli.
Kocha Pedro alisema amefurahishwa na kiwango walichokionyesha wachezaji wake, lakini bado ana kazi ya kuboresha maeneo mbalimbali katika mechi zijazo.
Alisema kila mchezaji alionyesha uwezo mkubwa hatua ambayo imechangia kuondoka na pointi tatu muhimu.
“Tumeshinda na kupata pointi tatu, lakini niseme tu ukweli ni ngumu sana kucheza katika Uwanja wa CCM Kirumba, ila niwapongeze wachezaji wangu kwa kiwango kikubwa walichokionyesha kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Pedro.
Kocha huyo alisema ushindi huo wanauelekeza kwa mashabiki wao kutokana na sapoti kubwa wanayowaonyesha kuhakikisha wanashinda katika kila mchezo.
Naye Kocha wa Pamba Jiji, Francis Baraza alisema haelewi ni kitu gani kimewapata wachezaji wake hadi kuwa “wazito” kiasi cha kushindwa kufuata maelekzo na mpango kazi wa kiufundi waliokubaliana.
Alisema pamoja na ubora wa wapinzani, wachezaji wake wameshindwa kufuata kile ambacho amewafundisha.
“Kwa sasa nina kazi kubwa ya kwenda kufanya kurekebisha mapungufu yaliojitokeza katika mchezo huo, tunahitaji kupata ushindi katika mechi zinazofuata,” alisema.
Katika msimamo wa ligi hiyo, Yanga ipo kileleni ikiwa na pointi 44 huku Pamba Jiji ikishika nafasi ya sita kwa pointi 26 katika michezo 18.




