Na NASRA KITANA
BAADA ya kushindwa kupata ushindi dhidi ya TRA United, kocha wa Simba, Steve Barker amesema kuwa amesikitishwa na kiwango walichoonesha wachezaji wake.
Pia, amesema ana kazi ya kubwa ya kufanya kupata matokeo mazuri katika michezo ijayo.
Simba juzi ilikubali suluhu dhidi ya TRA United katika mchezo wake uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Barker alisema kuwa, wachezaji wake hawakuwa na mechi nzuri juzi.
“Sare mbili mfululizo siyo nzuri kwetu, lakini pia leo(Alhamisi) wachezaji wangu hakuwa bora, kiukweli nimesikitishwa na kiwango walichokionyesha.
“Nitapambana mwanzo mwisho kuhakikisha nafanya marekebisho katika kikosi changu tufanye vizuri katika mechi zinazofuata,” alisema.
Barker alisema atajipanga vizuri na viongozi wenzake wa benchi la ufundi kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza katika michezo ya hivi karibuni ambayo timu hiyo imecheza.
Aliongeza kuwa atahakikisha anafanya marekebishohasa sehemu ya ushambuliaji nafasi za kupachika mabao wazitumie vizuri.
“Tuna mechi nyingi bado, nataka kuona kikosi changu kinabadilika kiuchezaji na kuwa bora zaidi,”alisema.
Kocha huyo aliwaomba mashabiki wa timu hiyo, kutokata tamaa na kuwataka waendelee kuwapa sapoti ya kutosha kuwaongezea morari wachezaji wake wafanye vizuri.
Naye kocha wa TRA United, Ettiene Ndayiragije, alisema kuwa walicheza katika mchezo huo, kupata ushindi lakini bahati haikuwa yao.
Ndayiragije aliipongeza timu ya Simba kwa kuwapa mechi ngumu, lakini ameridhishwa na maendeleo ya kikosi chake.
“Sisi leo(Alhamisi) tulistahili kupata ushindi katika mchezo huu, lakini niwapongeze Simba kwa kutupa mechi ngumu, kikosi changu kwa sasa kimezidi kuwa bora na tutahakikisha tunafanya vizuri mechi zinazofuata,” alisema Ndayiragije.
Katika msimamo wa Ligi Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 36 huku TRA United ikishika nafasi ya saba na kujizolewa pointi 24 baada ya wote kushuka dimbani mara 18.




